Nimewahi kusikia baadhi ya vijana wakisema haina shida kuolewa/kuoa mwanamke/mwanaume yeyote ukiwa umeokoka, wakiwa na maana kwamba anaweza kuoa/kuolewa hata na yule asiyemwamini Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wake.

Wakifikiri kwamba kupitia kuolewa/kuoa kwake na huyo mwanamke/mwanaume, ataweza kumbadilisha huyo mwanamke/mwanaume akawa mtu mzuri kwa kumpokea Yesu Kristo.

Kijana kama huyu anayewaza haya anakuwa amekutana na mafundisho ambayo yanamfanya aone kila mwanaume/mwanamke anamfaa yeye. Haijalishi ameokoka, ama hajaokoka, kwake ni sawa tu kutokana na mafundisho aliyokutana nayo.

Baadaye akishaingia kwenye ndoa na mtu aliye wa imani tofauti na yake, anakuja kugundua kuwa mawazo aliyokuwa nayo ya kumbadilisha awe mtu wa tofauti. Mawazo hayo yanafeli na kumwona anaendelea na msimamo wake ule ule wa kutotaka kumwamini Yesu Kristo.

Kijana yule asipokuwa makini anaweza kujikuta ameua kabisa uhusiano wake na Mungu, wakati aliingia naye kwenye mahusiano ya ndoa akiwa anajua ataweza kumbadilisha. Badala yake anabadilishwa yeye mwenyewe.

Lazima tuwe makini sana tunapokuwa tumechagua kuishi maisha ya wokovu, hatupaswi kugusa vitu vilivyo vichafu, haijalishi wale ambao wanatutaka tushirikiane nao ni watu wetu wa karibu sana.

Hatupaswi kuchangamana na wasioamini, hasa kwenye maeneo nyeti kama nilianza mfano wa mahusiano ya ndoa. Tena unapaswa kukaa nao mbali sana, wale ambao unajua kuna tabia wanataka kukuambukiza.

Huwezi kujitenga kabisa na watu wasioamini, maana tunafanya nao kazi, tunasoma nao, tunaishi nao, unapaswa kuelewa hapa na si kukariri. Yapo mambo unapaswa kujitenga nao kabisa, wala hupaswi kukaribiana nao kabisa.

Rejea: Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema Bwana, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha. 2 KOR. 6:17 SUV.

Mungu mwenyewe anasema haya kupitia maandiko yake matakatifu, ukiona hili jambo ambalo nakueleza haliwezi kukuathiri chochote. Endelea kushirikiana nao kwa vitu visivyofaa mbele za Mungu, taratibu utaona kiroho chako kinanyonywa chote.

Unaona watu wana mzaha sana, umewaeleza hawataki kukuelewa, toka katikati yao, usiendelee kukaa katikati ya watu wenye mizaha mbele za Mungu. Kuendelea kukaa pale maana yake umekubaliana nao.

Mahali popote na jambo lolote unapoona halifai, hakikisha unajitenga nalo lisije likakuondoa kwenye uwepo wa Mungu, au likavunja uhusiano wako na Mungu.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com