Mtu aliyepofushwa akili zake asiweze kuelewa jambo fulani kusudiwa, uwe na uhakika huyo mtu hawezi kukuelewa kamwe hata kama utatumia muda mwingi kumwelewesha huyo mtu.

Haijalishi una uwezo mkubwa wa ushawishi, kama mtu huyo akili zake zimetiwa giza, uwe na uhakika mtu huyo hutomuweza kwenye kile unachotaka akuelewe. Zaidi sana mtaishia kubishana, au mtaishia kugombana na kuachana pasipo amani.

Wakati mwingine huenda umefika mahali unaanza kujiuliza labda huna nguvu ya ushawishi, kutokana na vile unatumia muda mwingi kuwaeleza watu habari za kuwasaidia maisha yao. Lakini pamoja na kueleza yale yanayoweza kuwasaidia wao wenyewe, bado hakuelewi na wanakuona unapoteza muda wako.

Upande mwingine unapaswa kujua sio kana kwamba huna uwezo wa kuongea maneno mazuri, unapaswa kujua watu unaoongea nao, au watu unaowapa elimu. Akili zao zimetiwa giza katika hilo, shetani hataki kabisa wapokee kile kina msaada kwao.

Unaweza ukawa unaumiza sana kichwa kuhusu wale wasiomini, labda ukawa unawaza kwanini hawataki kuifuata kweli ya Mungu. Badala yake wameng’ang’ana na upotovu ambao upo wazi kabisa, kwa akili ya kawaida unaweza ukawa unafikiri wanafanya makusudi.

Hawafanyi makusudi bali fikira zao zimetiwa giza, hawana uwezo wa kupokea kweli ya Kristo, zaidi wataona unawapigia kelele, zaidi watakuona wewe mwenyewe unayewahubiria umepotoka.

Rejea: Ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu. 2 KOR. 4:4 SUV.

Shetani akimkamata mtu, ambaye katika andiko hili ametajwa mungu wa dunia hii, mtu huyo anaweza akaendelea kushikilia imani yake potovu siku zote. Bila kujalisha mtu huyo ameelezwa mara ngapi mahali alipo sio sahihi, bila kujalisha wahubiri wangapi wamemwambia kuhusu habari ya kuokoka.

Habari njema ni kwamba, mtu huyo anaweza kufunguliwa fikira zake na Yesu Kristo, na mtu huyo akabadilika kabisa akatoka mahali ambapo alikuwa haamini jina la Yesu Kristo. Akawa mtu ambaye analiamini na kulitangaza kwa watu wengine wasiomini.

Ukiwa kama mtumishi wa Mungu, tusichoke kuwaombea na kuwahubiria wale wasiomini, ili waweze kufunguliwa fikira zao, wakishafunguliwa fikira zao watamgeukia Mungu wa kweli na kuiamini kweli ya Kristo.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com