Kinachotufanya tuishi maisha ya kumpendeza Mungu sio uwezo wa akili zetu tulizonazo, hili tunapaswa kulifahamu ili tuache kufikiri wanaoishi maisha ya kumpendeza Mungu wana uwezo fulani waliozaliwa nao kushinda dhambi.

Unaweza ukamwona mtu ameokoka vizuri na ametulia, unaweza ukawa na mawazo potovu juu yake kwa kufikiri anadanganya, hii inakuja pale unapojitahidi kuacha tabia fulani mbaya. Inakuwa inakushinda kuacha, kila ukijaribu kuacha hiyo tabia, unajitahidi labda mwezi mmoja ila baada ya hapo unajikuta umerudia kile kile.

Unapoangalia wengine wanavyoenenda vizuri, unaanza kuwaona hawawezi kuishi maisha ya kumpendeza Mungu lazima kuna mahali watakuwa wanamkosea ila kwa siri. Au unaweza kufikiri labda wao Mungu amewaumba kwa namna ya tofauti kuweza kushinda dhambi.

Kinachomfanya mtu achukie dhambi kwa vitendo, na kinachomfanya mtu aishi maisha ya kumpendeza Mungu, fahamu mtu huyo anakuwa amempokea Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wake.

Utasema mbona mimi ni mkristo kabisa ila kuna dhambi nimeshindwa kuiacha, kabla sijakujibu moja kwa moja, hebu jiulize kwanza kweli unamaanisha ndani ya moyo wako, maana kila mtu anaweza kujiita mkristo ila ndani ya moyo wake hayumo Kristo.

Ukiri wako unapaswa kumaanisha kutoka ndani ya moyo wako, unaweza ukawa ni mkristo jina ila hufanyi vile vitu vya kukufanya uimarike kiroho. Huenda ni mkristo ila huna muda wa kuhudhuria mafundisho ya Neno la Mungu, huenda ni mkristo huna muda wa kufunga na kuomba, huenda ni mkristo ila una marafiki wasiofaa.

Mbaya zaidi unasema wewe ni mkristo ila huna muda kabisa wa kusoma Neno la Mungu, ila kwa sababu uliongozwa sala ya toba ukaona imetosha, huenda kwa sababu unahudhuria kanisani siku za jpili unafikiri ndio utaweza kushinda dhambi.

Tunapompokea Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wetu, tukaendelea kuishi maisha matakatifu ya kumpendeza Mungu, tunakuwa tumekufa pamoja na Kristo katika dhambi. Maana yake ile tamaa ya kutamani vitu visivyofaa inakuwa haimo ndani yako tena.

Unaweza ukamwona mtu alikuwa anatenda mambo mabaya sana, lakini alivyompokea Yesu Kristo moyoni mwake kwa kumaanisha kweli. Ile tabia yake mbaya ilibadilika kabisa, unaweza kufikiri labda anaigiza ila fahamu ni ukweli kabadilika.

Rejea: Na Kristo akiwa ndani yenu, mwili wenu umekufa kwa sababu ya dhambi; bali roho yenu i hai, kwa sababu ya haki. RUM. 8:10 SUV.

Unaona hilo andiko linavyosema, kumbe Kristo akiwa ndani yetu, miili yetu inakuwa imekufa kwa sababu ya dhambi. Kwa maneno mengine tunakuja kuifufua dhambi ndani yetu kwa kumwondoa Yesu Kristo kwa matendo yetu machafu.

Lakini Kristo akiwa ndani yetu, miili yetu inakuwa imekufa kwa habari ya dhambi, huwezi kutamani sigara Yesu Kristo akiwa ndani yako, huwezi kutamani pombe Yesu Kristo akiwa ndani yako, huwezi kutamani uasherati/uzinzi Yesu Kristo akiwa ndani yako, huwezi kutamani kuiba kitu cha mtu Yesu Kristo akiwa ndani yako.

Usishangae unamwona mtu aliyeokoka sawasawa hana parapara na vitu vibaya vinavyokutesa wewe, unaweza kufikiri labda kutokana na uwezo fulani ambao amezaliwa nao. Ukweli ni kwamba hakuna uwezo wowote aliozaliwa nao, isipokuwa amekubali Kristo awe ndani yake.

Rejea: Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu. RUM. 8:14 SUV.

Ukitaka kushinda dhambi unapaswa kuokoka sawasawa, yaani kwa kumaanisha kweli, na unapaswa kujazwa Roho Mtakatifu, maana pasipo kuongozwa na Roho wa Mungu napo ni shida.

Na ukishaokoka unapaswa kujibiidisha katika kusoma Neno la Mungu. Neno la Mungu linapaswa kuwa kwa wingi moyoni mwako, bila Neno la Mungu napo utarudi nyuma tu.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com