Yapo maisha ambayo mtu anakuwa amefikia kiwango cha juu, kiwango ambacho anakuwa labda na kazi nzuri yenye mshahara mzuri, labda anakuwa na biashara zake zinaenda vizuri.

Mwingine anakuwa yupo kwenye familia yenye uwezo mkubwa, kila hitaji la fedha analohitaji kwa wazazi wake analipata kwa wakati unaotakiwa. Hana mawazo kwamba itakuwaje, pale anapoomba kitu fulani kwa baba/mama yake anapewa kwa wakati.

Tofauti kabisa na yule mtoto ambaye wazazi wake hawana uwezo huo wa kumsaidia haraka kile anakihitaji, hata pesa yenyewe ya matumizi ya kawaida kabisa inaweza ikawa ngumu kuipewa. Na wakati mwingine hitaji lake linaweza kuishia hewani bila kupata kiasi cha fedha alichokihitaji.

Yule ambaye alizoea mzazi wake ana pesa za kutosha, alikuwa anasoma shule ya gharama kubwa, ikatokea mzazi wake akawa hana hizo pesa tena. Mtoto huyo anaweza kupata shida kubwa sana, kama hakujua kuna upande wa pili wa kukosa kabisa.

Vile vile yule ambaye hajawahi kujua upande wa pili wa kukosa kabisa au akawa hajui kuwa ipo ya kupoteza kabisa kila kitu ulichokuwa nacho. Mtu yule siku akipoteza kile alichokuwa nacho, anaweza akapata matatizo makubwa sana kwa kupoteza kazi yake au biashara yake.

Wapo watu wengine hawajui kuwa kuna kufiwa, wanaweza wakawa wanahudhuria misiba ya wengine ila hawajawahi kukaa chini wakafikiri na wao wanaweza kupoteza watu wao wa Karibu sana na wa muhimu sana.

Kwa kuwa hawakuwahi kufikiri hilo, siku ikitokea wakaondokewa na mpendwa wao, watu hawa huwa wanapata shida kubwa sana. Wengine hufika wakati huanza kutamani na wao wafe, kitu ambacho hakipaswi kufikiriwa na mtu aliyekomaa sawasawa.

Sasa mtume Paulo anatufundisha jambo la msingi sana, ambalo tunapaswa kulizingatia sana na kuliweka katika mioyo yetu, anatuonyesha ni jinsi gani alijua kuishi katika hali zote.

Rejea: Si kwamba nasema haya kwa kuwa nina mahitaji; maana nimejifunza kuwa radhi na hali yo yote niliyo nayo. Najua kudhiliwa, tena najua kufanikiwa; katika hali yo yote, na katika mambo yo yote, nimefundishwa kushiba na kuona njaa, kuwa na vingi na kupungukiwa. FLP. 4:11‭-‬12 SUV.

Hebu jiulize, ukijipima unajua kuishi katika hali zote? Au umejifunza kuishi katika hali zote? Yaani ukiwa huna na ukiwa nacho? Kama umezoea kuishi katika hali ya kuwa nacho tu. Siku ikitokea ukakosa kabisa, unaweza kupoteza uhai wako au unaweza kupata matatizo mengine ya kiafya kutokana na mshtuko au msongo wa mawazo.

Habari njema ni kwamba tunajifunza hili katika somo hili, unaweza kubadili mtazamo wako, na uanze kujifunza au kufikiri kuna upande wa pili, kama leo huna unapaswa kujua kesho utakuwa nacho. Kama unacho leo, kesho unaweza usiwe nacho, yote ni maisha.

Usiwe mtu aliyefundishwa kushiba tu, unapaswa kuwa mtu anayejua kuna njaa pia, unajua vile njaa inauma. Unajua upo wakati wa kulala njaa, na upo wakati wa kushiba kabisa, haya yote mtu unajifunza mwenyewe.

Usikae kwenye upande mmoja wa kujua mazuri tu au kwa kujua mabaya tu, njaa ikikuuma ujue nao ni wakati, na ukiwa umekula umeshiba napo unapaswa kujua ni wakati wake. Fahamu hali zote, fahamu nyakati zote.

Tena ikiwezekana zifahamu kwa vitendo, ili siku ukiamka huna kazi yako nzuri, tusije tukakukuta umelazwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi au tusije tukasikia umepata presha ya ghafla baada ya kuachishwa kazi.

Ndio maana kufahamu maandiko matakatifu ni muhimu sana, Neno la Mungu linakuimarisha kiasi kwamba ukipatwa na hali ngumu hutomwacha Yesu Kristo. Wala hutopata mishtuko ya kukusababishia shida kwenye mwili wako, kama ni maumivu utapata kama binadamu ila hayatachukua nafasi ya kupoteza uhai wako.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com