Wapo watu wamekuwa sehemu ya kusababisha maumivu na majuto kwa wengine, wamekosa kabisa jambo zuri la kuwatendea wengine. Zaidi sana wamegeuka miiba kwenye maisha ya watu, na wamekuwa hawaoni kama wanafanya vibaya.

Wapo wengine wamekuwa sehemu ya kuwafanya wengine wakose haki zao, wamesimama kama ukuta mkubwa wa kuzuia watu wengine wasipate kile ambacho walikuwa wanastahili kupata. Hii ni kutokana na kutumia nafasi zao vibaya.

Wakati wengine wanaonyesha ubaya wao kwa wengine, wapo watu wamekuwa sehemu ya kusababisha furaha nyingi kwa watu. Na wapo wamekuwa sehemu ya kuleta faraja kwa wengine.

Kuna watu walishakata tamaa kabisa ya maisha ila kupitia watu hawa wenye upendo wa kiMungu ndani yao, wamesababisha kule kukata tamaa kwa wengine. Wamegeuza kuwa furaha na faraja ndani yao, kule kukata tamaa kumetoweka kutokana na upendo mkubwa walionyeshwa na hawa ndugu wazuri.

Wapo watu wengine walishafika mahali na kuona hakuna watu wazuri wenye upendo wa kweli, kupitia wao wamewafanya watu hao kuona kuwa dunia bado ina watu wazuri kabisa.

Unaweza ukajiuliza wewe binafsi, umekuwa sehemu ya maumivu kwa wengine kutokana na roho yako mbaya au umekuwa sehemu ya furaha na faraja kwa wengine kutokana na upendo mkubwa ulionao?

Jibu unaweza ukawa nalo kabisa, maana wewe unajifahamu vizuri tabia yako ilivyo na dhamira yako inakushuhudia vile ulivyo kwa wengine. Hii tunajifunza kupitia maandiko matakatifu, tunaona vile Filemoni alikuwa sehemu ya kusababisha furaha nyingi na faraja kwa mtume Paulo, kwa sababu ya upendo wake Filemoni.

Rejea: Maana nalikuwa na furaha nyingi na faraja kwa sababu ya upendo wako, kwa kuwa mioyo ya watakatifu imeburudishwa nawe, ndugu yangu. FLM. 1:7 SUV.

Sio tu Paulo peke yake, na watakatifu wengine waliburudishwa na Filemoni, inaonyesha ni jinsi gani mtu huyu alikuwa baraka kwa wengine kutokana na upendo wake wa Kristo ndani yake.

Jambo la kumletea sifa na utukufu Bwana Yesu, ni ikiwa utakuwa sehemu ya kusababisha furaha na faraja kwa wengine kutokana na upendo wako ulionao juu yao. Watu wengi sana watatamani kumjua Mungu wako kutokana na matendo yako mazuri kwao.

Tofauti kabisa na yule mtu ambaye ameokoka alafu bado tabia yake inawafanya watu wengine waendelee kujuta kwa sababu ya kumfahamu yeye. Wakati watu wanapaswa kumtukuza Mungu kwa sababu ya kukutana na mpendwa kama huyo mzuri.

Hebu kupitia somo hili usiache kuwa furaha na faraja kwa wengine kutokana na upendo mkubwa wa Kristo ulionao ndani yako, watu watatafuta kujua siri ya mafanikio yako ni nini kupitia yale unayatenda na watu wanabarikiwa kupitia wewe.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com