Zipo nyakati ukimtazama mtu unayemfahamu unajikuta unaumia sana moyoni, kinachokufanya uumie sio kana kwamba kuna jambo baya amekufanyia. Hakuna baya alilokufanyia bali vile ulivyokuwa unamfahamu ni mtu anayejituma sana, alafu ghafla ukawa unamwona sio yule wa mwanzo, lazima ikuumize.

Wapo watu walikuwa ni watu wenye bidii sana kwa mambo ya Mungu, watu ambao ulikuwa ukiwatazama hadi unapata hasira ya hali uliyonayo ya uvivu, watu ambao ulikuwa ukiwatazama unasikia kuinuka kwa upya ndani yako.

Watu ambao ulikuwa ukiwatazama jinsi wanavyojitoa kwa Mungu unajiona kabisa moyoni mwako bado hujajitoa vizuri kama inavyotakiwa, ni watu ambao walikuwa hawana mchezo kabisa wanapofika kwenye eneo la kutumika.

Watu ambao walikuwa hawana muda wa kupoteza inapofika saa ya kwenda kwenye ibada, kama ulikuwa mahali umekaa unapomwona unajua kabisa huyo ndugu anawahi kwenye ibada. Hata wewe ambaye ulikuwa unajisikia kutokwenda kwenye ibada unajikuta unanyanyuka.

Watu ambao walikuwa wasomaji wazuri wa Neno la Mungu, wakianza kukuambia uzuri wa Neno la Mungu, wakianza kukuambia vile Neno la Mungu limewasaidia, wakianza kukuambia vile Neno la Mungu limewabadilisha. Ndani yako ulikuwa unajisikia kuhukumiwa kutokana na uzembe wako wa kutokusoma Neno la Mungu.

Lakini pamoja na kuwafahamu hao watu wenye bidii hizo zote, wamefika mahali hawafanyi kama ilivyokuwa awali, yaani kila ukiwaangalia huamini unachokiona kwao. Ile bidii yao iliyokufanya hadi wewe ukapata hasira ya kuachana na uzembe/uvivu, haipo tena ndani yao.

Wamechoka kiasi kwamba unakosa hata neno zuri la kuwaambia, wakati mwingine umeshindwa kuvumilia na kuwauliza vipi mbona mpo hivi. Lakini pamoja na kuwaambia hivyo, sababu wanazokueleza unaona kabisa sio kitu kikubwa sana cha kuwafanya wawe na hali hiyo.

Kuchoka wamechoka, ule ushawishi wao mkubwa juu ya mambo mazuri haupo tena ndani yao, ulikuwa unamwona mtu anahimiza sana wengine kusoma Neno la Mungu. Baada ya muda fulani kupita, yeye mwenyewe amegeuka na kuwa mtu ambaye anahitaji msaada wa kuhimizwa kwa nguvu asome Neno la Mungu.

Hebu jiangalie hapo ulipo, bidii uliyonayo sasa ipo vile vile, au imepanda juu zaidi, au imeshuka chini zaidi, au haipo kabisa kwako, upo wapi, ulivyoanza na ulivyo sasa. Unaona una hatua unapiga au unaona kabisa kadri siku zinavyozidi kwenda mbele hali yako ya kiroho inazidi kushuka chini zaidi.

Fahamu kwamba Mungu hataangalia mwanzo wako mzuri, haijalishi ulikuwa na bidii sana ya kumcha Mungu, haijalishi ulikuwa msomaji mzuri sana wa Neno la Mungu, Mungu anachoangalia ni mwisho mwema.

Rejea: Heri mwisho wa neno kuliko mwanzo wake, Na mvumilivu rohoni kuliko mwenye roho ya kiburi. MHU. 7:8 SUV.

Kama umepita kwenye hali fulani ngumu, alafu hiyo hali imekuondoa kabisa kwenye bidii yako, huna tena ule msukumo wa kufanya mambo mazuri ya kiMungu. Ile bidii yako uliyokuwa nayo haipo tena, umebaki kama mtu tu anayesema ameokoka, unaenda ilimradi kumekucha.

Kuanzia sasa kataa hiyo hali kwa kumwambia Yesu Kristo, mwambie akupe nguvu mpya, usikubali kurudi nyuma wakati unapaswa kwenda mbele. Mbaya zaidi Mungu hataangalia mwanzo wako mzuri, Mungu ataangalia mwisho wako mzuri.

Kama ulikuwa na bidii sana, hiyo bidii inapaswa kuonekana kwako kila siku, hupaswi kupungua bali unapaswa kuongezeka viwango vya juu zaidi. Kadri watu wanavyozidi kukuona, kila siku wanaona mabadiliko mapya ya kiungu ndani yako.

Usichotwe na hali yeyote ya udhaifu ukarudi nyuma, linda sana moyo wako, unapofika mahali unajiona huna hamu tena na kile ulikuwa unafanya, tafuta kujua chanzo ni nini. Ukishajua shughulika na hicho chanzo, kama kipo ndani ya uwezo wako kiondoe, na kama kipo nje ya uwezo wako mwambie Yesu akutie nguvu usije ukarudi nyuma.

Tabia ya kuinuka kwa kasi kubwa alafu baada ya muda unarudi nyuma kama hukuwahi kuwa mtu mwenye kufanya jambo fulani, huko sio kuzuri, bidii yako inapaswa kuendelea kuonekana matunda yake hata kama hutokuwepo duniani.

Kama ulikuwa bado hujajiunga na kundi letu la wasap la kusoma Neno la Mungu kila siku, nakukaribisha sasa uchukue hatua ya kujiunga na kundi hili la wasap la kusoma Neno. Tuma ujumbe wako kwa wasap namba +255759808081 utapatiwa taratibu zingine za kuweza kuendana na kundi.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com