Jambo gumu sana mtu aliyekutenda jambo baya, alafu mtu akaja akakuambia mwache huyo usimtende jambo lolote baya, au akaja mtu akakuambia msamehe huyo aliyekukosea. Alafu wewe ndani yako unapanga umlipize kisasi.

Ukiwa kama mtu wa Mungu au ukiwa umeokoka sawasawa hupaswi kulipa baya kwa baya au ovu kwa ovu, mtu aliyekutenda jambo baya na wewe usianze kutafuta kulipa baya. Utakuwa umemkosea sana Mungu wako, haijalishi huyo mtu amekutenda nini, hupaswi kulipa baya.

Unaweza kusema mbona ni kitendo cha kikatili sana kukuambia usilipe baya/ovu, hakuna ukatili hapo, hupaswi kulipa baya kwa aliyekukosea, haijalishi amekutendea jambo gani baya sana. Huna mamlaka ya kuanza kumtafuta na wewe umlipe ubaya wake.

Kutafuta kulipa ovu kwa ovu au baya kwa baya, huko ni kumkosea Mungu wako, hata kama unajisikia kufanya hivyo au hata kama unasikia amani baada ya kurudisha baya kwa baya au ovu kwa ovu. Ujue ulitenda kosa mbele za Mungu na unapaswa kutubu.

Nimewahi kusikia habari moja ya wanandoa fulani, mwanaume baada ya kutoka nje ya ndoa kwa habari ya uzinzi, mke wake naye alivyoona mume wake ametoka nje ya ndoa. Na yeye mwanamke aliamua kutoka nje ya ndoa na mwanaume mwingine, sasa hapa ukiangalia huyu mwanamke alimkomoa mume wake au alijiangamiza mwenyewe nafsi yake.

Utaona kwamba amejiangamiza mwenyewe, maana hapo hajamkomoa mume wake, bali ameharibu uhusiano wake na Mungu wake. Alipaswa kuendelea kutunza uhusiano wake na Mungu, na sio kukimbilia kulipa uovu alilofanya mume wake.

Watu wengi wamekuwa hivyo, hasa walio kwenye mahusiano ya ndoa na wengine ya uchumba, kisa amemwona mwenzake ameshindwa kuwa mwaminifu. Na yeye anageuka na kuwa mtu asiye mwaminifu kwenye ndoa yake.

Hivi kama ni mchumba wako ameshindwa kuwa mwaminifu kwenye uchumba, na wewe baada ya kumwona ameanza tabia mbaya. Na wewe unaanza ile ile tabia mbaya, sasa hapo nani alaumiwe kuwa hajatulia? Kwa sababu wote mmeingia kwenye kundi lile lile la watu wasiotunza ujana wao.

Rejea: Msimlipe mtu ovu kwa ovu. Angalieni yaliyo mema machoni pa watu wote. RUM. 12:17 SUV.

Huenda umekaa na kitu moyoni mwako cha miaka mingi sana iliyopita, huwa unasubiri siku ya kulipiza kisasi kwa huyo mtu aliyewahi kukutenda jambo baya. Kuanzia sasa nakusihi kwa jina la Yesu Kristo uondoe hayo mawazo mabaya.

Hupaswi kulipiza kisasi, kazi ya kulipa kisasi ni ya Bwana, kazi ya kurudisha baya kwa baya sio ya kwako, usianze kujichukulia sheria mkononi. Hilo sio jukumu lako la kulipa kisasi kwa aliyekukosea, haijalishi amekukosea nini, haijalishi kila mtu anashangaa kwanini umemwache.

Pamoja na watu kukuona hupaswi kumwacha hivi hivi, lazima ulipize kisasi, ukiwa kama mkristo hupaswi kuangalia watu wanasema nini, unapaswa kuangalia maandiko matakatifu yanasemaje kuhusu kulipiza kisasi.

Rejea: Wapenzi, msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana imeandikwa, Kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena Bwana. RUM. 12:19 SUV.

Acha kabisa mawazo ya kulipiza kisasi, ukiona moyoni mwako umejaa hasira na umeahidi kabisa lazima umtende jambo baya huyo aliyekukosea. Ujue Neno la Mungu halimo moyoni mwako, ujue Kristo hayumo ndani yako, mtu mwenye Yesu moyoni, aliyejazwa Roho Mtakatifu huwezi kumkuta anawaza kulipiza kisasi.

Anajua kabisa kisasi cha adui yake ni juu ya Bwana mwenyewe, na kweli malipo yake huwa yanaonekana hapa hapa duniani. Hata kabla ya kufika mahali popote, huwa wanaanza kupata malipo yao kwa kile walipanda kwa watu.

Ubaya wao waliotendea wengine huwa unaanza kuonekana kwa uwazi kabisa, kama ni hivyo ya nini kuanza kutafuta kulipiza kisasi wakati dunia yenyewe inaweza kumwadhibu moja kwa moja mtu wa namna hiyo.

Usiruhusu moyo wako ukaweka kinyongo chochote kile cha kulipa ovu kwa aliyekutendea ovu au usipange kulipa baya kwa baya kwa yule aliyekutenda baya.

Kufanya hivyo ni kuingilia kazi ya Mungu, maana amesema kisasi ni juu yake, mtu akikutenda baya lolote usifikiri Mungu hamuoni, Mungu anamwona vizuri sana na atamwadhibu kwa wakati wake mwenyewe. Labda mtu huyo aliamue kutubu mapema kabla hajamfika hayo.

Usiache kusoma Neno la Mungu kila siku, ukiwa na maarifa sahihi ya Neno la Mungu huwezi kuanza kufikiri kulipa baya kwa mwenzako. Utajua ni kweli amekukosea ila sio kazi yako kumrudishia baya alilokutenda.

Kama bado hujajiunga na kundi la wasap la kusoma Neno la Mungu kila siku, nakukaribisha sana uungane na wenzako wanaosoma Neno kila siku. Tuma ujumbe wako kwa wasap namba +255759808081 utapatiwa taratibu za kundi kisha utaunganishwa.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com