Katika maisha ya kawaida kabisa, mtu anaweza akawa mwenye bidii sana katika jambo fulani au katika kazi fulani, juhudi zake nyingi zinaweza zisimzalie matunda yeyote kutokana na kukosa maarifa sahihi ya kufanya hicho anachofanya.

Anaweza akatumia nguvu kubwa kufanya kazi kubwa sana, akajikuta amepata matunda kidogo sana au asipate kabisa matunda yeyote yanayotokana na kazi yake kubwa aliyofanya.

Yupo mtu mwingine akawa ana maarifa/ufahamu wa kutosha kuhusu kile anachokifanya, akafanya kazi kubwa sana, na hiyo kazi ikazaa matunda mazuri kwa sababu alikuwa na maarifa sahihi ya kufanya hicho alichokuwa anafanya.

Kuna wakati tunatumia nguvu kubwa sana kufanya mambo mengi makubwa ila kwa kukosa maarifa sahihi tumejikuta tunavuna matunda kidogo sana, wakati mwingine hatuvuni kabisa chochote. Tumebaki tukilalamika wenyewe au tumebaki tukilaumu wengine.

Kuwa na maarifa sahihi kwa unachokifanya ni jambo la msingi sana, kuwa na maarifa sahihi na ya kutosha kwa kile unachokiamini ni jambo la msingi sana. Kwanini ni jambo la msingi sana kuwa na maarifa sahihi na ya kutosha kwa kile unakiamini?

Zipo sababu nyingi sana, ila nitakueleza sababu chache za muhimu sana ambazo zinaweza kukusaidia katika maisha yako ya kiroho na kimwili. Maana wengi tumeenda kwa kufuata wengine pasipo kukaa chini kujifunza kwa kile tunakifanya au kwa kile tunaamini.

Wapo watu wanaamini wanamwabudu Mungu wa kweli, lakini ukweli ni kwamba hawamwabudu Mungu wa kweli, bali wanaabudu miungu mingine.  Sio kana kwamba wanaigiza katika hilo, ufahamu wao na kukosa kwao maarifa sahihi wanaona wapo sawa kabisa.

Ndio maana unaweza kumwambia mtu acha kuabudu sanamu ni chukizo mbele za Mungu, anaweza asikuelewe kabisa kama hutompa elimu sahihi ya kumfanya aone anachofanya sio sahihi. Ama unaweza ukampa elimu ya kutosha ila kutokana na maarifa potovu aliyonayo juu ya kile anakiamini anaweza asikuelewe kabisa.

Lakini pamoja na kutokuelewa bado ataona wote mnamwabudu Mungu mmoja, lakini sio kweli mnamwabudu Mungu mmoja, kukosa kwake maarifa sahihi ndio kunamwaminisha kuwa wote mwanabudu Mungu mmoja.

Hujawahi kuona watu wanasema ya nini kugombana wakati wote tunamwabudu/tunamwamini Mungu mmoja, hata yule ambaye anaabudu mizimu ya mababu zake naye anasema mnamwabudu Mungu mmoja, hata yule ambaye anasujudia sanamu naye atakuambia mnamwabudu Mungu mmoja.

Wapo wengine wanaabudu ng’ombe, waamini kupitia huyo ng’ombe Mungu anawasikia maombi yao, wapo wanaabudu jua na wao wanaamini Mungu wao ni yule yule wanaomwabudu wengine. Ni kama vile inachanganya sana ila ukweli ni kwamba shetani ameteka ufahamu wao, kwa sababu ya kukosa kwao maarifa sahihi ya Neno la Mungu.

Watu wanaweza wakawa na juhudi kubwa sana kwa ajili ya Mungu, lakini si katika maarifa sahihi, ukiwabana vizuri wathibitishe kile wanakifanya watashindwa. Kama watakujibu watajibu majibu yanayoonyesha wamepotea njia sahihi.

Rejea: Kwa maana nawashuhudia kwamba wana juhudi kwa ajili ya Mungu, lakini si katika maarifa. Kwa maana, wakiwa hawaijui haki ya Mungu, na wakitaka kuithibitisha haki yao wenyewe, hawakujitia chini ya haki ya Mungu. RUM. 10:2‭-‬3 SUV.

Unaona hayo maandiko matakatifu, unaweza kumwona mtu anajiweka mbali na baadhi ya mambo, unaweza kumwona mtu, ni mtu wa kuzingatia sheria sana za dini yake. Kwa uchanga wako wa kiroho au kwa kukosa kwako maarifa sahihi ya Neno la Mungu, ukawa unamwona huyo ndiye atakayeingia peponi.

Kumbe pamoja na kujitahidi kuenenda katika sheria za dini yake, mtu huyo hakujitia chini ya haki ya Mungu, lakini yeye anajiona yupo sahihi sana kupita wengine ambao hawaendi kama yeye.

Rejea: Kwa maana Kristo ni mwisho wa sheria, ili kila aaminiye ahesabiwe haki. RUM. 10:4 SUV.

Ndugu, usipuuze maarifa ya Neno la Mungu, unapoambiwa soma Neno la Mungu usione ni jambo ambalo linamletea mtu mwingine manufaa. Kusoma kwako maandiko matakatifu kunakufanya ujue mahali ulipo ni sahihi? Kunakufanya ujue misimamo ya dini yako uliyonayo ni sahihi? Kile unachokifanya na unajua utapata malipo yake mbinguni ni kweli kipo sahihi?

Lazima ukae chini upate maarifa sahihi, na maarifa sahihi yanapatikana ndani ya Biblia yako, kama huna Biblia kanunue uisome. Maana kila aaminiye moyoni mwake Yesu Kristo ni Bwana na mwokozi wa maisha yake, na Mungu alimfufua katika wafu, huyo atahesabiwa haki.

Kama bado hujajiunga na kundi la wasap la kusoma Neno la Mungu kila siku, chukua hatua sasa ya kuwasiliana nasi kwa namba hii +255759808081 ili uweze kuunganishwa.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com