
Watu wengi hufikiri kutoa vizuri ni kutoa kile kilicho nje ya uwezo wake, kufikiri hivyo kumewafanya watu wengi washindwe kutoa kile walichonacho kwa kukiona ni kidogo sana, kwa kukiona hakifai.
Wengi sana tunakuwa na nia ya kutoa kile tulichonacho, lakini kuna sauti inakuwa inapiga kelele ndani yetu kuwa hicho ni kidogo. Labda ungekuwa na zaidi ndio ungetoa, hapo mtu hatoi tena kwa kufikiri akipata kikubwa ndio atatoa.
Utoaji wa mtu haupimwi sana kile ametoa, mtu anaweza kuonekana ametoa sana, kumbe kiwango chake alichonacho hakupaswa kutoa hicho kiasi alichotoa. Kama ni kipimo cha kupima kile alichotoa, hakifiki hata robo ya vile alivyonavyo.
Lakini yupo mwingine anaonekana ametoa kidogo sana, lakini alichotoa amekitoa kwa nia, pia ametoa kile alichokuwa nacho, sio kile ambacho hakuwa nacho. Kwa nje anaonekana ametoa kidogo sana, ila mbele za Mungu anahesabika ametoa kikubwa.
Wengi sana tunahangaika na vile ambavyo hatuna, tukifikiri tukivitoa hivyo ndivyo tutaonekana tumefanya vizuri, bila kujua kutoa kwa mtu kunaanza na nia. Tena kwa kile alichonacho, ndicho anapaswa kukitoa, na sio kile ambacho hana.
Kile ambacho mtu anatoa kwa nia moja, kitolewacho kinakubalika kulingana na alicho nacho mtu, na si kile ambacho hana mtu. Shika hili litakusaidia sana katika maisha yako.
Rejea: Kwa kuwa kama nia ya kutoa ipo, kitolewacho kinakubalika kulingana na kile mtu alicho nacho, wala si kwa kile ambacho hana. 2 Wakorintho 8:12 NEN.
Tuache kuhangaika na vitu ambavyo hatuna, kwenye kutoa kinachoangaliwa ni nia, unaweza ukawa na vingi, lakini kama huna nia ya kutoa hutoweza kutoa. Unaweza ukawa na vichache lakini ukawa na nia ya kutoa, vile vichache utakavyotoa vikawa vinakubalika kabisa mbele za Mungu.
Usisubiri uwe na kikubwa sana ndipo utoe, kile kidogo ulichonacho unaweza kumsaidia mtu, kinachoangaliwa ni nia yako, kwa kile ambacho unacho. Na sio vile ambavyo huna, shika hili sana.
Pia inaweza ikatokea huna kabisa, lakini ukawa na nia yako kutoa, nakuambia utapata cha kutoa tu, hata kama hakihusiani sana na hitaji husika. Unaweza ukatoa kwa nia ya kwenda kubadilishwa kiwe hitaji husika, hicho nacho kinakubalika.
Ikiwa nia ya kutoa ipo, chochote ukitoacho kinakubalika kulingana na kile unacho, na si kile ambacho huna, kwa hiyo usiwe mtu wa kuhukumiwa kwa vile ambavyo huna. Angalia vile ambavyo unavyo, utaona utoaji wako ukiwa unakubalika sana moyoni mwako, bila kuwa na hukumu yeyote.
Kama bado hujajiunga na kundi la wasap la kusoma Neno la Mungu kila siku, tuma ujumbe wako kwa wasap namba 0759808081 utaunganishwa.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com