Kama umekuwa makini na umekuwa ukijifuatilia kwenye mambo yako mengi, utakuwa umeona mwili ulivyo kinyume na vile unataka kufanya mambo mazuri. Mara nyingi usipojisukuma kwa nguvu, utajikuta hujafanya jambo ulilopanga kufanya.

Hata kwenye usomaji wa Neno la Mungu, wengi wanashindwa kusoma kwa kusema hawana muda wa kutosha ila ukweli sio kwamba hawana muda wa kusoma Biblia zao. Isipokuwa mwili unawashinda mbinu, muda wa kusoma Biblia wao ndio wanakuwa wanazurura kwenye mitandao ya kijamii, au wanakuwa wamekaa tu bila kazi ya msingi sana.

Mwili siku zote upo kinyume na roho zetu, hata kama roho yako inakuwa radhi kufanya jambo fulani la kumtukuza Mungu wako, mwili wako unaweza kukukatalia kabisa. Usipojisukuma kwa nguvu unaweza kuishia kusema tu.

Na ili tuweze kuishinda miili yetu ni lazima roho zetu ziwe zimeshiba Neno la Mungu kila wakati, maana adui yetu mkubwa ni mwili. Japo wengine tunaweza kufikiri adui yetu mkubwa ni shetani ila ukweli adui namba moja ni kitu ambacho tunacho tayari.

Kama tutausikiliza sana mwili, kumtenda Mungu dhambi itakuwa sehemu ya maisha yetu kila siku, tena tutafanya dhambi hadi kufikia hatua tukawa tunafikiri tupo sahihi. Ama tukawa tunafikiri hatuwezi kuishi maisha yanayompendeza Mungu kwa kujihalalishia mambo mabaya.

Ukiwa kama mtu uliyeokoka au uliyempokea Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wa maisha yako, yaani umefanyika mwana wa Mungu. Unapaswa kujitawala mwenyewe, mwili wako unapaswa kuutawala na sio wewe utawaliwa na mwili wako.

Rejea: Kila mmoja wenu ajue kuuweza mwili wake katika utakatifu na heshima; si katika hali ya tamaa mbaya, kama Mataifa wasiomjua Mungu. 1 THE. 4:4‭-‬5 SUV.

Unaona hilo andiko linavyosema, bila kujua kuutawala mwili wako katika utakatifu na heshima, utaishia kumtenda Mungu dhambi siku zote na huku unajiita mkristo.

Maisha yetu ya wokovu yatakuwa safi kama tutajua kuutawala mwili au tutakataa mwili ututawale, ili tuweze kuenenda katika utakatifu na heshima. Lazima tujue kuutawala mwili, bila kuutawala mwili, hatutaweza kufikia hata yale maono yetu.

Lazima tujue kuutawala mwili, tujue kujiwekea mipaka kwenye maeneo ambayo tunaona yatatuingiza kwenye dhambi, umakini wetu ni muhimu sana. Hapa hupaswi kuleta mazoea kabisa, utawale mwili wako, na ujiangalie usije ukajisahau.

Na ili usiupe nafasi mwili wako, hakikisha roho yako imeshiba kila wakati, upo kwenye gari sikiliza mahubiri kwa njia ya audio, sikiliza Biblia ya audio, sikiliza nyimbo za watumishi wa Mungu, soma kitabu cha kukujenga kiroho.

Ukifanya hivyo utaona unakuwa na nguvu za ndani zaidi, na ukiwa na nguvu za ndani zaidi inakuwa rahisi kwako kuulazimisha mwili kile unataka wewe na sio wenyewe unavyotaka ufanye.

Utafika wakati umechoka, hata ile kushika Biblia yako usome utaona ni ngumu ila kama una nguvu za ndani, yaani kama yule mtu wa ndani atakuwa na nguvu zaidi. Utashinda hiyo hali ya uchovu, hapa utakuwa umefaulu kuuamrisha mwili wako kwa kile unataka ufanye.

Kama bado hujajiunga na kundi la wasap la kusoma Neno la Mungu kila siku, nikualike kwenye hili kundi kwa kuwasiliana nasi kwa wasap namba +255759808081.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com