Miongoni mwa eneo ambalo watu wengi bado hatujajua madhara yake ni pamoja na eneo la kushiriki meza ya Bwana, yaani ushirika Mtakatifu. Watu wengi huwa tunashiriki tu meza ya Bwana isivyostahili, na mtu anakuwa hana wasiwasi wowote kabisa.

Hii inaweza ikawa ni kukosa maarifa sahihi kuhusu faida ya kushiriki meza ya Bwana, na madhara ya kushiriki meza ya Bwana isivyostahili. Ukilitazama kimwili unaweza kulichukulia ni jambo la kawaida, ila fahamu kuwa sio jambo la kawaida kabisa.

Kabla ya kushiriki meza ya Bwana au ushirika Mtakatifu ni lazima ujihoji mwenyewe kwanza, maisha yako mbele za Mungu yanapaswa yawe safi kabisa. Na kama hayapo safi unapaswa kutengeneza kwanza na Mungu ndipo ushiriki meza ya Bwana.

Tofauti kabisa na wengi wetu huwa tunashiriki tu meza ya Bwana bila kujalisha maisha yetu yapo salama au hayapo salama, hasa yakiwa hayapo salama. Kama hayapo salama mtu huyo anakuwa anajipatia hatia ya mwili na damu ya Bwana.

Maana mtu anapokula mkate na kunywa kile kikombe, hula na kunywa hukumu ya nafsi yake. Maana maisha yake hayapo salama, anapoendelea kufanya hivyo bila kutengeneza na Mungu anakuwa anajiangamiza mwenyewe.

Rejea: Basi kila aulaye mkate huo, au kukinywea kikombe hicho cha Bwana isivyostahili, atakuwa amejipatia hatia ya mwili na damu ya Bwana. Lakini mtu ajihoji mwenyewe, na hivyo aule mkate, na kukinywea kikombe. Maana alaye na kunywa, hula na kunywa hukumu ya nafsi yake, kwa kutokuupambanua ule mwili. 1 KOR. 11:27‭-‬29 SUV.

Sijui kama unanielewa ninachokizungumza hapa, hili ndilo eneo ambalo watu wengi tunamuuzi Mungu wetu pasipo kujua, ama kwa kujua. Nina sema hivi kwa sababu ambazo utakubaliana na mimi hapa kutokana na mifano hii nitakayoenda kukupa hapa.

Mfano, unamkuta dada/kaka wanafanya uasherati kabisa, lakini inapofika saa ya kushiriki meza ya Bwana(ushirika Mtakatifu) utamwona na yeye anashiriki. Watu wanaweza wasijue kuhusu tabia yake mbaya, yeye akawa anajua kile ambacho anakifanya gizani.

Mwanaume/mwanaume anatembea na mke/mume wa mtu, lakini siku ya ushirika Mtakatifu huwezi kumkosa, anaona asije akaulizwa na watu mbona siku hizi hushiriki meza ya Bwana. Anaula mkate na kukinywea kikombe, hajui madhara ya hicho anachofanya.

Mwingine ni mchawi, mwingine ni mlevi, na mwingine ni mwizi, lakini saa ya kushiriki meza ya Bwana huwezi kumkosa, na akitoka kushiriki meza ya Bwana anaenda kuendelea na tabia yake.

Kama ni janga basi hili ni janga la wakristo wengi sana, kitakachotufanya kuhukumiwa siku ya mwisho ni pamoja na hichi. Tunaweza tukachukulia jambo la kawaida, lakini litatuletea madhara makubwa sana kiroho na kimwili.

Unaweza ukawa ulikuwa unafanya hili bila kujua, kuanzia sasa umejua kupitia somo hili, nimekutolea mifano michache ila zipo dhambi nyingi sana ambazo Biblia imezitaja. Unapaswa kutengeneza kwanza kabla ya kwenda kushiriki meza ya Bwana.

Kila watu au kila dhehebu lina utaratibu wake wa kushiriki meza ya Bwana, hilo la utaratibu halina shida kama haliendi kinyume na Neno la Mungu. Shida inakuja pale mtu mwenyewe anaposhiriki isivyostahili, hapa ndipo palipo na shida.

Ninachokushauri ni kwamba usome Biblia yako, unaweza ukatupia lawama mtu mwingine ila huwezi kujiondoa/kujinasua kwenye hili la kusoma Neno la Mungu. Biblia unayo, na kama hunayo unaweza ukainunua, na ukaanza kuisoma.

Unaposoma Biblia yako yapo mambo mengi sana unajifunza mwenyewe, unapojifunza ni rahisi kwako kuchukua hatua kuliko kusubiri uje uhubiriwe au ufundishwe. Na ni rahisi kusema hukufundishwa, kumbe ulishafundishwa mara nyingi sana ila umesahau, labda kutokana na kupuuza kwako.

Muhimu; kama bado hujajiunga na kundi la wasap la kusoma Neno la Mungu kila siku isipokuwa jumapili, chukua hatua sasa kwa kuwasiliana nasi kwa wasap namba +255759808081 utaunganishwa baada ya kupewa kanuni za kundi.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com