Kuna wakati huwa tunajisumbua sana tujulikane kwa watu, kama ni mwimbaji unataka kila mtu akutambue kuwa wewe ni mwimbaji, kama wewe ni mhubiri wa injili unahangaika kujulikana na kila mtu.

Mtu anaweza akawa anatumia muda mwingi sana kuwaza hilo, kuwaza kwake kunaweza kumfanya mpaka akawa anakwazika pale watu wanapoacha kutambua nafasi yake.

Mwingine anaweza akawa anakwazika pale anapoona wenzake wanapata nafasi zaidi kuliko yeye, au wenzake wanajulikana zaidi ya yeye. Anapoona hivyo anaona labda kuna mahali anakosea, kumbe ni wakati tu bado hujafika.

Ndugu yangu leo napenda nikufungue macho katika hili, ili uache kuwa mtumwa kwa kitu ambacho hupaswi kuwa mtumwa nacho. Bali unapaswa kuendelea kuweka bidii zaidi kwenye eneo ambalo Mungu amekuitia umtumikie.

Jambo lolote ambalo unalifanya wakati huu au siku zote, fahamu kwamba kile unafanya ndicho utakachovuna, haijalishi kwa sasa unaona mambo ni magumu. Haijalishi unaona watu hawakuoni kabisa kama unafanya la maana sana, elewa kile unapanda sasa upo wakati utavuna matunda yake.

Kama umeweka nguvu zako zote kwa Mungu, umeweka moyo wako wote kwenye huduma yako, umeweka akili zako zote kwenye utumishi wako. Fahamu kwamba utavuna matunda ya bidii yako kwenye utumishi wako kwa Mungu.

Chochote unachokifanya kiwe kwa uzuri au kwa ubaya, kiwe kwa unyonge au kwa uimara, uwe na uhakika utavuna matunda ya kile ambacho ulikuwa unakipanda. Unaweza usione matokeo yake haraka ila fahamu kwamba kanuni ya Mungu ni kuvuna kile upandacho.

Rejea: Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa cho chote apandacho mtu, ndicho atakachovuna. Maana yeye apandaye kwa mwili wake, katika mwili wake atavuna uharibifu; bali yeye apandaye kwa Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele. Wagalatia 6:7-8.

Ndugu usijaribiwa na eneo hili, eneo ambalo lazima uvune matunda ya kile unafanya, inawezekana kabisa watu hawakuoni kabisa kuwa wewe ndiye unayejitoa sana kwenye eneo fulani. Fahamu kwamba ipo saa yako ya kuvuna kile ambacho ulikuwa unapanda kwenye maisha yako yote.

Inawezekana kabisa ni mwalimu mzuri sana wa Neno la Mungu, lakini hapo kanisani kwako hawana muda na wewe, hilo lisikupe shida kabisa. Endelea kutumika kwenye maeneo ambayo yana uhitaji, endelea kuchochea karama yako kila siku.

Nakueleza ukweli kupitia maandiko haya, utavuna kwa wakati wake, tena utavuna angali u hai bado, utaona matunda ya bidii yako katika huduma uliyopewa na Mungu.

Rejea: Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho. Kwa hiyo kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema; na hasa jamaa ya waaminio. Wagalatia 6:9-10.

Usije ukazimia moyo ukaacha kutenda mema, ukaacha kuwasaidia wengine kile ulikuwa unawasaidia, ukaona pamoja na kutoa sana msaada wako, pamoja na kutoa sana muda wako. Bado unaonekana hakuna ulichokifanya kabisa.

Ndugu fahamu kwamba utavuna matunda ya kujitoa kwako, haijalishi ni jinsi gani watu wanafanya kama hawakuoni kabisa, haijalishi wale uliowatendea mema wao wakaja kukutendea ubaya. Kwenye kumbukumbu zako uwe unajua upo wakati wako wa kuvuna.

Leo unasoma sana Biblia yako, kila siku lazima usome Neno la Mungu, hakuna siku inapita bila kusoma Biblia yako, unafika mahali unaona kama vile hakuna ulichokifanya. Ndugu nakueleza ukweli, kipo kitu umekifanya kikubwa sana, na matunda ya kusoma kwako biblia lazima uyavune ya kutosha.

Kile ambacho unatumia muda wako kukifanya ndicho kitu unachokipanda, wakati wake wa kuvuna matunda ukifika, lazima uvune hayo matunda. Kama ni mazuri ulipanda utavuna mazuri, na kama ni mabaya ulipanda utavuna mabaya.

Kile Mungu amekupa ndani yako, kitumikie kwa uaminifu wako wote, upo wakati utafika utavuna matunda ya uaminifu wako kwenye kile ulikuwa unajibidiisha nacho.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com