Kwa siku za leo inaweza ikawa tofauti kabisa kutokana na mambo yalivyo, lakini kwa kawaida mtoto anapaswa kukuta amewekewa akiba ya kutosha na mzazi wake, na si mtoto aje aanze kuhangaika kuwawekea wazazi wake akiba.

Hii inatusukuma tukiwa wazazi alafu bado vijana, tunapaswa kutafuta mali kwa bidii sana, tunapaswa kufanya kazi kwa bidii, ili tuwawekee watoto wetu akiba. Na sio kusubiri tuje tuwekewe na watoto wetu.

Mtoto wako ni haki yake ya asili kupata urithi kutoka kwa wazazi wake, usione sio haki yake kumpa vile ulivyotafuta kwa jasho lako. Ukiwa unatafuta unapaswa kujua na akiba ya mtoto/watoto wako inapaswa kuwepo kwa vile unavyotafuta.

Je, hili unalifahamu ukiwa kama mzazi mwenye watoto/mtoto? Au ukiwa kama mzazi mtarajiwa? Kama hukuwa unafahamu unapaswa kufahamu leo. Mtoto anapaswa kuwekewa akiba na wewe, na sio mtoto wako aje akuwekee akiba wewe.

Hili tunajifunza kupitia maandiko matakatifu, sio maneno ya hewani, maana unaweza kufikiri ni maneno ya kuokota tu, hapana, haya sio maneno ya kuokota. Bali ni maneno yanayotokana na maandiko;

Rejea: Tazama, hii ni mara ya tatu ya mimi kuwa tayari kuja kwenu, wala sitawalemea. Maana sivitafuti vitu vyenu, bali nawatafuta ninyi; maana haiwapasi watoto kuweka akiba kwa wazazi, bali wazazi kwa watoto. 2 KOR. 12:14 SUV.

Hebu tuondoe dhana potovu, tunapaswa kuwawekea watoto wetu akiba ya kutosha, viwepo vitu vya kuwagawia watoto wako, tena kwa utaratibu mzuri. Maana ni vitu vyao ulivyokuwa umewawekea akiba, akiba ambayo uliitafuta kwa jasho lako halali.

Andiko hili tunatufumbua macho tuweze kuona kuwa, kuwawekea watoto wetu akiba ni jambo ambalo linapaswa kuwepo kwa mzazi. Kama bado una nguvu na unasoma ujumbe huu, unapaswa kupambana haswa kuhakikisha unawawekea watoto wako akiba.

Inaweza ikawa akiba ya ardhi, akiba ya fedha taslimu, akiba ya nyumba, au chochote kile ambacho kitakuwa ni kitu chema kwako. Hiyo ndio kazi ya mzazi kwa watoto wake, akiba ni muhimu sana uwawekee watoto wako.

Unatafuta mwenyewe kwa jasho lako kwa kusudi la kuwawekea akiba wanao, unajinyima baadhi ya vitu ili wanao wawe na akiba yao ya kutosha, kufanya hivyo utakuwa umetimiza maandiko matakatifu.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com