Kuna watu ni hodari wa kuwafundisha wengine wazishike sheria za Bwana, wanawahubiri waache ulevi, waache kuiba, waache uzinzi, waache uasherati, waache kuabudu sanamu, lakini wao wenyewe wanafanya hayo hayo wanayowakataza wengine wasifanye.

Mzazi anamsihi sana mwanaye asije akawa mlevi, yeye mwenyewe ni hodari wa kunywa pombe, kama mzazi anaona pombe ina madhara kwenye maisha yake, kwanini yeye mwenyewe asiwe mfano wa kuacha hiyo pombe?

Mzazi anawafundisha watoto wake na kuwaonya wasijiingize kwenye ngono, alafu yeye mzazi ni hodari wa hayo mambo, tabia zake ni chafu kupindukia. Kwanini hayo mahubiri yasimsaidie yeye kwanza kabla hajaanza kufundisha wengine waache hayo.

Mtu anakuambia usiibe, wala usije ukajaribu kuiba kitu cha mtu, lakini yeye ni hodari wa kuiba, hiyo tahadhari anayokupa kwanini asijipe yeye na akaacha tabia ya kuibia watu. Kama ni tabia mbaya, kwanini yeye asiache kwanza ndipo aendee na wengine kuwaambia waache.

Rejea: Basi wewe umfundishaye mwingine, je! Hujifundishi mwenyewe? Wewe uhubiriye kwamba mtu asiibe, waiba mwenyewe? Wewe usemaye kwamba mtu asizini, wazini mwenyewe? Wewe uchukiaye sanamu, wateka mahekalu? RUM. 2:21‭-‬22 SUV.

Yamekushinda wewe, hiyo tabia unayokemea waumini wako, hiyo tabia unayokemea watoto wako, na hiyo tabia unayokemea kwa watu wengine wanaokuzunguka. Mbona wewe unaifanya, kama ni rahisi kuacha kwanini hujaanza wewe kuacha kabla hujamwambia mwingine aache?

Unapata wapi ujasiri wa kukemea uzinzi/uasherati wakati wewe mwenyewe unatembea na wanaume/wanawake hovyo, hata kama unatembea na mmoja sawa, kwani huyo mmoja ni mume/mke wako wa ndoa? Unajua kabisa sio mke/mume wako, bali unajua ni mke/mume wa fulani.

Unajua kabisa huyo bado ni mwanafunzi anasoma, lakini wewe unatembea naye kimapenzi, alafu ukisimama mbele za watu unawaambia wasiwe na tabia hiyo. Kama ni tabia mbaya na ni dhambi mbele za Mungu, kwanini wewe umeshindwa kuwa mfano bora, huna haja kuhangaika kuwahubiria wengine wawe watu wema wakati wewe sio mwema.

Huna haja ya kuwahubiria wengine amani, wakati ndani ya nyumba yako, au ndani ya ndoa yako ni uwanja wa vita humo ndani. Unampiga mke wako kisawasawa, una nyumba ndogo na mke wako yupo ndani, alafu ukikaa na wenzako unajifanya unampenda sana mke wako.

Kwenye mitandao ya kijamii unaonyesha unampenda sana mume/mke wako, mkiwa wawili hamuongei, kila mmoja ana chumba chake, mume wako akigusa unampa masharti utafikiri hajakuoa. Lakini ukiwa kwa wanawake wenzako unawafundisha kuwapenda waume zao, kwako umeshindwa kumpenda ila unawaambia wengine wawapenda waume zao!!

Rejea: Bali mtu asiye haki, Mungu amwambia, Una nini wewe kuitangaza sheria yangu, Na kuliweka agano langu kinywani mwako?   Maana wewe umechukia maonyo, Na kuyatupa maneno yangu nyuma yako.   Ulipomwona mwivi ulikuwa radhi naye, Ukashirikiana na wazinzi.  Umekiachia kinywa chako kinene mabaya, Na ulimi wako watunga hila. ZAB. 50:16‭-‬19 SUV.

Ndugu hadi hapo unaufanya moyo wako kuwa mgumu, hadi hapo unasema ina shida gani kumwambia mtu mwingine acha pombe na wakati wewe mwenyewe unakunywa. Labda unajitetea kwa kusema si vile umeona madhara yake, kama umeona madhara yake, bado una nafasi ya kurekebisha wewe mwenyewe mbele za Mungu. Kwanini sasa hutubu mbele za Mungu uache hizo njia chafu?

Siku ya harusi ya mwanao unampa mahusia mbele za watu wengi, ampende mume wake, amheshimu mume wake, awe mama bora wa familia, asiwe anatoa nje mambo ya ndani. Lakini wewe mwenyewe ni namba moja kwa kutomheshimu mume wako, wewe mwenyewe ni mvivu kupindukia hadi mtoto huyo kukua ulikuwa unamwachia dada wa kazi amlee, mtoto hakupata malezi ya mama.

Unamwambia mtoto wako anayeenda kuanza maisha ya ndoa asiwe anatoa nje mambo ya ndani ya ndoa yake, yaani ya mume wake; wewe mwenyewe ni fundi mzuri wa kuzungumza mambo ya mume wako kwa watu wa nje, wanajua madhaifu yote ya mume wako utafikiri wao ndio wanalala naye, kumbe umewaambia wewe mwenyewe.

Ukiwa kama kijana ukikutana na mama/baba anakufundisha tabia fulani, alafu unajua yeye mwenyewe yamemshinda, chunga sana hilo usije ukabeba matendo yake ukaacha maneno yake. Na kama wewe mwenyewe unatabia fulani mbaya alafu unawaambia wengine waache hiyo tabia, ujue unaweza ukawa unafanya kazi ya bure.

Matendo yako yana nguvu kuliko maneno, unaweza kuwa unawaambia watoto wako wasiwe na tabia fulani chafu, labda wawaepuke wanaume kama ukoma. Alafu wakati huo huo wanakuona mama yao unapishanisha wanaume tofauti tofauti ndani ya nyumba yako, ujue watakuona unachowaambia sio kweli.

Kwanini uwatwike wengine mizigo mizito iliyokushinda wewe mwenyewe, kwanini usianze mwenyewe kuacha hizo tabia mbaya. Uwe mfano basi wa kuigwa, acha pombe, acha wizi, acha kutembea hovyo na wanaume/wanawake, acha kuabudu sanamu.

Rejea: Basi, yo yote watakayowaambia, myashike na kuyatenda; lakini kwa mfano wa matendo yao, msitende; maana wao hunena lakini hawatendi. Wao hufunga mizigo mizito na kuwatwika watu mabegani mwao; wasitake wenyewe kuigusa kwa kidole chao. MT. 23:3‭-‬4 SUV.

Unaona hayo maandiko yote niliyokupa yanavyosema, usije ukafikiri ukiwa mwongeaji sana ndio utaweza kuwabadilisha watu, matendo yako yana nguvu kuliko maneno yako. Ukiwaambia watu acheni tabia fulani ni mbaya, ukawafundisha vizuri sana kwa ufasaha, alafu wakaja kukuta wewe mwenyewe huishi yale unawaambia, usifikiri watayafuata.

Haiwezekani nikawa nakusisitiza na kukufundisha umhimu wa kusoma Neno la Mungu kila siku, alafu mimi mwenyewe nikawa sisomi kabisa Neno la Mungu. Lakini unaniona kila siku nakuambia SOMA NENO UKUE KIROHO, kwanini nikutwishe mzigo ulionishinda mimi?

Tuache hizo tabia, kemea tabia ambayo wewe mwenyewe umeishinda, fundisha yale ambayo unayaishi, unaona huyaishi jifundishe kwanza na uanze kuyaishi ndipo uwaendee na wengine waache hayo mabaya.

Nakukumbusha kama bado hujajiunga na kundi la wasap la kusoma Neno la Mungu kila siku, nakusihi uchukue hatua ya kujiunga na darasa hili. Tuma ujumbe wako kwa wasap namba +255759808081 utapatiwa maelekezo mengine ya kujiunga na darasa hili.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com