Baada ya kuokoka kwako ulifanya bidii ya kuijua kweli ya Mungu? Maana unaweza ukawa umeokoka kweli ila ukawa una mashaka na wokovu wako. Kinachokufanya uwe na mashaka ni kwa sababu hujui ukweli wa Neno la Mungu japo unajiita mkristo.

Kusudi la Mungu wetu ni tuokolewe kutoka kwenye vifungo vya dhambi na tuwe huru katika Kristo, baada ya kuwekwa huru tunapaswa kuukulia wokovu kwa kujifunza kweli ya Mungu kupitia Neno lake.

Hatupaswi kuishia tu kumwamini Yesu Kristo, tunapaswa kupata mafundisho sahihi ya Neno la Mungu, unapaswa kuwa na muda wa kusoma biblia yako ya Neno la Mungu. Hiyo yote inakufanya umjue zaidi uliyemwamini, ukishamjua unakuwa na uhakika wa maisha yako ya wokovu.

Tunapoacha kujibidiisha kujifunza kweli ya Mungu kupitia maandiko matakatifu au kupitia watumishi wake, tunakuwa na upungufu mkubwa ndani yetu. Yapo maeneo tutakuwa tunakwama kwa sababu ya kukosa maarifa sahihi ya Neno la Mungu.

Mungu kumtoa mwanaye wa pekee, ilikuwa ni upendo wake kwetu sisi wanadamu, kazi iliyobaki kwa kila mtu ni kumpokea/kumkiri kwa kinywa chake Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wa maisha yake. Hiyo ndio inatamfanya kuitwa mwana wa Mungu, hiyo ndio hatua mojawapo ya kuingia mbinguni.

Hebu tuone maandiko matakatifu yanasemaje kuhusu hili la kuolewa na kuijua kweli ya Mungu, huenda ukawa unaona kuokoka inatosha, huenda ukawa unaona kujua maandiko mengi inatosha bila kumwamini Yesu.

Rejea: Ambaye hutaka watu wote waokolewe, na kupata kujua yaliyo kweli. 1 TIM. 2:4 SUV.

Mungu wetu ni mzuri sana, atutaka tuokolewe kutoka kwenye dhambi kisha tuijue kweli yake, si unajua huwezi kujua mengi siku moja. Utapaswa kwenda hatua kwa hatua katika kuukulia wokovu wako, bila kujifunza huwezi kutoka kwenye uchanga wa kiroho.

Nimeona baadhi ya madhehebu wanakuwa na madarasa ya mafundisho ya wanafunzi wa ubatizo, kabla hawajaenda kubatizwa wanakuwa wamewekewa msingi wa kuwasaidia kusimama na Yesu Kristo.

Tena yapo madhehebu yana shule ya jumapili, kabla ya lile Neno la jumla kunakuwepo na mafundisho sahihi yanayomfanya mtu aendelee kufahamu mambo mbalimbali kuhusu Mungu.

Makanisa/madhehebu wanaofanya hivyo wapo sahihi kabisa, maana kama mtu ameshatimiza hatua ya kwanza ya kumpokea/kumkiri Yesu, anapaswa kupiga hatua ya pili ya kuujua ukweli kupitia Neno la Mungu.

Hili tunapaswa kulizingatia sana kama watu wenye safari ya kwenda mbinguni, tunapaswa kuendelea kujifunza zaidi Neno la Mungu. Tutaujua ukweli mwingi sana kupitia Neno la Mungu, hata ule uwezekano wa kudanganywa na adui unakuwa haupo.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com