Wizi umekuwa sehemu ya maisha ya wengine, wapo watu wameruhusu watoto wao, na wengine wamewafundisha watoto wao na kuwapandia tabia ya wizi ndani yao. Kwa kuwatuma wakaibe vitu vya watu, na watoto wao wamefanikiwa mara nyingi kuiba vitu vya watu.

Huenda wazazi hao walifanya hivyo wakiwa na shida kweli, wakawatumia watoto wao kufanya mambo yasiyofaa, ambapo baadaye hiyo tabia inakomaa kwa mtoto na kuja kuwa vile ambavyo alifundishwa na mzazi wake.

Mwanzoni huenda mzazi asione madhara yake ila baadaye anakuja kuwa jambazi sugu au kibaka sugu anayesumbua sana jamii. Lakini chanzo cha hayo yote ni mzazi wake, mzazi ana mchango mkubwa kwa mtoto wake kuharibika kitabia.

Hii huenda mbali zaidi, wazazi wanajua kabisa mtoto wao ni mwizi, mali anazopata zinatokana na kuiba vitu vya watu. Lakini unakuta mzazi anavitumia kana kwamba ni jambo la kawaida kabisa, na mzazi mwingine humtakia mafanikio mema katika shughuli hiyo.

Pia wapo wanawake wanajua kabisa waume zao hawana kazi nyingine zaidi ya kuiba/wizi, wanakuwa wanaishi kwa hali hiyo. Na maisha yao huenda yakawa vizuri zaidi kiuchumi, na mwanamke huyu akawa anafurahia bila kutazama madhara yake.

Wizi upo hata kwa watu ambao wanasema wameokoka, sisemi hivi kwa sababu nasema ni mambo ambayo yapo wazi katika jamii zetu. Wengine ni watoto wetu, wengine ni wadogo zetu, wengine ni dada/kaka zetu, wengine ni wazazi wetu, na wengine ni marafiki zetu au majirani zetu.

Kama ni ndugu zetu, kwa jinsi ambayo tumeona mwanzo wa somo hili, tulikuwa na uwezo wa kuwasihi kabisa, nguvu na akili zile zile ambazo wanazitumia kuiba. Wangezitumia kufanya kazi halali za mikono yao wangefanikiwa sana.

Watoto ambao tunawafundisha kwenda kuiba vitu vya watu, tungeweza kuwatumia watoto wale wale kwenda kufanya vibarua ambavyo vinaendana na umri wao. Wakaingiza fedha ambayo ingesaidia familia nzima, badala ya kumfundisha mtoto tabia ya wizi, unakuwa unamjengea tabia ya kufanya kwa bidii.

Rejea: Yeye ambaye amekuwa akiiba, asiibe tena, lakini lazima ajishughulishe, afanye kitu kifaacho kwa mikono yake mwenyewe, ili awe na kitu cha kuwagawia wahitaji. Waefeso 4:28 NEN.

Maandiko yanatoa suluhisho kwa hili kama tunavyosoma hapo, huyu mtu aliyekuwa anaiba mali za watu, aache kuiba na afanye kazi halali itakayomwingizia kipato.

Nguvu na akili zile zile alizokuwa anazitumia kinyume, azitumie sasa kwa njia sahihi ya kumletea Mungu sifa na utukufu. Kama alikuwa anafanya hivyo ili awasaidie watoto wake, wazazi wake, ndugu zake, afanye kilicho halali ili awagawie na wahitaji.

Asiwape wahitaji kitu alichokiiba, awape kile ambacho amekipata kwa jasho lake, kile ambacho ni matunda ya kazi ya mikono yake. Kitakuwa baraka kwa Mungu na kwake pia.

Faida ya kusoma Neno la Mungu ndio hii, unaweza kupata Neno la maarifa la kumsaidia mtu mwingine aliyekwama kifikra na kuona anachofanya ni sahihi kabisa kutokana na kukosa kingine cha kufanya. Kupitia ufahamu wa maandiko unaweza kumfungua ufahamu wake na akapona kabisa.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com