Wapo watu wanakuwa ndani ya moyo wa mtumishi wa Mungu, kwa sababu ya mambo mabaya wanayomfanyia mtumishi, ndani ya moyo wake anakuwa anafikiri anafanya nini ili watu wale waache kumsumbua.

Kwahiyo mtumishi huyu anapoenda mbele za Mungu, maombi yake yanakuwa ya namna ya tofauti kidogo. Maombi ambayo yanahitaji msaada wa Mungu au Mungu aingilie kati juu ya hao watu wanaosumbua.

Sawasawa na mzazi ambaye ana mtoto ambaye tabia yake sio nzuri, mtoto huyu atakuwa mwiba kwa wazazi wake. Atakuwa anawaumiza mioyo yao kutokana na matendo yake mabaya, wazazi hawa hata namna ya uombaji wao unakuwa tofauti kabisa na watoto wengine waliotulia.

Hiyo ni kwa sifa mbaya mtu anakuwa ndani ya moyo wa mtu, sasa ipo sifa njema kabisa mtu anaweza kuwa ndani ya moyo wa mtu mwingine. Mtoto anaweza akawa moyoni mwa mzazi wake kwa sifa njema, mshirika anaweza akawa moyoni mwa mchungaji wake kwa sifa njema.

Hadi uwe moyoni mwa mtu au watu kwa sifa njema, sio jambo rahisi kabisa, lazima uwe kuna kitu umekifanya kwenye maisha ya watu. Hilo jambo jema ulilowafanyia wengine ndio linakufanya uwe mioyoni mwao.

Mtumishi wa Mungu ili awe mioyoni mwa washirika wake au wale watu watakaobahatika kuhudumiwa naye, lazima awe anatumia vizuri huduma aliyopewa na Mungu.

Na ili mshirika aweze kuwa ndani ya moyo wa mchungaji wake kwa sifa njema, lazima huyo mshirika atakuwa amefanya jambo ambalo limeweka kumbukumbu njema kwake.

Mchungaji, mwalimu, nabii, mtume, mwinjilisti, kuwa na kumbukumbu, au kuwa na picha ya mshirika wake kwenye maombi, wakati mwingine sio kana kwamba mshirika huyo ametoa hitaji la kuombewa.

Wakati mwingine ni ule moyo wa kujitoa kwa mshirika kwa kazi ya Bwana, na huenda huyo mshirika amekuwa sehemu ya kusapoti huduma yake ya injili., au kanisani kwake amekuwa akijitoa sana kwa mambo mbalimbali.

Sasa mshirika huyo hawezi kufutika kwenye moyo wa mchungaji wake, lazima atakuwa ndani ya moyo wake, sio kana kwamba hili jambo halipo kibiblia. Hili jambo lipo kibiblia kabisa, maana huenda ulikuwa unafikiri mchungaji anapendelea baadhi ya watu.

Rejea: Vile vile kama ilivyo wajibu wangu kufikiri haya juu yenu nyote; kwa sababu ninyi mmo moyoni mwangu; kwa kuwa katika kufungwa kwangu na katika kazi ya kutetea Injili na kuithibitisha, ninyi nyote mmeshirikiana nami neema hii. FLP. 1:7 SUV.

Unaona hilo andiko linavyosema, mtume Paulo anatuthibitishia hili kuwa wafilipi walikuwa moyoni mwake kutokana na vile wameshirikiana naye katika huduma ya injili. Wapo walitoa mali zao kuhakikisha mtumishi wa Mungu Paulo anaitenda kazi ya Mungu vizuri.

Ukisoma sura yote hiyo ya kwanza, utaona mtume Paulo akiwaombea Mungu, maana alikuwa anawakumbuka sana. Tunaona kumbe kukaa moyoni mwa mtu au watu, unapaswa kuwatendea jambo zuri, au unaweza kuwa moyoni mwa mtu kwa jambo baya ulilomtendea.

Wewe kama mtu uliyeokoka sawasawa, hupaswi kuwa kwenye mioyo ya watu kwa sifa mbaya, bali unapaswa kuwa ndani ya mioyo ya watu kwa sifa njema. Japo huwezi kumpendeza kila mtu ila ukiwa unatenda kwa nia njema, Mungu atakubariki kupitia hilo.

Je, unapenda kukaa ndani ya moyo wa mtumishi wa Mungu, fanya jambo jema kwake, hata ile kusapoti huduma yake kwa kumtia moyo au kwa kumpa sehemu ya kulala kwenye nyumba yako. Hutasahaulika kwenye moyo wake, na kila anapoingia kwenye maombi lazima picha yako ije kichwani mwake.

Hii ndio faida ya kusoma Neno la Mungu, unakuwa unajua mambo mengi ya kukusaidia kwenye maisha yako. Yale maswali au yale mawazo potovu yanakuwa mbali nawe, maana unapoona jambo kama hili linatendeka unakuwa unajua nini kimefanyika.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com