Vipo vitu vya pekee sana ambavyo wanavyo baadhi ya watu waliompokea Yesu Kristo kama na mwokozi wao, vitu ambao vinakuwa vya kipekee sana hadi vinatia wivu kwa wengine.

Upekee huu hauji hivi hivi kwa mtu, ni mpaka pale mtu huyo anapoamua kujikabidhi mbele za Mungu, yaani pale anapoamua maisha yake yote yanapaswa kuongozwa na Mungu.

Mtu aliyeamua maisha yake ayakabidhi kwa Yesu Kristo, kila jambo ambalo atataka kulifanya lazima amtangulize kwanza Yesu Kristo. Mtu huyo hawezi kufanana na wengine, lazima awe na upekee wa namna yake, upekee ambao watu wengine wasiomjua Kristo au wale walio nusu nusu kwa Yesu hawezi kuwa nao.

Unaweza ukamwona mtu fulani unayemfahamu siku nyingi sana ila akawa mtu ambaye ana utofauti ambao hata wewe unashindwa kuelewa umetokana na nini. Usipate shida shida kwa hilo fahamu kwamba, mtu huyo ameamua kumkabidhi Yesu Kristo maisha yake.

Hajamkabidhi kwa maneno tu, ameamua kujitoa kisawasawa kwa Yesu Kristo, wakati wengine wanaitwa wakristo majina ila matendo yao yanamkataa Yesu Kristo. Wapo ambao wamejitoa kweli kweli kwa Yesu Kristo, hawana mchezo kabisa na maisha yao ya wokovu.

Watu wengine wanapoona upekee fulani kwa mtu aliyeokoka sawasawa, huwa wanaanza kutafuta namna na wao kuwa hivyo. Wanaweza wasielewa upekee wa wale watu umetokana na nini wakabaki wanahaingika tu.

Kuhangaika kwao kunaweza kusiwe na matunda mazuri, kwa sababu hawajajua siri ya watu wale upekee wao umetokana na nini. Wengine hufika wakati wanaanza kuiga kila kitu cha yule anachofanya, lakini pamoja na kuiga wanajikuta hawaonekani kama wale wanaowaiga.

Upo upekee wa namna ya kufundisha Neno la Mungu ambao hutaupata mpaka ujiungamanishe vizuri na Mungu wako, utahangaika sana kama uhusiano wako na Yesu Kristo haupo sawa. Huwezi kupata upekee unaoutaka wewe.

Upo upekee wa namna ya kuhubiri, kuimba, kufundisha, kuomba, hutokaa uupate hadi ujue maandiko matakatifu. Pale maarifa ya Neno la Mungu yatakapojaa kwa wingi moyoni mwako, utaanza kuona namna uimbaji wako, ufundishaji wako, uombaji wako, na uhubiriji wako unavyobadilika.

Upo upekee hutokaa uupate hadi ukubali kuzaliwa mara ya pili, haijalishi unaonyesha kumpenda sana Yesu Kristo, kama kuna matendo machafu unayafanya gizani ujue Yesu hayumo ndani yako.

Rejea: Imekuwaje basi? Kitu kile ambacho Israeli alikuwa akikitafuta hakukipata; lakini wale waliochaguliwa walikipata, na wengine walitiwa uzito. Kama ilivyoandikwa, Mungu aliwapa roho ya usingizi, macho hata wasione, na masikio hata wasisikie, hata siku hii ya leo. RUM. 11:7‭-‬8 SUV.

Unaona hapo, wale waliochagulia ndio walikipata kile ambacho wengine walikitafuta wakakikosa, na wengine walitiwa uzito, na Mungu aliwapa roho ya usingizi. Kumbe inawezekana kabisa ukawa unaonekana upo vizuri kwenye maisha ya kimwili ila ndani yako ukawa una usingizi mzito.

Hakikisha unakuwa kwenye kundi la waliochagulia, na hakikisha unaepuka kundi la wasiochaguliwa, kuepuka au kutoka kundi la wasiochaguliwa ni wewe  kuamua kumpokea Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wako.

Shida nyingine unaweza kumpokea Yesu Kristo, lakini ndani yako ukakosa unyenyekevu, hii itakufanya ukose upekee, hii itakufanya usipate vile vitu vizuri kwa Mungu wako.

Hakikisha unajazwa na Roho Mtakatifu, hakikisha Neno la Mungu linakuwa chakula chako cha kila siku, usikubali siku ikapita bila kusoma Biblia yako, ukizingatia hayo utaanza kujiona unatoka hatua moja kwenda hatua nyingine.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com
+255759808081