Sio wakati wote mtu atakuwa kwenye hali ya maumivu makali au atakuwa kwenye kipindi cha majaribu mazito au sio wakati wote mtu atakuwa kwenye kipindi cha kulia tu.

Kipo kipindi mtu anakuwa kwenye hali nzuri, kama ndoa yake inakuwa na amani ya kutosha, kama ni kazi anayo na analipwa vizuri, kama afya njema inakuwepo ya kutosha. Na ni kipindi ambacho hata magonjwa hayapo kabisa, anakuwa anabaki anasikia kwa wengine wanaumwa.

Kama ni watoto anakuwa nao, ile changamoto ya kukosa mtoto kwake anakuwa hana kabisa, wakati huo anakuwa na watoto wazuri wenye afya njema kabisa. Na wanaishi kwenye nyumba nzuri ya kifahari.

Kama ni shule, watoto wanakuwa wapo shule nzuri sana tena za gharama kubwa tu, hata watoto wenyewe wanakuwa wanajisikia fahari kubwa kusoma shule kama hizo. Shule ambazo mtoto wa mkulima wa kawaida hawezi kumpeleka mwanaye.

Kipindi ambacho mtu anakuwa amelima shamba lake la eka 10, 20, 30… alafu mvua ikawa haijakatika njiani, mimea yake ikawa imezaa vizuri kabisa. Akafika kipindi cha mavuno napo akawa amevuna vizuri kabisa na kupata mazao ya kutosha haswa.

Kipindi ambacho mtu anakuwa anafanya vizuri katika biashara zake, kila anachogusa mambo yake yanaenda vizuri kabisa. Hata kama kunakuwepo changamoto, zinakuwepo changamoto ndogo ndogo sana ambazo hata hazimuuzi kichwa chake sana.

Kipindi ambacho mtu alisota miaka mingi sana kwa jambo fulani bila mafanikio, alafu akafikia hatua sasa akawa amefikia kwenye kipindi cha mafanikio. Baada ya kupita kwenye mabonde na milima mingi sana mbele yake huko nyuma.

Vipindi kama hivi shwari na salama anapokuwa navyo mtu, wengi sana huwa wanajisahau kabisa, hata mahali ambapo mtu alitoka huwa wengi wanasahau kabisa na kuona kila kitu kipo sawa. Wanaona haina haja ya kuwaza vitu vingine zaidi, tena wengine hata ule utu wao huwa unapotea kabisa.

Sasa madhara ya kujisahau na kujiona huna haja sana ya kuzingatia baadhi ya maeneo, wengi sana wameanguka na kurudi chini kabisa, na wengine kupoteza uhai wao, na wengine kubaki hawaelewi kabisa wafanye nini.

Rejea: Wakati wasemapo, Kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa. 1 THE. 5:3 SUV.

Ndugu wakati unaona kila kitu kipo sawa, ndipo uharibifu unapoingia, kama vile mwanamke mjamzito. Anaweza akawa vizuri kabisa lakini hali yake inaweza ikabadilika ghafla kwa kushikwa na uchungu wa kuzaa.

Hivi ndivyo itakavyokuwa siku ya mwisho wa dunia, wakati watu wamejisahau na kufikiri hakuna siku ya mwisho, wakati ambao wanaendelea kujenga majumba ya kifahari, wakati ambao tecknolojia itakuwa juu sana, wakati ambao watu watakuwa wanafurahia starehe za dunia hii.

Ndio wakati ambao mwana wa Adamu atakaposhuka kulichukua kanisa lake, wale ambao watakuwa tayari watanyakuliwa hiyo siku, na wale ambao walimwacha Mungu na kuendelea na uchafu wa dunia hii wataachwa.

Ni kama jambo lisiloweza kutokea ila yaja saa usiyoidhania kabisa, utashangaa parapanda inalia, wale waliotunza maisha yao katika hali ya utakatifu ndio watakaoenda mbinguni.

Mteule uwe macho, usije ukajisahau wakati unakula vizuri, wakati una mali za kutosha, wakati mambo yako yanaenda vizuri, fahamu kwamba duniani tunapita. Ile saa usiyoidhania ndiyo itakuwa yenyewe, unaweza kusema una muda wa kutosha wa kuishi ila ghafla ukakatishwa uhai wako na jambo ambalo hukulitarajia.

Uwe macho, usilale usingizi wa kiroho, usijione umefika, dunia hii tunapita rafiki, jambo lolote unalolifanya, mafanikio yeyote uliyonayo, usije ukajisahau, wakati wowote mambo yanaweza kubadilika.

Nakusihi sana kama unasoma ujumbe huu na bado hujamwamini Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wa maisha yako, chukua hatua sasa ya kuokoka, njoo kwa Yesu, na kama ulirudi nyuma hakikisha unamrudia Yesu haraka.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
Cell: +255759808081