
Kwenye nyumba ya Mungu, Mungu ameweka watu tofauti tofauti, kila mmoja ana kazi yake, kila mmoja anafaa kwenye eneo fulani ambalo Mungu amemchagua. Ambapo kila mmoja akitambua nafasi yake na kuisimamia vizuri, mambo yataenda vizuri kabisa.
Kila kiungo ndani ya kanisa kinafaa kwenye eneo lake, hata yale maeneo ambayo hayaonekani sana kwa watu, au hata kama wale wanaofanya kazi hayo maeneo. Hawaonekani sana kwa watu, pamoja na kutoonekana kwao ni viungo muhimu sana vya kanisa.
Leo tuangalie kundi hili la wanawake wazee, kundi hili lina kazi moja kubwa sana kuwafunza wanawake vijana, ambao wameshaingia kwenye ndoa na ambao bado hawajaingia kwenye ndoa ila wana muda mchache kuingia humo.
Kabla ya kuangalia kazi haswa ya wanawake wazee kwa wanawake vijana, hebu tuone hawa wanawake wazee wanapaswa kuwaje kwanza. Maana wasipokuwa na sifa hizi hawapaswi kufanya kazi ninayokwenda kukueleza kupitia somo hili.
Kwanza kabisa, mwanamke mzee anapaswa awe na mwenendo wa utakatifu, maisha yake ya wokovu yanapaswa kuwa safi. Maisha yanayompendeza Mungu, sio maisha yasiyompendeza Kristo, ndivyo anapaswa kuwa mwanamke mzee aliyeokoka.
Pili, mwanamke mzee anapaswa asiwe msingiziaji, yule mtu ambaye anasingizia vitu ambavyo hana ushahidi navyo, wala hana uhakika navyo. Anaweza kumtwishwa mpendwa wa kanisani jambo ambalo hajalifanya kabisa, anaweza kusema fulani ni mwizi ila ki uhalisia sio mwizi kabisa na ana uhakika hana tabia hiyo.
Tatu, mwanamke mzee hapaswi kuwa mtu anayekunywa pombe, mwanamke huyu mzee ili afae kwenye kazi hii ninayokwenda kukueleza hapa. Hapaswi kabisa kuwa mlevi, akiwa mlevi anakosa sifa njema ya kuwasaidia wengine.
Nne, mwanamke mzee anapaswa kuwa mtu anayefundisha mema, mambo ambayo akiyapata binti ambaye bado hajaanza maisha ya ndoa. Anapata maarifa sahihi ya kumsaidia kwenye maisha yake ya usichana, hata pale anapotaka kufanya maamzi ya nani awe mume wake inakuwa rahisi kwake.
Baada ya kuona hivyo vipengele vinne, hebu tuone mwanamke mzee huyu anapaswa kufanya nini, huyu mwanamke mzee anapaswa kuwa mwalimu mzuri kwa mwanamke kijana.
Wanawake wazee wana jukumu kubwa sana la kuhakikisha wanawafundisha wanawake vijana jinsi ya kuishi na waume zao, wanawake vijana bila kupewa elimu sahihi kutoka kwa wanawake wazee. Ndoa za mabinti hawa ambao ni wanawake vijana, hazitakuwa salama sana.
Kazi kubwa haswa wanayotakiwa kuifanya kwa wanawake vijana ni kuwafundisha kuwapenda waume zao, na kuwapenda watoto wao. Sio kila mwanamke kijana anayeingia kwenye ndoa anakuwa anajua umhimu wa kumpenda mume wake au kumtii mume wake.
Na sio kila mwanamke kijana anayezaa watoto wake ndani ya ndoa, atakuwa anaelewa kuwa anapaswa kuwapenda watoto wake. Wapo wanawake hawana upendo kabisa kwa watoto wao, unaweza kushangaa kama hujawahi kukutana na hilo ila fahamu haya yapo.
Biblia ipo wazi kuhusu hili ninalokuambia hapa, usifikiri ni maneno tu, maandiko yameweka wazi hili na kutoa maelekezo sahihi namna anavyopaswa kufanya mwanamke mzee.
Rejea: Vivyo hivyo na wazee wa kike wawe na mwenendo wa utakatifu; wasiwe wasingiziaji, wasiwe wenye kutumia mvinyo nyingi, bali wafundishao mema; ili wawatie wanawake vijana akili, wawapende waume zao, na kuwapenda watoto wao. TIT. 2:3-4 SUV.
Kazi kubwa kwa wanawake wazee ni kuhakikisha hili jukumu wanalitekeleza kama wazazi, bila kuwapa elimu ya kutosha binti zao. Watajikuta wanapata shida kubwa kwenye ndoa zao, wanaweza kuona wanaume hawawajali kumbe wao ndio chanzo ya yote.
Wanawake vijana lazima wapewe elimu ya kutosha namna ya kuwapenda waume zao, watafurahia sana maisha yao ya ndoa zao. Tofauti na wakiwa hawana elimu yeyote kuhusu ndoa zao, watakuwa ni wanawake wasio na furaha ndani ya ndoa zao.
Kama unasoma ujumbe huu na ni mwanamke ambaye ni mzee na umeokoka, hili somo linakuhusu kabisa, na kama unasoma ujumbe huu na bado wewe ni mwanamke kijana. Utakuwa umepata elimu ya kukusaidia kwa baadaye, na kama unasoma ujumbe huu na sio mwanamke, utakuwa umepata maarifa ya kumsaidia mke wako au mwanamke mwingine ili awe mwalimu mzuri wa mabinti.
Hii ndio faida ya kusoma Neno la Mungu kila siku, unakutana na maarifa sahihi ya kukusaidia katika maisha yako ya wokovu, unakuwa upo vizuri kiroho na kimwili. Adui anakosa nafasi ya kukuihangaisha katika maisha yako, maana wakati mwingine adui anatutabisha sana kwa kukosa maarifa sahihi ya Neno la Mungu.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com
+255759808081