
Kama kuna kitu adimu siku hizi kwa watu ni uaminifu, uaminifu umekuwa wa kutafuta sana kwa watu, ukikutana na wapendwa kadhaa unaweza kupata wachache waaminifu na wengine wote wakawa sio waaminifu.
Uaminifu wa mtu haupimwi kwa maneno ya mdomoni, uaminifu unapimwa kwa matendo, kwanini matendo, kila mtu ni mwaminifu kwa kuongea ila ukija katika matendo/utekelezaji uaminifu unaukosa kabisa kwa mtu.
Kama kuna watu wanatafutwa dunia ya leo, ni watu waaminifu, uaminifu umekuwa ni mgumu sana kwa watu kuupata, mnaweza kuongea na mtu vizuri. Lakini kwenye utekelezaji wake ikawa ni ngumu sana, tena atatumia na uongo kukudanganya.
Mbaya zaidi huu ugonjwa wa kukosa uaminifu umehamia hadi kwa watu wanaosema wameokoka, utasema kwanini niwatupie mzigo huu waliokoka. Bila shaka umewahi kukutana na hili kwa baadhi ya wapendwa, nazungumza mambo ambayo yapo wazi na kila mmoja anakutana nayo, na kama hukutani nayo basi umewahi kusikia ndugu yako au rafiki yako akiwa mhanga wa hili.
Unaweza ukafika mahali ukaona ni heri kufanya jambo na mtu asiyemjua Mungu kabisa kuliko na ndugu yako wa kiroho, hii inakuja pale ulipoumizwa na mpendwa mwenzako uliyekuwa unamwamini hawezi kukufanyia hivyo alivyokufanyia.
Vinywa vyetu vinapaswa kuwa na uaminifu, kile tunasema tunapaswa kukitoa ndani ya mioyo yetu, hata kama hutofanya kwa asilimia zote itajulikana huyu mtu ni mwaminifu. Na sababu utakayotoa ndiyo itakuwa na maana na utaeleweka pasipo shaka yeyote.
Rejea: Maana vinywani mwao hamna uaminifu; Mtima wao ni shimo tupu, koo lao ni kaburi wazi, Ulimi wao hujipendekeza. Zaburi 5:9.
Umeona hapo, watu wengi vinywani mwao hamna uaminifu, hili ndilo tatizo la wengi wetu, kile tunachosema au kile tunachoahidi ni tofauti kabisa. Nilisema sio kila kitu unachoahidi kinaweza kufanyika vile uliahidi, hilo haliwezi kuwa kigezo cha kukufanya usiwe mwaminifu.
Shida inaanzia pale unaahidi kitu ambacho una uhakika kabisa hutokiweza, sio hilo tu unakuwa unaendelea kudanganya zaidi huku ukijua hutokifanya. Wakati ulikuwa na uwezo wa kusema kweli, ama ukamwambia mtu nimekwama, ama siwezi hili, naweza hili.
Maandiko matakatifu yanasisitiza sana uaminifu, maana yake ni jambo la muhimu sana kwa mwamini, bila uaminifu bado hujawa mtu unayeyashika maandiko ipasavyo.
Rejea: Wasiwe waibaji; bali wauonyeshe uaminifu mwema wote, ili wayapambe mafundisho ya Mwokozi wetu Mungu katika mambo yote. Tito 2:10.
Tuwe waaminifu kwa vitu vya watu, mtu amekupa kitu umtunzie usikile kitunze, wala usikiuze kitu cha mtu, mtu amekukabidhi mtoto wake umelelee uwe mwaminifu katika hilo.
Uaminifu wako mbele za Mungu, utakufanya upendwe na watu ambao waliona dunia haina watu waaminifu, tena utawafanya watu waanze kurejeza imani zao kwa Mungu kwa kuona kuwa bado ana watu wazuri waaminifu.
Uaminifu unalipa sana, usifikiri kuwa mtu mwaminifu ni jambo ambalo halikuletei matunda ya haraka, kweli linaweza lisikuletee matunda ya haraka ila siku ikifika utafurahi. Ni kama haionekani haraka kwa watu ukiwa mwaminifu, ni kama inakufanya upitwe na mambo mengi ambayo yangekupatia fedha haraka.
Ila fahamu kwamba uaminifu unalipa, tena uaminifu unakufanya uaminiwe na watu, unaweza kufanya kosa mahali fulani likafunikwa na sifa ya uaminifu wako. Linaweza lisichukiliwe kwa uzito mkubwa sana, bali ukaonekana ulitereza kidogo ila sio makusudi yako, hii ni kutokana na uaminifu wako.
Rejea: Lakini hawakuulizwa habari za ile fedha waliyokabidhiwa; maana walitenda kazi kwa uaminifu. 2 Wafalme 22:7.
Unaona uaminifu ulivyo, unasahaulisha na mambo mengine kabisa, sikuambii hivi ili uwe unatumia nafasi ya uaminifu wako vibaya. Nakuambia sifa ya uaminifu kupitia maandiko ili uweze kuona uzito wake.
Fanya/tenda kazi yako kwa uaminifu mkubwa, utaona jinsi Mungu atakavyokubariki kupitia uaminifu wako. Haijalishi utachukua muda mrefu ukiwa huoni matunda makubwa kwa kile unafanya, kama unafanya kwa uaminifu, ipo siku utang’aa zaidi ya hapo.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com