
Kuna hali bado zinawasumbua sana watu, hasa yule mtu ambaye alikuwa kwenye maisha fulani mbaya yasiyompendeza Mungu wake. Mtu huyo akija kuokoka huwa bado anajiona ana hatia mbele za Mungu, hata anapoenda mbele za Mungu kuomba anaona maombi yake hayawezi kupokelewa/kusikilizwa na Mungu.
Kinachomfanya mtu kufikiri hivyo ni yale maisha yake ya nyuma, yale maisha ya hovyo aliyoishi huko nyuma, anaona Mungu hawezi kumsamehe yale aliyoyatenda katika maisha yake.
Mwingine huenda ameshaambiwa kabisa umesamehewa kabisa na Mungu hazikumbuki tena dhambi zake, lakini pamoja na kuambiwa hivyo bado anajiona sio mtu aliye safi mbele za Mungu.
Mtu anakuwa na hofu nyingi au anakuwa anaona mambo aliyoyafanya anafikiri labda kuna njia nyingine ya kusamehewa, ndio awe na uhakika wa kuwa amesamehewa dhambi zake.
Pamoja na mawazo hayo yote, mtu huyu anakuwa hayupo sahihi kwa mawazo yake hayo, siku anachukua uamzi wa kuokoka, yaani kumpokea Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wa maisha yake. Tangu siku hiyo alisamehewa dhambi zake zote.
Baada ya kumpokea Yesu Kristo, kuanzia siku hiyo amefanyika kiumbe kipya kabisa, yale mambo ya zamani Mungu hayakumbuki tena. Tena sio hilo tu, tena amekuwa kiumbe kipya ndani ya Yesu Kristo.
Rejea: Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya. 2 KOR. 5:17 SUV.
Kama unasoma ujumbe huu na ulikuwa unajisikia vibaya pamoja na kuokoka kwako, ulikuwa unajiona bado ni mkosaji, kuanzia sasa hivi futa kabisa mawazo hayo kichwani.
Acha mawazo potovu, mawazo ambayo yanakufanya ukose ujasiri mbele za Mungu, mawazo ambayo yanakufanya wale ambao bado hawajaokoka watumie nafasi hiyo ya kutojitambua kwako, waendelee kukuumiza kwa maneno ya kukuvunja moyo.
Ukishajua ukimpokea Yesu Kristo au ukawa ndani ya Yesu Kristo, uwe na uhakika kuanzia siku hiyo umeokoka, wewe umehesabika kwenye kundi la walio ndani ya Yesu Kristo.
Huna haja ya kuwa na mashaka kuhusu kuokoka kwako, ukishaokoka huna hatia tena mbele za Mungu, maana umekubali kutoka kwenye maisha mabaya, na kuingia kwenye maisha mazuri ya kumpendeza Mungu.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com