Kuna watu wanafanya mambo ya ajabu kiasi kwamba unaanza kujiuliza hivi Mungu hawaoni watu hao ama vipi, wakati mwingine unaweza kuanza kujisemea labda wapo sawa ndio maana Mungu amewaacha.

Mungu kuwaacha watu wanaomtenda mambo yasiyofaa, sio kana kwamba Mungu amekubaliana na mambo mabaya wanayoyafanya. Mungu mwenyewe ameamua kuwaacha wafuate akili zao zisizofaa.

Kuna watu wakishaamua kufanya vitu, hata uende kuwaambia hichi mnachofanya sio sahihi, wataendelea kufanya hivyo hivyo. Hao Mungu amewaaacha wafanye yasiyofaa, kuwaacha hivyo sio kana kwamba wapo sawa.

Sasa kuna watu wakishaona watu fulani wanafanya mambo mabaya, mambo ambayo ni chukizo hata kwa jamii, wanaanza kuona labda wapo sahihi. Wanajiwa na mawazo hayo ya kuwa sahihi kutokana na wanaona Mungu yupo kimya juu yao.

Mungu ameamua mwenyewe kuwaacha wafuate akili zao, yaani Mungu ametupa uhuru wa kufanya kuchagua wenyewe. Unaweza ukawa unafanya mambo mabaya sana, usifikiri Mungu hakuoni, Mungu amekuacha ufanye unavyojua mwenyewe.

Unaweza kuona mtu fulani anafanya mambo mabaya ya kuua watu wengine, alafu mtu huyo unamwona kanisani tena ni muumini mwaminifu sana. Pamoja na uaminifu wake huo, nyuma ya pazia kuna mambo mabaya sana anafanya, anajua anachofanya, na Mungu ameamua kumwacha afanye yasiyofaa.

Rejea: Na kama walivyokataa kuwa na Mungu katika fahamu zao, Mungu aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wayafanye yasiyowapasa. RUM. 1:28 SUV.

Kuna watu wanakataa kabisa kumkiri Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wa maisha yao, wameamua kuabudu miungu yao, wameamua kuabudu sanamu. Sio kana kwamba Mungu hawaoni, bali Mungu amewaaacha wafuate akili zao zisizofaa.

Haijalishi wanajiona wapo sahihi, haijalishi wanaona wakiomba kwa miungu yao wanajibiwa, hiyo ni kwa sababu Mungu ameamua kuwaacha wafuate akili zao. Lakini Mungu akiamua kuwaangamiza anaweza kabisa, na ni jambo ambalo lipo ndani ya uwezo wake.

Mungu kukuacha uendelee kufanya mambo yasiyofaa, sio kana kwamba amekushindwa, au sio kana kwamba wewe unajua sana, wala sio kana kwamba unayofanya ni sahihi. Mungu amekuacha tu, ila usipobadilika na kuendana katika njia sahihi ikupasayo kuendana, uwe na uhakika siku ya mwisho hatakuonea huruma.

Umeamua kuishi na waume za watu, sio kana kwamba unafanya jambo zuri sana, Mungu amekuacha ufuate akili zako. Ila kama kuonywa umeonywa sana kuhusu hilo, na huenda umesoma Neno la Mungu lakini umepuuza.

Umeamua kumwacha mke wako nyumbani na kuwa na mwanamke mwingine wa nje, na unaona kwa huyo mwanamke hali ni shwari sana hadi unaanza kuona huyo ndiyo mwanamke wa kuishi naye. Sio kana kwamba unachofanya ni kizuri, ndio maana huoni madhara yeyote, ujue Mungu amekuacha ufuate akili zako za kipuuzi.

Wakati mwingine unaweza kujivuna na kuwaambia watu, kama ungekuwa unafanya dhambi, Mungu asingekuacha salama, huko ni kujipa tu moyo. Mungu mwenyewe anasema amekuacha ufuate akili zako za kipuuzi, sio kana kwamba unayofanya ni mazuri sana.

Jichunguze mwenyewe, kitu gani ambacho unajua unakifanya lakini moyoni mwako una uhakika kabisa ni chukizo mbele za Mungu. Hata kama unaona hali ni shwari, una uhakika hicho ukifanyacho ni chukizo mbele za Mungu, kiache mara moja na utubu mbele za Mungu.

Kama bado hujajiunga na kundi la wasap la kusoma Neno la Mungu kila siku, jiunge sasa kwenye kundi hili la kukujengea tabia ya kusoma Neno la Mungu. Tuma ujumbe wako kwa wasap namba +255759808081 utapewa taratibu zote za kundi hili la wasap.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com