
Ukisikia neno upendo bila shaka kuna picha inakuja ndani yako, inaweza ikaja picha yenye maumivu makali kwako kutokana na labda ulivyoonyesha upendo wako kwa mtu fulani. Mtu huyo akaja akutenda jambo baya sana, ambapo hakupaswa kufanya hivyo kabisa kutokana na upendo wako uliouonyesha kwake.
Picha ya pili inaweza ikawa nzuri kwako kutokana na matokeo mazuri uliyoyaona kwa watu, baada ya kuwa mtu unayeonyesha upendo kwa wengine waliokosa upendo huo wa kweli.
Upendo linaweza likawa neno rahisi sana kulitamka ila katika utekelezaji wake katika vitendo, likawa ni suala gumu sana, japo mdomoni mwako ukawa unalitamka kwa urahisi kabisa.
Hili linaweza likawa jambo ambalo lina changamoto kwa waamini wengi sana, na unaposikia upendo sio jambo la hewani hewani tu. Ni jambo ambalo linapaswa kuwa ndani ya mtu mmoja mmoja, kwa kifupi ni jambo la ndani ya mtu.
Na ili uwe na pendo la kweli, lazima uwe na Yesu Kristo moyoni mwako, lazima uwe na Roho Mtakatifu ndani yako. Maana Yesu Kristo ndiye Baba wa upendo, huwezi kuwa na upendo wa kweli bila ya kuwa na Yesu Kristo ndani yako, lijue hili.
Upendo wa dunia upo ila sio upendo wa kweli, upendo wa kweli ni wa Yesu Kristo, ukimpokea kama Bwana na mwokozi wa maisha yako. Na ukaamua kutulia kwake na kujifunza Neno lake, upendo wa kweli utakuwa ndani yako.
Sasa mtu mwenye upendo ndani yake, mtu huyo unafiki kwake haupo, mtu huyo hawezi kudanganya, bali atakuwa ni mtu anayesema kweli. Umekosea mahali atakuambia ukweli, hawezi kukunyamazia kimya, wala hawezi kukusifia mahali ambapo sio pakusifiwa.
Mtu aliye na pendo la kweli ndani yake, ukiwa kama ndugu yake kimwili au kiroho, lazima akuonye, lazima akukemee, lazima akusahishe ulipokosea. Nia yake usipoteze uhusiano wako na Mungu, wala usiendelee kumkasirisha Mungu kwa matendo mabaya.
Sifa mojawapo kuu ya upendo ni ukweli, mtu anayekuambia ukweli ni yule mwenye upendo wa Mungu ndani yake, ni yule mtu anayekupenda, hapendi kukuona ukipotelea gizani. Bali hupenda kukuona ukiwa ung’aa nuruni.
Rejea: Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli. 1 KOR. 13:4, 6 SUV.
Huo ndio upendo, upendo haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli, penye udhalimu wowote upendo hauwezi kukaa mahali pale. Na kwa kuwa upendo upo ndani ya mtu, mtu huyo hawezi kuchekelea udhalimu wowote ule.
Upendo wa kweli hauna unafiki, kama ni jambo baya mtu mwenye upendo atasema kwa uwazi hili jambo halifai, tena atasisitiza kufanya lililo jema. Tofauti na mtu mwenye pendo lenye unafiki ndani yake, anaweza kukuambia upo vizuri, kumbe ndani yake anajua kabisa upo vibaya.
Usije ukawa na pendo la unafiki, pendo ambalo linasifia hadi uovu, pendo ambalo linamremba mtu mwovu hadi anaonekana anachokifanya ni kizuri. Wakati hicho anachokifanya kinamuuzi Mungu, na kinazidi kumwangamiza kabisa nafsi yake.
Rejea: Pendo na lisiwe na unafiki lichukieni lililo ovu, mkiambatana na lililo jema. RUM. 12:9 SUV.
Hilo ndilo pendo la kweli, pendo linalochukia ovu, pendo linaloambatana na lililo jema, hilo ndilo pendo la kweli. Ambalo kila amwaminiye Yesu Kristo anapaswa kuwa nalo, na linapaswa kuonekana katika matendo yake.
Mnafiki ni yule anakusifia upuuzi wako unaoufanya, jambo lolote lile linalomchukiza Mungu ni upuuzi ambao hupaswi kukubalika na mtu yeyote mwenye upendo wa kiMungu ndani yake.
Lazima atakuambia ukweli uweze kubadilika, sio ukimwona mtu anakuambia ukweli unamwona kama adui yako, unamwona anafuatilia maisha yako, utakuwa hujajua vizuri kutofautisha wanaofuatilia maisha yako, na wanaokutakia mema katika maisha yako.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com