Bila shaka utakuwa sio mgeni wa hadithi mbalimbali za wazee, kwa namna moja ama nyingine utakuwa umewahi kusimliwa hadithi au wewe mwenyewe utakuwa umewahi kuwasilimlia watoto wako au wadogo zako hadithi fulani.

Ukifuatilia hadithi nyingi hazijengi kitu cha maana ndani ya mtu, zaidi zinakuwa zinaweka msingi mbovu ndani ya mtu, na zinaweza kumharibu kabisa mtu na akawa na imani mbovu ndani yake.

Japo hadithi nyingi zimekuwa zikiteka fahamu za watoto, utakuwa shahidi wa hili, babu/bibi zetu walikuwa wanatuhadithia hadithi ndipo tulale. Wakati mwingine bila kuhadithiwa hadithi fulani tulikuwa tunaona siku haijaisha vizuri kabisa.

Hadithi hizi huwa zinaendelea kuwepo hadi utu uzima, zinaweza zikawa tofauti kidogo na za watoto ila zikawa zinawateka watu wazima fahamu zao. Hadithi hizo zinakuwa zinawaingia mioyoni mwao na kuanza kutengeneza kitu ambacho hakimpendezi Mungu.

Madhara ya kusikiliza hadithi za kizee zilionekana tangu zamani, ndio maana ukisoma maandiko matakatifu unaweza kuona tumepewa tahadhari juu ya hili. Inaonekana ni jambo linapaswa kutiliwa mkazo na kuzingatiwa sana katika maisha yetu.

Rejea: Bali hadithi za kizee, zisizokuwa za dini, uzikatae; nawe ujizoeze kupata utauwa. 1 TIM. 4:7 SUV.

Kataa kabisa hadithi zisizokuwa za dini, wala usiseme hazina shida, kuziona hazina shida mwisho wake utaona kuna kitu zimekujengea ndani yako. Ndio maana hapa tunaona mtume Paulo anampa agizo Timotheo azikatae hadithi za kizee.

Kupitia andiko hili, nami nakusihi ujiweke mbali na hadithi za kizee, hadithi ambazo unaona hazina maana yeyote zaidi ya kukuharibia uhusiano wako na Mungu.

Hadithi ambazo hazina maadili ya kikristo, hadithi ambazo ukisubiri au ukiziacha ziendelee kusikika kwenye masikio yako, mwisho wake utaona uharibifu umeingia ndani yako.

Usikubali kurudishwa nyuma na hadithi za kizee, bali zikatae kabisa kwenye maisha yako ya wokovu, mtu anakuletea hadithi za kipuuzi mkatae kabisa au mweleze ukweli hupendi au hubarikiwi na mazungumzo yake.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com