Miongoni mwa watu ambao wapo kwenye kundi la makwazo, la kudharauliwa, la kuhatarisha uhai wao ni wale walioamua kuokoka. Kundi hili limekuwa likikutana na misukosuko mingi sana kiasi kwamba wengine huona kama kero na kuamua kurudi maisha yao ya awali.

Kwanini sasa wanakuwa wanakutana na mambo kama haya, shetani huwa anajua mahali walipopachagua ni mahali sahihi kabisa. Mahali ambapo panamfanya yeye akose watu, anachokifanya ni kuinua watu wake wenye chuki kubwa sana kwa wale waliokoka.

Sio ajabu mtu kuokoka akafukuzwa nyumbani ila wakati bado hajaokoka na anafanya uhalifu kwenye maeneo mbalimbali na wazazi wake au ndugu zake wakawa wanalijua hilo. Kuhusu huo uhalifu wake, hawakumfukuza nyumbani ila waliposikia ameokoka na sasa amekuwa mtu mzuri, ndio wakati ambao wanachukia na kumfukuza nyumbani ama kumtenga kabisa na familia.

Unaweza ukaona ni jinsi gani shetani alivyo na hila zake pale mtu anapotangaza tu kuokoka kwake, lakini kabla hajaokoka anaweza akawa rafiki mzuri kwa ndugu zake. Siku akisema sasa nimeamua kuachana na haya mabaya na kumpokea Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wa maisha yake, inakuwa kesi kubwa sana.

Sio kana kwamba ni vibaya kuokoka, na sio kana kwamba nakueleza haya ili kukutisha na kukufanya uanze kuogopa kuwa mkristo, au uanze kuuona ukristo ni mbaya. Nataka ujifunze hili ili unapokutana na ugumu wowote uwe unajua ni kwanini unakutana nao.

Unaweza ukawa na marafiki zako wazuri sana mnaoshirikiana kwa mambo mbalimbali, hadi yale yasiyompendeza Kristo, lakini ukawa na furaha nao na wao wakawa na furaha na wewe.

Siku utakaposema umeokoka na hutoshirikiana nao kwenye baadhi ya maeneo ambayo yanamkosea Mungu wako, ni sawa na umetangaza kuvunja urafiki nao. Unageuka adui yao mkubwa ambapo wanaweza hata wao wasijue sana ni kwanini umegeuka mtu mbaya kwao, kumbe ni shetani anawatumia.

Elewa kuokoka kwako na kuanza kuishi maisha yanayompendeza Mungu wako, ujue kwamba hutoepuka kuudhiwa. Haijalishi uhusiano wako na Mungu upo vizuri sana, uwe unajua hili hutoliepuka kwenye maisha yako ya wokovu.

Rejea: Naam, na wote wapendao kuishi maisha ya utauwa katika Kristo Yesu wataudhiwa. 2 TIM. 3:12 SUV.

Tena usipokuwa na Neno la Mungu la kutosha unaweza kufika mahali ukaukatia tamaa ukristo wako, ukaanza kuona ni tabu kwako badala ya baraka kwako.

Ujue kwamba ukristo sio tambarare, shetani hapendi kabisa njia uliyochagua uende nayo, atakuletea kila aina ya maudhi kwako, hata wazazi wako waliokuzaa wanaweza kugeuka kwako. Wakawa ni sababu ya wewe kuudhika kila wakati, bila kujijua kuwa wanatumika.

Ndugu yangu umechagua fungu jema kabisa la kumpokea Yesu Kristo, pamoja na umechagua fungu jema kuudhiwa kwako kutakuwepo sana. Unaweza ukaona bora ya maisha ya dhambi maana yenyewe hayana maudhi kama unayoyaona, japo yapo ila huwezi kuyaona sana maana ufahamu wako unakuwa umefungwa wakati huo.

Huenda leo nimekufundisha somo gumu kidogo ila fahamu kwamba ni somo muhimu sana la kukusaidia katika maisha yako ya wokovu au katika utumishi wako. Uwe unajua kuudhiwa kwa mtu aliyeokoka ni jambo ambalo haliepukiki kwake, hata kama atajitahidi kila namna ila ajue atakutana tu na maneno ya kuudhiwa kwake.

Ndio maana ni muhimu sana kwa mkristo kuwa na Neno la Mungu la kutosha moyoni mwake, bila kuwa na Neno la Mungu la kutosha atafika mahali atazidiwa na maneno yanayomshambulia. Lile Neno la Mungu ambalo lilipaswa limsaidie linakuwa halimo ndani yake, kwahiyo anabaki anahangaika tu.

Wewe usiwe hivyo, hakikisha unasoma Biblia yako kila siku, hujui mistari ya biblia unayosoma sasa hivi itaenda kukusaidia mahali gani. Unaweza ukaona haina sana umhimu wakati huo ila utafika mahali itaonekana umhimu wake mkubwa tu.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com