
Tukitaka kuenenda kwa sheria hatutaweza, yapo mambo mengi sana tunaweza kufikiri tutaweza kuenenda kwa sheria ila ni ngumu sana kuenenda kama inavyotakiwa.
Sheria ilikuwa mtu akitenda dhambi iliyokatazwa, mtu huyo alipaswa kupigwa mawe mpaka kufa, hebu fikiri ni dhambi ngapi umemtenda Mungu. Kama sheria ingechukulia hatua, unafikiri ungekuwepo hai hadi leo? Bila shaka usingekuwepo.
Mungu wetu hatuhesabu kuwa tumetenda vyema kutokana na matendo ya sheria, tunahesabiwa haki kwa imani ya Yesu Kristo. Kumwamini kwetu Yesu Kristo ni ili tuhesabiwe haki kwa imani ya Kristo na si kwa matendo ya sheria.
Kama unafikiri unaweza kumpendeza Mungu kwa kuzishika sana sheria utakuwa unajidanganya sana, tena utakuwa haina maana kusema umeokoka. Tuliomwamini Yesu Kristo tunahesabiwa haki kwa imani ya Kristo, na si kwa matendo ya sheria.
Unapaswa kuelewa hili ndugu, pasipo kuelewa hili unaweza ukawa unaishi kwenye kifungo kigumu sana cha sheria huku unasema umeokoka na Yesu Kristo ni Bwana na mwokozi wa maisha yako.
Unachopaswa kuelewa ni kwamba tunahesabiwa haki kwa imani ya Kristo, na si kwa matendo ya sheria, unapoelewa hili itakusaidia kusimama vizuri na Mungu wako ukijua utahesabiwa haki kwa imani ya Kristo.
Rejea: Basi, twaona ya kuwa mwanadamu huhesabiwa haki kwa imani pasipo matendo ya sheria. RUM. 3:28 SUV.
Weka hili akilini mwako, hatuhesabiwi haki kwa matendo ya sheria, bali tunahesabiwa haki kwa imani ya Kristo, hatupaswi kufungwa na matendo ya sheria. Maana haitatusaidia chochote, sisi kama wakristo tunahesabiwa haki kwa imani ya Kristo.
Huwezi kuhesabiwa haki kwa matendo ya sheria ukapona, hasa ukiwa na huu mwili wa nyama ni vigumu sana. Tunachopaswa ni kuhakikisha tunaimarisha imani yetu kwa Yesu Kristo, maana ndipo tutakapohesabiwa haki kwa imani ya Kristo.
Na imani yako inakua na kuimarishwa zaidi kwa kulisoma Neno la Mungu, Neno la Mungu ndio linakujenga na kukuweka imara katika maisha yako ya wokovu.
Rejea: Hali tukijua ya kuwa mwanadamu hahesabiwi haki kwa matendo ya sheria, bali kwa imani ya Kristo Yesu; sisi tulimwamini Kristo Yesu ili tuhesabiwe haki kwa imani ya Kristo, wala si kwa matendo ya sheria; maana kwa matendo ya sheria hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki. GAL. 2:16 SUV.
Kama unataka uhesabiwe haki kwa matendo ya sheria huna haja ya kumpokea Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wa maisha yako, maana tumemwamini Yesu Kristo ili tuhesabiwe haki kwa imani ya Kristo.
Ndivyo maandiko matakatifu yanavyosema hapa, hata kama unakataa na kusema kwamba lazima mtu huhesabiwa haki kwa matendo ya sheria. Utakuwa unaenda kinyume na Neno la Mungu, hili ndilo limetuambia haya ninayokueleza hapa.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com