Vizuri kukumbushana hili, wengi wetu huwa tuna tabia ya kujisahau na kuona vitu tulivyonavyo tunadumu navyo au wengine huona wale kwanza raha za dunia hii. Wanasahau yale maisha baada ya kifo, ambapo ni maisha ya umilele.

Hapa duniani ni wapitaji, uwe unapenda au uwe hupendi, fahamu kwamba hapa duniani tunapita, yote unayofanya kumbuka kujiwekea vizuri makao yako ya milele.

Tunaona waajiriwa wengi kabla ya kustafu huwa wanahakikisha wanajitengenezea mazingira mazuri ya kustafu, kama mtu hakuwa na nyumba utamwona anajenga, na mengine mengi.

Mwingine anapoingia tu kazini huanza kutengeneza mazingira mazuri ya kuwekeza sehemu na sehemu, ili siku hana kazi awe ana kitu cha kumfanya aendelee kupata chakula na mahitaji yake ya muhimu.

Japo sio kila mipango hufanikiwa asilimia zote, ipo mipango itaharibika, lakini tunaona kuwa mtu anakuwa na nia gani katika kujiandaa kwa wakati ujao. Hata kama wakati huo ana maisha mazuri, anatafuta njia nzuri ya kumsaidia kuingiza kipato wakati hana kazi hiyo.

Nasi tukiwa kama watu waliokoka, tunapaswa kufahamu maisha mazuri tuliyonayo, utajiri tulionao, watoto wazuri tulionao, wazazi wazuri tulionao, elimu kubwa tuliyonayo, chochote kile kizuri tulichonacho.

Tujue kuwa tutaviacha siku moja, hakuna mtu atakayeondoka na utajiri wake, hakuna mtu atakayeondoka na watoto wake wazuri, hakuna mtu atakayeondoka na wazazi wake wazuri, hakuna mtu atakayeondoka na elimu yake ya darasani ya kiwango cha juu.

Kila kitu tutakiacha hapa duniani, miongoni mwa suti zako nyingi sana au magauni yako mazuri, watachagua suti yako moja tu au gauni lako moja la kuzikwa nalo, miongoni mwa viatu vyako vingi, watachagua pea moja tu ya viatu.

Nyumba zako nzuri utaziacha, magari yako mazuri utayaacha, simu yako nzuri ya gharama kubwa utaiacha, ulikuja huna kitu utaondoka huna kitu. Kama moyo wako uliuweka kwenye vitu vyako, ukasahau kumpa Yesu maisha yako, utakuwa umeingia hasara.

Sikuambii hivi ili uache kufanya kazi kwa bidii, ili uache kufanya biashara, ili uache kusoma kwa bidii, ili uache kujenga nyumba nzuri, ili uache kujijali wewe kama wewe, kwa sababu unajua utaondoka bila kitu chochote. Hiyo sio akili, ujumbe huu unatukumbusha kujiandaa kwa maisha ya umilele.

Rejea: Kwa maana hatukuja na kitu duniani, tena hatuwezi kutoka na kitu. 1 TIM. 6:7 SUV.

Umeona hilo andiko linavyosema hapo? Unaweza ukawa unafikiri labda ni maneno tu, sio maneno tu, ni andiko kabisa linatukumbusha kuwa hatukuja na kitu duniani, tutaondoka bila kitu.

Fanya kila jambo kwa bidii ila kumbuka hukuja na kitu duniani na utaondoka bila kitu, sasa kama hutojiwekea hazina mbinguni, ukaendelea kuhangaika na vitu ambavyo hukuja navyo na kumsahau Mungu kabisa. Ujue jehanamu itakuhusu.

Rejea: Alivyotoka tumboni mwa mamaye, atakwenda tena tupu-tupu kama alivyokuja; asichume kitu cho chote kwa ajili ya kazi yake, hata akichukue mkononi mwake. MHU. 5:15 SUV.

Moyo wako usitekwe na vitu ambavyo hukuja navyo ukaikosa mbingu, hakikisha uhusiano wako na Mungu unaenda pamoja na utajiri wako, unaenda pamoja na elimu yako, na unaenda pamoja na cheo chako kikubwa.

Hukuja na cheo hicho, utaondoka bila cheo hicho, vizuri sana kuwa makini kwa hili na kujiandaa vizuri ukiwa bado upo hai, maana hujui saa wala dakika ya kufa kwako.

Rejea: Akasema, Mimi nilitoka tumboni mwa mama yangu nili uchi, nami nitarudi tena huko uchi vilevile; Bwana alitoa, na Bwana ametwaa; jina la Bwana na libarikiwe. AYU. 1:21 SUV.

Ndugu yangu kuondoka utaondoka duniani, huwezi kuishi milele, “ULIKUJA HUNA KITU UTAONDOKA BILA KITU” kumbuka hili siku zote. Jambo la kujivuna sana kuwa na Yesu moyoni mwako, na maisha yako kuwa safi mbele za Mungu.

Ulichonacho umekitafuta kwa jasho lako halali kabisa, wala hujamwibia mtu yeyote, wala hujamdhulumu mtu kitu chake, pamoja na hayo yote hakuna utakachoondoka nacho. Muhimu ni uhusiano wako na Mungu ulikuwaje ukiwa duniani, hii dunia tu wapitaji ndugu usije ukasahau hili.

Mungu akusaidie uweze kuelewa vizuri huu ujumbe, utakusaidia sana katika safari ya maisha yako ya wokovu, na kama hujaokoka unakukumbusha kumpokea Yesu awe Bwana na mwokozi wa maisha yako.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com