
Nimeona watu wakilaumu baadhi ya watumishi wa Mungu kuwa mbona hawafanyi hivi na vile kwenye huduma zao, hadi imefika mahali wanaonekana si watumishi wa Mungu halisi kutokana na kutokutenda yale ambayo watu wamezoea kuona watumishi wengine wakifanya.
Wakati mwingine watumishi wale wanaotupiwa lawama imewabidi wafanye vile vitu ambavyo watu wanawashutumu kuwa hawavifanyi, pamoja na kujiingiza kwenye vitu ambavyo hakuna msukumo ndani yao kuvifanya. Hakuna matokeo mazuri waliyopata kupitia hicho walichoanza kukifanya.
Wale wale waliokuwa wanawashutumu kuwa hawafanyi hicho wanachokifanya sasa, wanabadilisha maneno mengine na kusema hawana nguvu ya Mungu ya kufanya hicho wanachokifanya. Ndio maana hakuna matunda yeyote mazuri.
Kumbe tatizo sio kukosa nguvu ya Mungu ndani ya mtumishi huyu, shida ipo kwake kusikiliza watu na kufanya wanavyotaka wao bila kujalisha Mungu anasema naye nini juu ya hicho alichokianzisha kukifanya.
Vipo vitu mtumishi wa Mungu hupaswi kujihangaisha navyo kabisa, kwa sababu Mungu hakukutuma kwa hicho, kama ni kufanya fanya tu kama mtumishi ikitokea kama dharura. Ipo sehemu yako ambayo unapaswa kukaa pale pale na ukamtumikia Mungu vizuri kabisa.
Kwa sababu ya kukosa maarifa sahihi ya Neno la Mungu, watu wengi tumeingia kufanya mambo ambayo hayakupaswa kufanywa na sisi. Tumeshindwa kutambua kwamba kila mmoja ana kazi ambayo Yesu Kristo amempa aifanye, na akisimama kwenye sehemu yake atafanya vizuri zaidi.
Mtumishi wa Mungu Paulo alilitambua hili kwenye huduma yake, ambapo anatupa ufahamu kwamba sio kila jambo unapaswa kulifanya. Yapo maeneo ni muhimu na ni agizo la Kristo ila hupaswi kujishughulisha nayo maana Kristo hakukutuma uyafanye.
Rejea: Maana Kristo hakunituma ili nibatize, bali niihubiri Habari Njema; wala si kwa hekima ya maneno, msalaba wa Kristo usije ukabatilika. 1 KOR. 1:17 SUV.
Hebu fikiri, mambo mangapi umejilazimisha kuyafanya kama mtumishi wa Mungu huku moyoni mwako hujisikii msukumo wa aina yeyote kufanya, wala hujisikii amani ya Kristo ndani yako kuyafanya ila umejilazimisha kuyafanya kutokana na maneno ya watu.
Sio kana kwamba hayo mambo ni mabaya, unapaswa kuangalia Yesu Kristo alikutuma uyafanye hayo au Yesu Kristo alikuita umtumikie kwenye eneo hilo unalohangaika nalo? Jibu unalo ndani ya moyo wako.
Na wewe unayelaumu mtumishi fulani mbona anahubiri tu watu wakiokoka hawabatizi, nami nakuuliza una uhakika kuwa ametumwa kwa hilo. Huenda hakutumwa kwa hilo, kazi yake ni kuhubiri na watu wakiokoka yupo mtu ambaye kazi yake ni kuwabatiza wale waliokoka.
Tusiwe tunawatupia lawama watumishi wa Mungu pasipo kujua maandiko matakatifu yanasemaje kuhusu hicho tunachowalaumu, tuelewe kwamba tatizo linaweza lisiwe kwao likawa kwetu. Kwa kuwa hatujui maandiko yanavyosema tukawa tunajiona tupo sahihi kumbe hatupo sahihi kabisa.
Nakusihi sana usome Neno la Mungu kila siku, kama hili ni changamoto kwako, nipo tayari kukusimamia kuhakikisha unajenga tabia ya kusoma Biblia yako kila siku. Tuma ujumbe wako kwa wasap namba +255759808081 utapata maelekezo mengine ya kujiunga na darasa hili la kusoma Neno la Mungu.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com