Upo utumwa wa dhambi, ambapo mtu anakuwa amefungwa kwenye dhambi, wakati mwingine anaweza akawa anatamani kutoka kwenye kifungo hicho cha dhambi anakuwa hajui atatokaje humo.

Shetani anaweza kufunga ufahamu wake asiweze kuona mlango sahihi wa kumtoa kwenye kifungo hicho cha dhambi, anaweza kuendelea kuutumikia utumwa wake kwa nguvu kubwa bila kuwa na namna ya kutoka mahali alipo.

Mtu huyu atakapopata mafundisho sahihi ya Neno la Mungu, mtu huyu ataweza kutoka kwenye utumwa wa dhambi aliokuwa anautumikia. Atakapoamua kweli kumpokea Yesu Kristo kuwa Bwana na mwokozi wake, ataondokana na utumwa wa dhambi na kuwa mtu huru mbele za Mungu.

Upo utumwa mwingine wa wanadamu, sio utumwa wa mwili, bali utumwa wa kiroho, mtu anakuwa amefungwa kwenye mapokeo ya dini yake. Hata kama dini yake ina mambo ambayo hayaendani na maandiko matakatifu, mtu huyo anakuwa anafuata dini yake inavyomtaka aenende.

Yupo mtu mwingine anakuwa anafuata ukoo wake unavyotaka, lazima atii matambiko ya jamii yake, lazima atoe sadaka za mizimu ya mababu. Lakini mtu huyu anajiita mkristo, huyu si mtu aliye huru katika Kristo, bali mtu huyu ni mtumwa wa wanadamu.

Zipo jamii nyingine huwezi kuoa binti yao bila kuwanunulia wazee pombe, ama wazazi hawawezi kutoa binti yao bila wazee kunywa pombe, huu sio ukristo. Kama wazazi hawawezi kumwozesha binti yao bila wazee kunywa pombe, huo ni utumwa wa wanadamu, bado watu hawa hawapo huru katika Kristo.

Watu walio huru hawawezi kuendeshwa na mapokeo mabaya ya kijamii na kidini, haijalishi unawapenda sana wazazi wako, kama wanakulazimisha kufanya mambo yanayomkosea Mungu wako. Hupaswi kufanya, kwa sababu wewe si wa huko tena, bali umekombolewa kwa damu ya thamani kubwa.

Tulinunuliwa kwa gharama/thamani kubwa, ili tusiwe watumwa tena wa wanadamu, kama unasema umeokoka alafu bado unashiriki ibada za kutoa kafara, ibada za kutoa sadaka kwa miungu ya mababu, ibada za sanamu. Wewe bado ni mtumwa wa wanadamu, bado hujawa yule mtu anayeonyesha alinunuliwa kwa thamani kubwa.

Rejea: Mlinunuliwa kwa thamani; msiwe watumwa wa wanadamu. 1 KOR. 7:23 SUV.

Hebu jiulize wewe ni mtumwa wa wanadamu, kama nilivyosema mwanzo utumwa ninaouzungumzia hapa si wa kimwili, bali ni ule utumwa ambao unakuwa upo kidini au kijamii. Utumwa ambao unakuwa unafanya yale mambo ambayo yamekatazwa na Mungu, alafu wewe unakuwa unayafanya kutokana na jamii yako inakutaka uyafanye.

Tumeona andiko linavyosema hapo juu, sisi tumenunuliwa kwa thamani, hatupaswi kuwa watumwa wa wanadamu. Hupaswi kufanya vitu ambavyo Neno la Mungu linakataza, haijalishi jamii yako inakusukuma ufanye, wala haijalishi wazazi wako wanakulazimisha ufanye.

Utapokubaliana na wazazi wako kufanya vitu ambavyo maandiko matakatifu yanazuia/yanakataza kushiriki hayo mambo, alafu wewe ukafanya utakuwa umemtenda Mungu dhambi. Bila kujalisha ni wazazi wako wamekuambia ufanye, maana unaweza kusema tunapaswa kuwatii wazazi kama ilivyoandikwa.

Tumeambiwa tuwatii wazazi wetu katika Bwana na si kwa kila jambo, tukiwatii kwa kila jambo tutamkosea Mungu wetu. Maana yapo mambo mabaya yanayopingana na Neno la Mungu, tukiwatii wazazi tukafanya hayo mabaya kwa kigezo cha kuwa tunapaswa kuwatii, hatutaweza kujitetea siku ya hukumu.

Nakusihi sana usome Neno la Mungu kila siku, na uombe Roho Mtakatifu akusaidie kuelewa yale unayosoma, usije ukawa unafanya mambo ambayo yanapingana na Neno la Mungu. Kama bado hujajiunga na darasa letu la wasap la kusoma Neno la Mungu kila siku, nakusihi ujiunge sasa, tuma ujumbe wako kwa wasap namba +255759808081.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com