
Watu wengi hufikiri mtu anapokuwa mtumishi wa Mungu, hapaswi kupatwa na mateso magumu, inapotokea mtumishi wa Mungu anapita kwenye mambo magumu anaonekana ametenda dhambi.
Wengine huwa wanaona mtumishi wa Mungu anapopata ajili mbaya ya gari, huwa wanaona labda atakuwa amemkosea Mungu kwenye huduma yake. Au kuna mahali atakuwa ameenda kinyume na maagizo ya Mungu.
Fikra kama hizi huwa zipo kwa watu wengi sana, hasa mtu anapokuwa anamtumikia Mungu kwenye nafasi aliyoitiwa, siku akipata tatizo ambalo ni gumu sana kwa akili za kibinadamu. Mtu huyo huanza kufikiriwa tofauti kabisa na wale wanaomfahamu.
Hata yeye mhusika anayepitia mambo magumu asipokuwa makini anaweza akaanza na yeye kufikiri labda kuna mahali amemkosea Mungu wake. Kumbe ni mambo anayoweza kukutana mtumishi yeyote wa Mungu, hata akiwa hajamtenda Mungu dhambi.
Mateso yeyote yale kwa mtume, nabii, mchungaji, mwalimu, mwinjilisti, sio kilelezo cha kumkosea Mungu wake, bali ni nyakati tu ambazo anakuwa anapitishwa kama mtumishi wa Mungu.
Sikatai kuwa mambo mengine mabaya kwa watu waliokuwa wameokoka, alafu baadaye wakarudi nyuma, alafu wakakutana na mateso mabaya ya shetani. Hiyo ipo ila ninachotaka utambue hapa, hupaswi kufahamu hivyo kwa upande mmoja, bali unapaswa kufahamu na upande wa pili.
Hili tunajifunza kwa mtume Paulo, anaeleza hatari/mateso aliyopitia katika maisha yake, kupitia mtume Paulo tunapata kujua kuwa mtumishi wa Mungu au mtu aliyeokoka sawasawa. Anaweza kupita katika mateso magumu pamoja na kuwa na uhusiano mzuri na Mungu.
Rejea: Katika kusafiri mara nyingi; hatari za mito; hatari za wanyang’anyi; hatari kwa taifa langu; hatari kwa mataifa mengine; hatari za mjini; hatari za jangwani; hatari za baharini; hatari kwa ndugu za uongo; katika taabu na masumbufu; katika kukesha mara nyingi; katika njaa na kiu; katika kufunga mara nyingi; katika baridi na kuwa uchi. 2 KOR. 11:26-27 SUV.
Unaona masumbufu aliyokutana nayo mtumishi wa Mungu Paulo, unaweza kurudia tena kusoma hilo andiko nililokupa hapo juu. Mambo ambayo tunaona wana wa Mungu tukikutana nayo kila wakati katika maisha yetu ya wokovu.
Huenda hapo ulipo sasa unapitia katika mateso magumu, dhamiri yako inakushuhudia nini, kama hakuna usichokosa mbele za Mungu. Fahamu hizo nyakati ambazo unapitia katika maisha yako, anaweza kupitia mtu aliyeokoka sawasawa.
Usianze kujiona una laana, au usianze kujiona una mikosi, au usianze kujiona umemkosea Mungu, ona ni kipindi tu unapitia. Upo wakati utaondoka katika hali hiyo, na utatoka ukiwa imara zaidi.
Na usiogope, ama ukaanza kukata tamaa ya kufunga kutokana na kuona maombi yako hayajibiwi, unaweza ukafunga na kuendelea kumtafuta Mungu kwa bidii katikati ya mateso yako.
Hii ndio faida ya kusoma Neno la Mungu, yapo mambo mengi ulikuwa hujui ila unaposoma neno la Mungu unakuwa unajua. Unapojua inakuwa rahisi kwako kutosumbuliwa/kutokuwa na maswali mengi, pale mambo magumu yanapojitokeza kwako.
Nakusihi sana utenge muda wa kusoma Neno la Mungu kila siku, usikubali siku ipite bila kusoma Biblia yako. Utavuna maarifa mengi sana ya kukusaidia katika maisha yako ya wokovu.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com