Tabia zetu au mienendo yetu ndio inatufanya tutambuliwe na watu wengine tukoje, wale tunaoishi nao kila siku wanaweza wakatusemea vizuri kwa wale ambao tupo nao mbali, au kwa wale ambao hatupo nao mbali sana ila hawatufahamu vizuri.

Mtu akishaokoka, anatarajiwa awe na sifa njema, je kweli sifa yako ni njema kwa watu wengine? Watu wasiomjua Yesu au wasiomkiri Yesu Kristo wanakusemaje? Jibu unaweza ukawa nalo au usiwe nalo ila ukweli unaweza ukaujua kutokana na vile unavyojijua.

Wapo watu wanajulikana kwa uongo, utasikia yule kaka muongo, au yule dada muongo muongo, au yule baba tapeli, au yule mama anayegombanishaga watu kwa maneno ya kutengeneza.

Utasikia yule fundi asiyemwaminifu akipewa kazi za watu hazifanyi kwa wakati, utasikia yule daktari asiye na kauli nzuri kwa wagonjwa, utasikia yule mwalimu anajua kupiga tu watoto wa watu ila kufundisha vizuri hafundishi.

Sifa yako ni ipi kwa watu, watu wanakujua/wanakufahamu kwa tabia ipi, wanakufahamu kwa mazuri, au wanakufahamu kwa mabaya. Kama unajulikana/unafahamika kwa mabaya, ni yapi hayo? Ukishayajua ni vizuri ukajirekebisha.

Pamoja na wapo watu wanajulikana kwa mambo mabaya, wapo watu wanaofahamika kwa sifa njema kabisa, utasikia yule kaka ni mwaminifu sana, yule dada mwaminifu sana, yule mama mwaminifu sana, yule baba ni mwaminifu sana.

Uaminifu wake unaosemwa sio wa kutengenezwa, ni mwaminifu kweli kweli, ukimpa kitu chako akupelekee mahali uwe na uhakika atakifikisha mahali husika. Bila usumbufu wa aina yeyote mzigo uliompa ataupeleka au ataufikisha.

Haya tunajifunza kwa mtu mmoja kwenye Biblia anatajwa na mtume Paulo alikuwa mtu mwaminifu, mtu huyo alikuwa ni Onesimo. Sifa ambayo kila mmoja anapaswa kuwa nayo kama mtu atakuwa hana, na kama atakuwa nayo, basi aendelee kuwa nayo.

Rejea: Pamoja na Onesimo, ndugu mwaminifu, mpendwa, aliye mtu wa kwenu. Hao watawaarifu mambo yote ya hapa petu. KOL. 4:9 SUV.

Badili sifa yako mbaya kuwa sifa njema, kama watu walikufahamu kwa kukosa uaminifu kwa mambo ya watu, imefika mahali hadi wanakuogopa kukupa vitu vyao. Unaweza ukageuza hilo na kuwa mtu unayeaminika na watu.

Wazazi wako walikuwa hawakuamini, marafiki zako walikuwa hawana imani na wewe kabisa, wafanyakazi wenzako walikuwa hawakuamini kwa chochote. Inawezekana kabisa wakaanza kukuamini kama utaamua mwenyewe kubadilika.

Badiliko hilo litakuja kwako kama utaamua kuishi maisha yanayompendeza Mungu wako, hofu ya kiMungu ikiwa ndani yako, uaminifu ndani yako utakuwepo. Huwezi kuiba kitu cha mtu kama ndani yako unaye Yesu sawasawa.

Hii ndio faida ya kusoma Neno la Mungu, kupitia kusoma kwako Biblia unaweza kujitathimini kupitia maandiko matakatifu ukajiona upo kundi gani. Hakikisha unasoma Biblia yako kila siku, kama unapenda tuwe pamoja katika hili tuwasiliane kwa wasap namba +255759808081.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com