Siku ulipoamua kumpokea Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wa maisha yako, wewe umebarikiwa kwa baraka zote za rohoni. Hata kama ulikuwa huelewi hili, kuanzia sasa fahamu kwamba umebarikiwa kwa baraka zote za rohoni.

Tumeshaona kuwa tumebarikiwa, swali la kujiuliza, tunaziona hizo baraka kwenye maisha yetu ya kiroho? Huenda tunaona bado hatujabarikiwa ila Neno lake linatuthibitishia kuwa tumeshabarikiwa kwa baraka zote za rohoni.

Kisheria unayo haki kuzivuta baraka zako kwa imani, huenda shetani amekuvuruga na unaishi kama mtu ambaye bado ana laana, unajiona hujabarikiwa kwa chochote. Unapaswa kufahamu umeshabarikiwa tangu siku ile unaokoka.

Sawa na mtu ambaye hajui kama ana haki kwenye jambo ambalo amezulumiwa na watu wengine, akipata mtu wa kumwambia kuwa ana haki kwenye lile alilonyang’anywa, mtu huyo atakuwa na ujasiri wa kwenda kudai jambo lake au kitu chake.

Lakini asipoambiwa kuwa ana haki kwa lile alilonyang’anywa, ataishia hivyo bila kujua na kile alichonyang’anywa atabaki kuamini hakikuwa haki yake. Kumbe kwa mjibu wa  kanuni kile alichonyang’anywa kilikuwa haki yake, na sheria zinatambua yeye ndio anapaswa kuwa mmiliki halali hicho kitu.

Sasa wengi wetu hatujui kuwa tumebarikiwa na Mungu kwa baraka zote za rohoni, haijalishi unapitia hali fulani ngumu sana katika ndoa yako, katika biashara yako, katika mahusiano yako ya uchumba, katika kazi yako, katika masomo yako.

Unapaswa kufahamu kuwa wewe ni mbarikiwa, na asije mtu akakuambia kuwa umelaniwa, asije mtu akakuambia huna uhalali wa baraka za Mungu. Uhalali wako upo kabisa kama utakuwa umempokea Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wako.

Na usipompokea Yesu Kristo, baraka zako zinakuwa zipo ila zinakuwa zinakusubiri utimize vigezo vinavyotakiwa, na vigezo hivyo ni kukubali kumkiri kwa kinywa chako, kuwa ni Bwana na mwokozi wa maisha yako.

Kama umeshaokoka tayari baraka zako zipo, usipojua hili unaweza kuishi maisha ya wokovu yasiyo na kiwango kinachotakiwa kama mkristo. Fahamu kuwa wewe ni mbarikiwa, umebarikiwa kwa baraka zote za rohoni.

Rejea: Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo. EFE. 1:3 SUV.

Shetani asije akakuzubaisha na mafundisho yake potovu, wewe ni mbarikiwa, kisheria unayo mamlaka ya kumnyang’anya adui aliyezichukua/aliyeziteka baraka zako.

Imani yako imara ndani ya Kristo, ndio itakayo kufanya uweze hayo yote, pasipo imani hutaweza, imani yako inapaswa kuwa imara na isiyoyumbishwa na makelele ya kukukatishwa tamaa.

Jua/fahamu ahadi zako alizokuahidia Mungu, au alizokupa Mungu, kwa kusoma Neno lake, unapojua kuwa wewe tayari umebarikiwa kwa baraka zote za rohoni. Unapata ujasiri mkubwa sana, na unajiona kwa namna isiyo ya mazoea/kawaida.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com