Kuna maswali yanaweza kuulizwa siyo kwa nia ya kupata majibu sahihi, bali ni kuibua hisia za watu ili wagombane au wafarakane tu wenyewe kwa wenyewe. Wengi wameshindwa kugundua hili mapema na badala yake wamejikuta wameingia kwenye ugomvi mkubwa.

Kama umekuwa ukiona, mijadala mingi imezuia ugomvi na mafarakano makubwa baina ya mtu na mtu, hii ni kutokana na kutojua yule aliyeulizwa swali au aliyeingia kwenye mjadala asioujua nia yake.

Unapaswa kuwa makini sana, yapo maswali huwa yanawataka watu waingie kwenye mabishano yasiyo na mwisho mwema, na muulizaji anakuwa anajua analenga nini.

Binafsi mijadala mingi ya Facebook au wasap huwa sishiriki sana siku hizi, hii ni kutokana na mingi haina kutaka kujifunza bali kutifuana na kuibua hasira za watu. Hadi inafika wakati watu wanaanza kutupiana maneno yasiyompendeza Kristo.

Mtu anaweza kukujia na kukuuliza swali la mtego, kabla hujalijibu angalia kwanza, maana wapo wanauliza maswali ya kukufanya ukose amani pale atakapoanza mabishano baada ya kumpa majibu ya kwanza.

Viongozi wengi wa magroup ya wasap hawakulijua hili na mwisho wake wamesababisha magroup hayo kusambaratika, sababu mojawapo ni hii ya kuruhusu mabishano yasiyo na maana.

Kuwa makini sana na maswali yanayoibua mabishano ya kipumbavu, maana mwisho wake huzaa magomvi. Magomvi ambayo yatawatawanya kama kikundi, au yatawafanya mgawanyike makundi makundi na kuondoa umoja wenu.

Rejea: Jiepushe na mabishano ya kipumbavu na yasiyo na maana, kwa kuwa wajua ya kwamba hayo huzaa magomvi. 2 Timotheo 2:23 NEN.

Unaona hilo andiko linavyosema? Sio tu maneno ya watu, bali ni maandiko matakatifu yanatupa angalizo juu ya hili jambo la mabishano yasiyo na maana. Ambayo mwisho wake huzaa magomvi au mafarakano makubwa.

Popote pale utakapokutana na swali lisilo na maana, wala usijimbue kulijibu, na kama utakutana na mjadala usio na maana usikubali kushiriki huo mjadala.

Acha watu wakuone huna ushirikiano, acha watu wakuone vyovyote vile wanavyoweza kukuona kutokana na kukataa maswali yasiyo na maana, ama mabishano yasiyo na maana. Wewe utakuwa unajua kwanini hupaswi kushiriki hayo.

Hii ndio faida ya kusoma Neno la Mungu kila siku, maarifa kama haya unaweza usiyapate mahali popote ila ukayapata ndani ya biblia yako. Unakuwa na hekima ambayo watu wanakuwa wanashindwa kuelewa umeipata wapi.

Hakikisha unaweka ratiba ya kusoma Neno la Mungu kila siku bila kukoma/kuacha, hakuna ugumu wowote ni wewe kuamua kujitoa kwa moyo wako wote, na nguvu zako zote. Utaona ukisoma Biblia yako bila kukatisha njiani kama inavyowasumbua wengi.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com