
Mungu wetu hana upendeleo, wale wanaompenda huenda nao, na wale wanaomkataa huwaacha wafuate akili zao, hakuna mtu ambaye analazimishwa katika hili. Kila mmoja anao uchaguzi wa kuchagua amfuate nani, Yesu Kristo au shetani.
Tunaweza kuona Mungu ametuacha peke yetu, bila kuelewa ni kutokana na sisi kujitenga naye kwa matendo yetu mabaya. Mungu anakuwa amejitenga nasi kutokana na kumkataa Yesu Kristo na kufuata yale yasiyompendeza yeye.
Tofauti kabisa na mtu ambaye alikuwa hajaokoka, akaamua kuchukua hatua akaokoka, mtu huyo anakuwa na uhakika wa maisha yake, akiwa duniani na baada ya kuondoka hapa duniani.
Mtu akiwa duniani akawa hana uhakika na usalama wa maisha yake, na akawa hataki kumpokea Yesu Kristo, ama akawa anasema amempokea Kristo ila matendo yake yakawa yanaonyesha dhahiri ni mtu asiye na Yesu moyoni. Mtu huyo itafika wakati ataenda kutafuta usalama wa maisha yake kwa miungu mingine.
Upo wakati utafika atafuta msaada kwa miungu mingine, kwa sababu atafika mahali ambapo anahitaji msaada wa Mungu, hataweza kuupata kwa kukataa kwake kuenenda vile anapaswa kuenenda sawasawa na maelekezo ya Mungu.
Mtu ambaye ameokoka sawasawa, Yesu Kristo ni Bwana na mwokozi wa maisha yake, anaenenda katika imani ya Kristo, mtu huyo Mungu hufanya naye kazi. Ndivyo maandiko matakatifu yanavyosema, tena anasema wale wanaompenda huwapatia mema.
Rejea: Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake. RUM. 8:28 SUV.
Ukiwa umeokoka, hupaswi kuogopa chochote, maana una uhakika wa maisha yako, sio uhakika tu, unakuwa unajua usalama wa maisha yako ni wa uhakika. Sio usalama tu, unakuwa unajua mema anayoachilia kwa watu wake nawe lazima yakupate.
Upendo wako kwa Mungu sio wa bure, upendo wako kwa Mungu unakufanya Mungu afanye kazi nawe katika kukupatia mema, mema yako yanakujilia kwa sababu ya kumpenda Mungu wako.
Unapompenda Mungu huwezi kumtenda dhambi, kama unasema unampenda Mungu alafu unaenda kinyume na maagizo yake, huko ni kumpenda kwa maneno ya mdomoni ila matendo yako yanaonyesha unamkataa.
Jihakikishie usalama wa maisha yako kwa kumpenda Mungu, yaani kumpokea Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wa maisha yako. Baada ya kumpokea na kujazwa na Roho Mtakatifu, enenda katika kutenda yale yanaonyesha unampenda kweli Mungu, utaona mema yakikujilia kwenye maisha yako.
Unataka kuendelea kujua ahadi za Mungu, na vile Mungu anatenda kazi juu ya maisha yako? Karibu ujiunge na kundi letu la wasap la kusoma Neno la Mungu kila siku, tuma ujumbe wako wasap namba +255759808081.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com