Linaweza likawa swali gumu kwako kujibu haraka, au linaweza likawa ni swali rahisi kwako kujibu, au unaweza kufikiri haraka kuwa ni swali rahisi kwako kujibu ila ukikaa ukitulia majibu ya awali yanaweza kubadilika yakawa mengine.

Imani sio kitu kinachoonekana na watu wengine kwa macho, wakati wengine hawaoni chochote wewe unakuwa na imani ndani yako itakuwa, wakati wenzako wamevunjika moyo na kuona hakuna kitakachoweza kutokea wewe unakuwa na imani ndani yako itaweza kutokea.

Kuna vitu unaweza ukawa na imani navyo ndani yako hadi ukimshirikisha mtu mwingine anaweza kukuona umechanganyikiwa kabisa kutokana na hali uliyonayo, au kutokana na uhalisia wa jambo lenyewe lilivyo.

Vipimo vyote vinaweza kuonyesha kabisa umri wako wa kuweza kupata mtoto haupo tena, na jamii inajua ukishakuwa na umri fulani unakuwa huna uwezo tena wa kubeba mimba, na kama mwanaume uwezekano wa kupata mtoto unakuwa haupo tena.

Alafu wakati huo unajua hayo, unamwambia mtu una imani utapata mtoto kwenye umri wako ule ule wa uzee, unapigilia msumari zaidi wa maneno kwa kumwambia mtu huyo kabla ya kufa lazima unyonyeshe mtoto wako. Na unawaambia watu kupitia mke wako huyo huyo mzee na wewe ni mzee, una imani mtapata mtoto.

Wakati wao wana imani dhaifu, imani isiyo na uhakika kama inawezekana ikatokea kitu kama hicho, wewe unakuwa imara katika kile unakiona ndani yako kinawezekana kutokea/kutendeka. Watu wengine wakati wanafikiri unatania wewe unakuwa unajua unamaanisha.

Yapo mambo magumu hata yule unayemjua ni mcha Mungu katika roho na kweli, yapo mambo anaweza asiwe na imani kabisa kama yanawezekana. Lakini kwako unakuwa unaona inawezekana kabisa ikatokea kwako, unakuwa huna mashaka kwa hilo.

Sasa wapo watu wengine wao wanakuwa tofauti kabisa, wakati wengine wanakuwa wana imani inawezekana, wao wanakuwa wanajua haiwezekani kabisa. Kwahiyo hapo wanakuwa wanapishana na wenzao, wao wanakuwa hawaamini, wenzao wanakuwa wanaamini, unaona inavyokuwa ngumu hapo.

Nasema inakuwa ngumu kwa sababu inaweza ikawa wale wanaoamini inawezekana, wanakuwa hawamfahamu huyu ndugu anayeona haiwezekani kabisa. Anaweza kukosa kile alichokuwa anakihitaji na akatoweka Duniani akiwa hajakipata kile alichokuwa anakihitaji, lakini yeye mwenyewe angekuwa ana imani ilikuwa ni rahisi kupokea hitaji la moyo wake kabla ya kufa.

Sasa wapo ambao wana imani inawezekana ila wanakuwa na imani dhaifu, leo wanaamka wanaona inawezekana kabisa kwa Mungu, kesho wakiamka wanaona haiwezekani kabisa labda kutokana na hadithi walizozisikia kwa watu.

Watu wa namna hii wapo wengi sana makanisani, watu ambao leo wanakuwa na imani, kesho ikifika wanakuwa hawana imani kabisa, watu hawa wana imani dhaifu. Watu ambao wanakuwa na hoja nyingi sana, ukiwagusa wanakuwa na maneno mengi kiasi kwamba unachoka ukianza kuwasikiliza.

Rejea: Yeye asiyekuwa dhaifu wa imani, alifikiri hali ya mwili wake uliokuwa umekwisha kufa, (akiwa amekwisha kupata umri wa kama miaka mia), na hali ya kufa ya tumbo lake Sara. RUM. 4:19 SUV.

Kupitia hilo andiko, imani yako ni dhaifu au sio dhaifu, vuta picha ya jambo moja tu ulilowahi kuwa na imani linawezekana, alafu baadaye ile imani imetoweka kabisa ndani yako. Japokuwa mdomoni unatamka kabisa inawezekana ila moyoni mwako unasema haiwezekani kabisa ila unasema tu.

Baba yetu wa imani Ibrahim hakuwa dhaifu wa imani, alikuwa na uhakika wa kile Mungu alimwambia, jambo ambalo hata kwetu leo linawezekana, jambo ambalo kwako leo linawezekana kabisa.

Pale unapochoka huwa unatazama ahadi za Mungu? Maana kupitia kuzitazama ahadi za Mungu kwetu ndipo tunatiwa nguvu za kuendelea kuamini inawezekana kabisa, hata kama imechelewa.

Rejea: Lakini akiiona ahadi ya Mungu hakusita kwa kutokuamini, bali alitiwa nguvu kwa imani, akimtukuza Mungu; huku akijua hakika ya kuwa Mungu aweza kufanya yale aliyoahidi. RUM. 4:20‭-‬21 SUV.

Hebu jihoji mwenyewe, hapo ulipo sasa bado una uhakika Mungu atafanya? Ni miaka mingi sana imepita sawa, je bado imani yako ni ile ile au imekuwa imani dhaifu. Imani isiyo na matumaini ya kupokea kitu chochote kwa Bwana.

Bado una imani kama ya Ibrahim, mtu aliyefikisha miaka mia moja bila kuwa na mtoto, mtu ambaye alikuwa na mwanamke tasa, wala haikuwa siri, mke wake Sara alikuwa anajulikana ni tasa, tena mwenye umri wa kutosha.

Pamoja na Sara kuwa tasa, na pamoja na Ibrahim kuwa mzee wa miaka 100, imani yake haikuwa dhaifu, alipotazama ahadi za Mungu, maandiko yanasema hakusita kwa kutokuamini, bali alitiwa nguvu kwa imani, na kuwa na uhakika Mungu anaweza kufanya yale aliyoahidi.

Wewe kama wewe unaona ahadi za Mungu kupitia nini? Je kupitia usomaji wako wa Neno la Mungu au kwa kusikia maneno ya watu wengine. Kama husomi neno la Mungu unasikia tu shuhuda za wengine ni hatari sana kwako, maana unaweza kufika mahali ukachoka kusubiri, maana imani yako haikuwa na mizizi ya Neno la Mungu. Lakini ukiwa na maandiko ya kutosha ndani yako, unakuwa na uhakika alichosema Mungu kwako kitatimia.

Hakikisha unasoma Neno la Mungu kila siku, na kama hili ni changamoto kwako, karibu sana uungane na marafiki wazuri wanaopenda kusoma Neno la Mungu. Tuma ujumbe wako kwa wasap namba +255759808081 ili uweze kuunganishwa na kundi hili la marafiki wanaosoma Neno kila siku, nami nitakuwa karibu nawe kuhakikisha unasoma Biblia.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com