Watu wanapopakutazama wewe kama baba au kama mama au kama kaka au kama dada, ni kilelezo kipi wanakipata kwako ambao wanakutazama kama mtu uliyeokoka?

Tunapaswa kujiuliza hili na kujipa majibu sahihi pasipo kujipendelea au pasipo kujionea haya, ili uweze kujua ni mahali gani pa kurekebisha au mahali gani hapahitaji maboresho yeyote.

Sisi kama watu waliomjua Yesu Kristo au waliompokea Kristo, tunapaswa kuwa Kielelezo kizuri, kielelezo ambacho kinaleta sifa njema kwa jamii na waamini wenzako.

Kuokoka kwako kunapaswa kuonekana vizuri kwa kanisa na jamii kwa ujumla, ili watu wanapokutazama wawe na hamu ya kumjua Yesu wako. Maana sifa zako ni njema kwa kanisa na jamii kwa ujumla.

Tukisoma maandiko tunakutana na andiko linaloonyesha kuna watu ambao walikuwa kielelezo, hii inaonyesha kwamba sio jambo ambalo utaanza wewe kwa mara ya kwanza. Tayari ni kitu ambacho kipo, kama kipo maana yake kinawezekana kufanyika kwako au kuwepo kwako.

Rejea: Hata mkawa kielelezo kwa watu wote waaminio katika Makedonia, na katika Akaya. 1 THE. 1:7 SUV.

Kielelezo chako kikoje kwa watu, unajulikana au unasifika kwa mazuri au kwa mabaya? Ukiwa kama mkristo unapaswa kusifika kwa mema, hata wale walio nje wamtamani huyo Yesu uliyenaye.

Sio jambo linaloshindikana kwako, ni jambo ambalo linapaswa kuwepo kwa kila mwamini wa Kristo, kama huna kielelezo kizuri. Maana yake kuna mahali unapungua, unapaswa kuparekebisha hapo penye shida.

Unaposoma Neno la Mungu kila siku ni njia moja wapo ya kujipima upo sawasawa na Neno linavyosema? Hii inakusaidia sana kujiona upo kundi gani. Ndio maana nakusisitiza uwe msomaji wa Neno la Mungu, na kama hujajiunga na kundi la wasap la kusoma Biblia kila siku, tuwasiliane kwa wasap +255759808081.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
www.chapeotz.com