Kutokana na mambo mabaya ambayo watumishi wa Mungu wengi wanakutana nayo, baadhi yao hufika mahali na kuona labda Mungu amewaacha au labda kuna mahali wanakosea katika huduma zao.

Lakini ukija kwenye uhalisia kabisa, uhusiano wao na Mungu upo vizuri kabisa na hakuna jambo lolote walilomkosea Mungu wao. Isipokuwa katika huduma mambo mabaya hutokea watumishi, kinachohitajika ni uvumilivu haswa.

Bila kuwa mvumilivu utafika mahali utaacha huduma uliyopewa na Mungu, kama ni kuhubiri utaacha, kama ni kufundisha Neno utaacha, kama ni utume utaacha, kama ni uchungaji utaacha, na kama ni uimbaji utaacha.

Badala ya kuwa na mwisho mzuri, unakuwa na mwisho mbaya katika huduma uliyopewa na Mungu, maana kile alichokupa Mungu unapaswa hadi unaingia kaburini uwe umekifanya vizuri. Hata yule unayemkabidhi kijiti unakuwa na uhakika kazi umeimaliza.

Rejea: Kwa maana, mimi sasa namiminwa, na wakati wa kufariki kwangu umefika. Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda. 2 TIM. 4:6‭-‬7 SUV.

Unapokuwa unatumika kwenye eneo ambalo Mungu amekuitia, usifikiri mabaya hayatakupata, utakutana nayo, cha msingi kwako ni kuwa mvumilivu. Yatakuja hayo mabaya na yataondoka yenyewe, maana Bwana yu pamoja nawe.

Rejea: Bali wewe, uwe na kiasi katika mambo yote, vumilia mabaya, fanya kazi ya mhubiri wa Injili, timiliza huduma yako. 2 TIM. 4:5 SUV.

Hapa mtume Paulo anamhusia Timotheo, anamweleza mambo ambayo atakutana nayo kwenye utumishi wake, maana alikuwa anajua lazima akakutane nayo kwenye huduma yake ya kuhubiri.

Ambapo Timotheo wa leo ni mimi na wewe, hili andiko linatuhusu kabisa, maana ni mambo ambayo lazima tukutane nayo kwenye utumishi wetu tulionao ndani yetu.

Huenda hujawahi kukutana na mambo mabaya kwenye huduma yako, hili andiko linakuandaa ili utakapokutana nayo uwe unajua ni jambo ambalo lipo na litapita. Cha msingi ni kulinda uhusiano wako na Mungu ili uumalize mwendo salama katika huduma uliyopewa na Mungu.

Kingine ambacho kinasisitizwa kwenye andiko hili ni kuwa na kiasi, ukiwa mtumishi wa Mungu unapaswa uwe na kiasi katika mambo yote. Kwa kuwa Roho Mtakatifu yumo ndani yako, atakusaidia kwenye eneo hili la kuwa na kiasi.

Lakini jambo la msingi ni kuwa na maarifa sahihi ya Neno la Mungu, bila kuwa na Neno la Mungu ndani yako la kutosha, hili la kuwa na kiasi litakuwa gumu kwako. Jambo ambalo sio zuri kwa mtumishi wa Mungu kukosa mwongozo sahihi  wa mwenye huduma aliyompa aifanye.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com