Mungu anayo njia nyingi za kuwafundisha watu wake, Mungu anazo njia nyingi za kuwaonya watu wake, Mungu anazo njia nyingi za kuwakemea watu wake, njia zote zipo sahihi kutokana na kile ambacho anamtaka mtu wake asimkosee yeye.

Pamoja na njia zote hizo nilizokutajia, ipo njia nyingine ya kuwatadharisha watu au kuwaonya watu, japo njia hii inaweza ikawa ina maumivu au ina hasara kwa wengine ila Mungu huitumia kutuonya.

Yupo mtu alikuwa anatamani kuiba, Mungu anaweza kumwonyesha mfano wa mtu mmoja aliyeiba, mfano huo unaweza ukawa mbaya sana. Yule mtu anayeiba anaweza kuawawa mbele yake, kifo kibaya sana.

Kupitia hicho kifo kibaya cha huyo mtu aliyekuwa anaiba mali za watu, Mungu anamtaka kumfundisha yule ambaye alikuwa anafikiri kuanza kuiba asije akafanya hivyo.

Huo ni mfano wa mtu anayeiba ila ipo mifano mingi sana ambayo Mungu huitumia kutuonya tusifanye mabaya, mtu mmoja anaweza kukutana na pigo kubwa la Mungu. Ili kuwafahamisha wengine wasije wakawa na tabia kama ya huyo mtu aliyekutana na pigo la Mungu.

Ndivyo ilivyo hata makanisani, mtu kutengwa au kupewa adhabu yeyote ile, ni kwa ajili ya kuwaonya na wengine wasije wakafanya hilo jambo. Wakithubutu kufanya mambo yasiyofaa na wao watatengwa na kanisa, hii inawafanya watu wawe na heshima/adabu.

Wanapokuwa na heshima, inakuwa ni usalama wa maisha yao ya wokovu, japo watu huwa wanafikiri kutengwa kwa mshirika. Asiwe anashiriki meza ya Bwana na baadhi ya mambo akayozuiliwa, huwa wanafikiri ni kitendo ambacho hakipaswi kufanywa kwa mshirika, hawajui wanaofanya wapo kimaandiko.

Adhabu nyingi sio tu kumwadhibu mhusika na iwe imeishia hapo, nia yake huwa ni kuwapa salamu wale ambao walikuwa wanapanga kufanya jambo hilo lisilofaa. Wakishaona mwenzao kilichompata hawatakaa wafanye hilo jambo, labda mtu mwenyewe ashupaze shingo yake.

Rejea: Lakini wengi sana katika wao, Mungu hakupendezwa nao; maana waliangamizwa jangwani. Basi mambo hayo yalikuwa mifano kwetu, kusudi sisi tusiwe watu wa kutamani mabaya, kama wale nao walivyotamani. 1 KOR. 10:5‭-‬6 SUV.

Hawa ni wana wa Israel Mungu aliwaangamiza jangwani baadhi yao wale waliomkosea Mungu, ili sisi tusomapo habari zao tusiwe watu wa kutamani mabaya. Tuone tukifanya mabaya yatakayotupata ni mabaya.

Najua umewahi kukutana na mtu aliyeharibu njia zake, vile anakusihi usije ukafanya kosa alilolifanya yeye, watu wale huwa wanaongea kwa uchungu sana. Ambapo ukimwangalia unamwona anajutia kabisa ila anakuwa hana jinsi ya kufanya.

Yapo mambo mabaya hutokaa uyapate kama utajiepusha nayo, na yapo mambo hutokaa uyapate ndipo ujifunze kuwa ni hatari. Mambo mengine utajiepusha nayo kwa kuona madhara yaliyowapata watu wengine, au kwa kusimliwa habari zao, au kwa kusoma kwenye vitabu.

Unaweza kutumika kama mfano wa kuwafundisha wengine wasije wakawa na tabia kama yako, kufanyika mfano wa wengine linaweza lisiwe jambo jema sana ila pale utakapoenda kinyume na Mungu, utakuwa mfano wa wengine.

Ili kuepuka kuwa mfano kwa makosa tunayomkosea Mungu, tusome Neno la Mungu kujua Mungu hapendi nini na anapenda nini, tujue wengine walikosea wapi na sisi hatupaswi kukosea wapi. Hiyo ndio itakuwa salama yetu, maana sio kila baya tunapaswa kulipitia kwenye maisha yetu.

Kama bado hujajiunga na kundi la wasap la kusoma Neno la Mungu kila siku, tuma ujumbe wako kwa wasap namba +255759808081 utaunganishwa kwenye kundi.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com