Kuwa na maarifa sahihi sio kigezo cha wewe kuwa kero kwa wengine ambao bado wachanga kiroho, kuwa na maarifa sahihi ndani yako kwanza inakufanya uwe mnyenyekevu na mtu anayeweza kuendana na wale wasiokuwa na maarifa sahihi.

Shida inakuja pale mtu anakuwa na maarifa sahihi, alafu kuwa kwake na maarifa sahihi inakuwa kero kwa wengine, badala ya kuwa baraka kwa wengine ambao bado ni wachanga. Anaanza kuwa kikwazo kikubwa sana kwa wengine walioingia kwenye wokovu siku sio nyingi.

Mtu aliyekuwa anajua kula chakula fulani au nyama ya mnyama fulani ni haramu/najisi kabla ya kuokoka, uwe na uhakika mtu huyo atakapopata Neema ya kuokoka. Ataendelea kuona vile vile kuwa chakula au nyama fulani ni haramu kula.

Lakini kadri atakavyozidi kupata mafundisho ya kuukulia wokovu, mtu huyo ataanza kubadilika kwa taratibu sana. Ataanza kuingia mwenyewe kwa moyo wa kupenda na sio wa kulazimishwa, na wengine wanaweza wasile kabisa wakaendelea na misimamo yao ya kutokula chakula fulani au nyama fulani.

Vile vile kwenye mavazi, kama mtu alizoea kujifunika kichwa kabla ya kuokoka, yaani mavazi yake makuu yalikuwa hijabu na alifundishwa kwenye dini yake kuwa anapaswa kuvaa hivyo. Uwe na uhakika hiyo hali inaweza isimtoke haraka, hadi pale atapozidi kupata maarifa sahihi ndio ataanza kubadilika mwenyewe.

Ama kubadilika kwake kukachukua miaka mingi sana, na wengine wanaweza wasiache hayo mavazi yao pamoja na kupata mafundisho mbalimbali ya Neno la Mungu. Na pamoja na kusoma sana Neno la Mungu kila siku, anaweza akawa bado anaendelea kuvaa vile vile.

Vile vile kwa mwanaume aliyekuwa anafuga rasta, alafu ukamhubiria Neno la Mungu akaokoka, usikimbilie kumwambia nyoa nywele zako au nyoa rasta zako. Ukimwambia hivyo uwe na uhakika hamtaelewana haraka, na anaweza akaona kuokoka kwake sio sawa.

Mtu anaweza akawa hapendi chakula fulani ambacho anaona kwake sio sahihi kula, sio kwa sababu kinamletea madhara kwenye mwili wake hapana. Sababu haswa ni mafundisho ya awali aliyokuwa nayo, aliambiwa hupaswi kula nyama au chakula hicho, tangu utoto wake hadi anakuwa mtu mzima.

Alafu aje atokee mtu ghafla akamwambia unapaswa kula hicho chakula, au ukawa kero kwake, anakwambia hali hicho chakula ni najisi kwake. Wewe unaenda kula mbele yake, kwake itakuwa ni maumivu makubwa sana na atajisikia vibaya sana kwa ukatili unaomfanyia.

Rejea: Kwa hiyo, chakula kikimkwaza ndugu yangu, hakika sitakula nyama hata milele, nisije nikamkwaza ndugu yangu. 1 KOR. 8:13 SUV.

Ndugu yangu kama nyama ya nguruwe ni najisi kwa ndugu yako au mpendwa mwenzako, na wewe kwako sio tatizo kutokana na maarifa uliyonayo. Hupaswi kula mbele yake, kula mbele yake ni kumfanyia ukatili ambao ni dhambi mbele za Mungu.

Utasema sasa dhambi inatoka wapi kula nyama ambayo inaonekana ni najisi kwa mpendwa au kwa ndugu au kwa rafiki? Ndio ni dhambi kama unajua kuwa hapendi hiyo nyama. Alafu ukaenda kuitenga mbele yake, hapo utakuwa unamkosea Yesu Kristo.

Rejea: Hivyo, mkiwatenda dhambi ndugu zenu na kuitia jeraha dhamiri iliyo dhaifu, mnamtenda dhambi Kristo. 1 KOR. 8:12 SUV.

Unapaswa kujua namna ya kuenenda na aliye dhaifu wa imani, mtu aliye okoka siku si nyingi na anajua kula chakula fulani au kula nyama fulani ni dhambi mbele za Mungu. Unapaswa kwenda naye taratibu na kuepuka kula mbele yake.

Lazima utumie hekima ya kiMungu iliyotokana na maarifa ya Neno la Mungu, hata kama wewe ni baba/mama wa familia alafu mna mfanyakazi wenu wa ndani ambaye hali chakula fulani au nyama fulani. Hebu kuweni waungwana katika hilo, unajua kabisa huyo mfanyakazi imani yake inamwambia ni dhambi kula nyama ya mnyama fulani, ninyi mnamwambia pika.

Kama sio kupika mnaenda kununua ikiwa imepikwa mnakuja kula naye meza moja, moja kwa moja mtakuwa mnafanya vibaya na kufanya hivyo ni dhambi mbele za Mungu. Kwanini msile huko huko zinapopikwa akiwa yeye hayupo?

Maarifa yako au kuelimika kwako chunga sana isije ikawa kero kwa wengine wasio na maarifa sahihi, vipo vyakula unavyoona wewe havina shida kutokana na maarifa uliyonayo ila mwenzako akaona ni najisi kwake.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com