Kama kuna jambo la kufurahia katika maisha haya ni kumpokea Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wa maisha yako, kwanini nakuambia hivyo, mateso ya mwenye haki ni tofauti kabisa na mateso ya mtu ambaye hajaokoka.

Utakuwa shahidi wa hili kama umeokoka, unaweza ukawa kwenye mateso makali, mateso ambayo yanasababishwa na majaribu makali, lakini pamoja na hayo yote. Ukikaa ukitulia unaona kuna faraja fulani unaiona ndani yako, au anatokea mtu anaanza kukutia moyo.

Au inatokea unakutana na ujumbe wa mtumishi wa Mungu, ukawa unagusa maisha yako moja kwa moja, ukawa unagusa yale mapito mazito unayopitia kwenye maisha yako. Ujumbe ambao unakupa tumaini la kusonga mbele, ujumbe ambao unakuinua tena pale ulivunjika moyo.

Unaweza kushangaa ndani ya mateso yako, au ndani ya jaribu lako zito, au ndani ya changamoto ngumu unazopitia kwenye maisha yako. Unaweza kujiona nguvu za rohoni zinakuwa kiwango cha juu zaidi, unashangaa kuna faraja ya namna ya pekee inakuwepo ndani yako.

Wale wasiomjua Yesu Kristo, wanaweza wakawa wanakushangaa ukiwa unazidi kusonga mbele pamoja na magumu unayopitia kwenye maisha yako. Yupo mwingine anaweza akawa anasubiri urukwe na akili, lakini badala yake unakuwa mtu unayefarijika ndani ya moyo wako.

Huenda ulikuwa huijui siri hii, huenda ulikuwa hujui maana yake ni nini, leo unaenda kujua ni nini huwa inatokea kwenye maisha yako. Unapokuwa umeokoka alafu ukawa unapitia mateso makali, ndivyo na faraja inavyozidi kuongezeka ndani yako.

Huwezi kulemewa na mateso kiasi kwamba ile furaha ya Bwana kutoweka kabisa ndani yako, ipo faraja inakuwa inazidi kuongezeka ndani yako. Huenda ulikuwa hujui ni kwanini unapita kwenye mateso makali ila unaendelea kuonyesha tumaini.

Hichi kitu cha pekee wanakuwa nayo wale ambao wameokoka, mateso yao hayawezi kuwafanya wakose kabisa ladha ya maisha ya wokovu, maana ndani yao ipo faraja ya Kristo inafanya kazi.

Rejea: Kwa kuwa kama vile mateso ya Kristo yanavyozidi kwetu, vivyo hivyo faraja yetu inazidi kwa njia ya Kristo. 2 KOR. 1:5 SUV.

Unaona hilo andiko linavyosema? Huenda ulikuwa na mashaka kuhusu hichi ninachokuambia hapa ila andiko hilo limetuthitishia hichi ninachokuambia. Mateso yako yanavyozidi kwako, vivyo hivyo na faraja yako inazidi kwako.

Hatuwezi kukwepa mateso katika maisha yetu, lakini kinachofurahisha hapa ni kwamba vile mateso yanazidi kuongezeka kwetu, ndivyo na faraja ya Kristo inazidi kuongezeka kwetu.

Huwezi kuta mateso yamezidi kipimo cha faraja ndani yetu, ni vitu ambavyo vinaenda vikifuatana pamoja, shetani akidhani anaenda kukumaliza, Yesu Kristo anazidi kuongeza faraja yake ndani yako. Mwisho wa siku unaona umevuka kwenye jaribu hilo.

Rejea: Mateso ya mwenye haki ni mengi, Lakini BWANA humponya nayo yote. ZAB. 34:19 SUV.

Sijui sasa unaposoma ujumbe huu upo kwenye mateso gani katika maisha yako, yawe mateso ya afya yako, yawe mateso ya ndoa yako, yawe mateso ya kazi yako, yawe mateso ya huduma na mengine ambayo sijayataja hapa. Fahamu kwamba ipo faraja ndani yako, na tena fahamu kwamba Mungu atakuponya nayo.

Lakini kabla hajafika kukuponya nayo, ipo faraja ndani yako anakuwa anaiachilia kwa nguvu, ukiwa makini utaona unafarijika kwa namna isiyo ya kawaida. Adui yako aliyekuwa anatamani kukuona ukilia kila siku, atashangaa kukuona ukiwa na farajiko ndani ya moyo wako.

Ipo faraja itakayo kwa Mungu, faraja ambayo inakuwa mkombozi wetu wakati wa mateso yetu, wakati wa mawazo mazito, mawazo ambayo hayana majibu ya maswali yetu. Lakini Bwana hutupa faraja zake zenye kufurahisha roho zetu.

Rejea: Katika wingi wa mawazo ya moyoni mwangu, Faraja zako zaifurahisha roho yangu. ZAB. 94:19 SUV.

Haleluya, hii ni neema ya pekee tuliyonayo wakristo, ipo faraja inayotusaidia ndani yetu, fahamu hili ndugu yangu. Inawezekana ulikuwa unaona wewe ni mtu wa kuteseka tu, huna tumaini lolote, pamoja na hayo yote ipo faraja inaambatana na wewe katikati ya mateso yako.

Endelea kulinda uhusiano wako na Mungu, haijalishi mateso yako yanazidi kuongezeka, jua na faraja ya Kristo inazidi kuongezeka ndani yako hadi unatoka kwenye mateso hayo. Usiondolewe kwenye njia sahihi ya Kristo, baki njia sahihi maana ipo faraja ya Kristo katikati ya mateso yako.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
www.chapeotz.com
+255759808081