
Chanzo cha mtu kuwa na imani ni kusikia, mtu yeyote mwenye msimamo mkali wa imani kuhusu jambo fulani, ujue huyo mtu imani yake haikutoka hewani. Kuna mahali ameichota hiyo imani, na wala haijaingia ghafla, kuna muda alitumia kusikia mafundisho mbalimbali ya kumjengea imani yake.
Tunapaswa kujichunga sana kwa vitu ambavyo tunapenda kusikiliza, maana vitu tunavyoona vidogo vidogo alafu tunatumia muda mwingi kuvisikiliza sana. Vitu hivyo ndivyo vinatujengea imani ndani yetu, imani ambayo muda mwingine huanza kutusumbua baadhi ya maeneo.
Imani moja ikishatangulia kuingia kwa mtu yeyote, kuja kuitoa na kuweka nyingine huwa kuna kazi sana, ugumu unakuja kwa sababu kuna imani nyingine tofauti imejenga mizizi ndani yake.
Na ili mizizi hiyo ya imani ing’olewe mtu huyo anapaswa kuanza kusikiliza mafundisho tofauti na yale aliyokuwa anaamini, kadri anavyosikia ndivyo kuna imani inazidi kujengeka ndani yake.
Hata kama ni kwa kidogo sana, hata kama itachukua sana muda, kadri anavyozidi kusikia kitu kile kile kila siku, ipo siku mtu huyo atabadilika na kugeukia yale ambayo amesikia sana.
Mtu unaweza kuongea naye kuhusu habari fulani, au unaweza kuhubiri sana, au unaweza kufundisha sana kuhusu habari za Yesu Kristo, mtu asikuelewe kabisa ila mtu huyo kadri atakavyozidi kusikia habari za Yesu Kristo ipo siku ataokoka. Anaweza asiokoke kwenye mikono yako akaja kuokoka kwenye mikono ya mtumishi mwingine kabisa tofauti.
Naomba unielewe hapa, tumeona imani ya mtu inakuja kwa kusikia neno au imani ya mtu inajengeka ndani yake kwa kusikia neno au mafundisho. Sasa inategemeana mtu huyu alikuwa anasikiliza neno la namna gani, maana kuna neno la Kristo, na kuna neno la shetani pia.
Sasa hapa lazima uwe makini, unaweza ukawa msikilizaji mzuri sana wa vipindi fulani kwenye redio au kwenye kifaa chochote kile au ikawa kwa marafiki zako. Kama hayo unayosikiliza hayana utukufu kwa Mungu, uwe na uhakika baada ya muda fulani utayaamini hayo na kuanza kuishi kama ulivyopata maelekezo.
Imani ni kitu kingine kabisa, imani ina uwezo wa kufanya mambo makubwa na ya ajabu, sasa inategemeana na huyo mtu ana imani gani. Ana imani sahihi au ana imani potovu, kama ni imani potovu ni hatari sana maana tayari huyo mtu anaamini yupo sahihi.
Linda sana mambo unayosikia, maana yale mambo unayosikia kwa muda mwingi yana mchango mkubwa wa kuondosha imani yako ya awali na kuingiza imani nyingine mpya. Hiyo imani mpya inaweza ikawa sahihi au ikawa sio sahihi.
Ukimwona mtu ana imani ya Kristo sawasawa uwe na uhakika imani yake ilianza kujengwa polepole na msingi wa Neno la Kristo, haijotekea kama muujiza huyo mtu akawa na imani thabiti hivyo bila Neno la Kristo.
Rejea: Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo. RUM. 10:17 SUV.
Angalia imani yako ni ipi, una imani ya mashaka mashaka mbele za Mungu, uwe na uhakika hayo mashaka hayajatokea ghafla yapo mafundisho yanakufanya uwe na mashaka. Na kama huna mafundisho ya kukupotosha, utakuwa una ukosefu wa Neno la Kristo au mafundisho sahihi ya Neno la Mungu.
Una imani ya uhakika mbele za Mungu, uwe na uhakika imani hiyo ya uhakika haijaota tu kama uyoga, hiyo imani imejengeka ndani yako kwa sababu ya kupenda kusikiliza mafundisho ya Neno la Mungu, na kwa sababu unapenda sana kusoma Neno la Mungu.
Kama husikilizi sana mafundisho ya Neno la Mungu, unasikiliza sana mambo mengine ya dunia, ujue imani yako thabiti itajengwa na yale ambayo hayaonekani sana machoni kama yanaweza kubadilisha mtu.
Linda sana unayosikia mara kwa mara, ndio unapaswa kujiepusha na mazungumzo mabaya, maana mazungumzo mabaya huharibu tabia njema. Unaweza kuona ulikuwa upo vizuri kitabia ila baada ya kuwa na makundi mabaya, utashangaa ghafla imani yako nzuri inabadilika.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com