Kitu ambacho wengi sana tumekosea, hasa viongozi au watumishi wa Mungu, ni kule kuchagua ilimradi watu wa kutusaidia katika utumishi au katika uongozi wetu. Kuchagua wale watu ambao wapo kinyume na sisi, wale watu ambao hawana nia moja na sisi.

Unachagua kiongozi awe chini yako kwa ajili ya kukusaidia kwenye majukumu, ili uweze kutimiza maono yako katika huduma uliyopewa na Mungu. Unayemchagua mwenyewe yupo kinyume na wewe, kwa sababu unamwona ana vitu fulani.

Ukishamchagua huyo mtu akusaidie majukumu, huyo huyo ndio atakuwa mtu wa kwanza kuanza kukusumbua, au atakuwa mtu ambaye atashirikiana na maadui zako kutaka kukuharibia baadhi ya mipango uliyonayo.

Unaweza usiwe kiongozi wa ngazi fulani katika jamii au taifa ila ukawa kiongozi kwenye biashara zako, sasa ukichagua kiongozi ambaye yupo kinyume na wewe. Uwe na uhakika mafanikio ya biashara yako yatakuwa chini zaidi, na utashuka zaidi, au unaweza ukaingia kwenye shida kubwa.

Sasa tukirudi katika utumishi wa Mungu, ukichagua au ukiwa na msaidizi wako aliye kinyume na wewe, au aliye na nia tofauti kabisa na maono yako. Itakuwa ngumu sana kufikia maono yako, hadi pale utakapojua wale wanaokuvuta nyuma.

Hili tunajifunza kupitia maandiko matakatifu, mtume Paulo katika huduma yake ya kuhubiri injili, alifika mahali ambapo alitakiwa kuwa na mtu wa kumtuma kwa kazi ya Bwana.

Alichofanya mtume Paulo ni kuangalia ni nani aliye nia moja na yeye, wale ambao hawakuwa nia moja na yeye hawakuwataka kabisa kuwapa majukumu aliyokuwa nayo.

Rejea: Maana sina mtu mwingine mwenye nia moja nami, atakayeiangalia hali yenu kweli kweli. Maana wote wanatafuta vyao wenyewe, sivyo vya Kristo Yesu. FLP. 2:20‭-‬21 SUV.

Kama mtumishi wa Mungu Paulo alilijua hili maana ni jambo ambalo Mungu anatufundisha jambo la msingi sana, jambo ambalo tunapaswa kulizingatia sana katika utumishi wetu.

Tukiendelea kusoma mistari inayoendelea chini tunaona mojawapo alipata mtu wa kumtuma, mtu ambaye alikuwa nia moja naye, mtu aliyemwamini anaweza kufanya kila kilichokusudiwa kufanyika.

Rejea: Lakini naliona imenilazimu kumtuma kwenu Epafrodito, ndugu yangu, mtenda kazi pamoja nami, askari pamoja nami; tena ni mtume wenu na mhudumu wa mahitaji yangu. FLP. 2:25 SUV.

Haleluya, hapa tunaona sifa anazomwagiwa huyu Epafrodito ni sifa zinazoonyesha ni jinsi gani Paulo alimfahamu vizuri ni mtu wa namna gani. Na wengine aliowaacha aliwajua vizuri ni watu ambao hawana nia njema kabisa, hata kama wangeonyesha wanamtumikia Mungu.

Mwisho, nikukumbushe kuwa maarifa kama haya yanapatikana ndani ya Biblia yako unayoibeba kila wakati kwenda nayo kanisani, au huenda hujaibeba siku nyingi ila ipo ndani ya nyumba yako.

Nikusihi usiwe na Biblia bila kuisoma, soma Biblia yako kila siku, tengeneza mpango au utaratibu ambao utaufuata kila siku bila kuuvunja. Kama unapenda kujiunga na kundi letu la wasap la kusoma Neno la Mungu kila siku, tuma ujumbe wako wasap kwa namba +255759808081.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com