Vile vitu tunavyoviona havina nguvu sana ya kutuzuia tusiuone ufalme wa Mungu, ndivyo vitu ambavyo vitatufanya tusiuone ufalme wa Mungu, ndivyo vitu vitakavyotukosesha mbingu kwa kuendelea kuvifanya katika maisha yetu.

Shida tuliyonayo ni kwamba tunaingiza ushabiki kwenye mambo ya msingi, shinda nyingine tunaingiza udini kwenye mambo ambayo maandiko matakatifu yanatukataza. Na dini zetu zinakuwa zinaturuhusu kufanya, tunaona bora kusikiliza mafundisho ya dini kuliko kulifuata Neno la Mungu.

Wapo watu wasipoachia dini zao mioyoni mwao, wakamruhusu Yesu Kristo aingie mioyoni mwao, na kulifuata Neno la Mungu linavyosema. Hawataurithi ufalme wa Mungu, haijalishi wanaonekana ni watu wazuri, kama matendo yao yanamkataa Kristo, itakuwa ni ngumu kwao.

Wapo watu wanaona uasherati ni kitu cha kawaida kabisa na hakuna shida yeyote ile akifanya huku akiendelea kuitwa mkristo, yupo ndani ya kanisa na anashiriki mambo mbalimbali ya kanisa ila ni mwasherati kupindukia.

Wapo watu wanasema wanamwamini Yesu Kristo ila wanaabudu sanamu, na hawana shaka kabisa na hilo, bila kujua kuabudu kwao sanamu kutawafanya wasiweze kuurithi ufalme wa Mungu.

Wapo watu ni wazinzi, lakini wanasema wameokoka, ukiwatazama matendo yao ni machafu sana kwa uzinzi, wanaona kwa sababu wapo kanisani na wanakiri Yesu ni Bwana. Wataenda mbinguni kwa kigezo hicho, bila kujua kitakachowafanya waurithi ufalme wa Mungu ni maisha ya utakatifu.

Wapo watu ni wafiraji, lakini wanasema wanamwabudu Mungu aliye hai, na wao wana amani kabisa mioyoni mwao kuwa wataingia mbinguni. Hakuna kitu kama hicho, hakuna mfiraji atakayeingia mbinguni.

Rejea: Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa Mungu? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti, wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang’anyi. 1 KOR. 6:9‭-‬10 SUV.

Kama wewe ni mtukanaji, usije ukafikiri ni jambo la kawaida tu, uwe na uhakika kutukana kwako kutakuzuia usiione mbingu. Kutukana kwako hakuna kibali mbele za Mungu, usipoacha hiyo tabia mbaya hutoweza kuiona mbingu, ni kama unaona ni jambo dogo ila amini hivyo.

Usijifariji ulevi hauna shida, wala usijifariji unywaji wa pombe hauna shida kabisa kwa mkristo, ukajaribu kutetea unywaji wa pombe kwa namna yeyote ile. Lakini jua kwamba walevi wote hawataurithi ufalme wa Mungu, haina mjadala mkubwa sana.

Na usifikiri tabia yako ya kunyang’anya watu vitu vyao na kuvifanya vyako, usifikiri hiyo inampendeza Mungu wako, uwe unafahamu tabia yako mbaya itakuzuia kuurithi ufalme wa Mungu. Hata kama unasaidia sana watu, hata kama unatoa misaada sana kwa yatima, kama wewe unawanyang’anya watu mali zao uwe na uhakika itakuwa ngumu kuingia mbinguni.

Vizuri kulifahamu Neno la Mungu na kulipokea ndani ya moyo wako, bila kukubali kulipokea utaishi vizuri hapa duniani, alafu siku ya mwisho unaingia Jehanam milele. Wakati ulikuwa na uwezo wa kurekebisha mapema kabla ungali hai.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com