Tunaweza kuuchukulia wokovu ni jambo la kawaida sana, wokovu ambao umepatikana kwa gharama kubwa sana, tukauona kuwa ni jambo la kawaida kwetu. Tukawa tunafanya vile tunajisikia kufanya, bila kujali tunamkosea sana Mungu wetu kwa yale tunayofanya.

Wakati mwingine tunaweza kuona Mungu hawezi kututupa jehanamu ya milele, kwa sababu anatupenda sana, tukawa na fikira hizo ndani mwetu na tukaendelea kufanya machukizo mbele zake zaidi.

Pamoja na kuchukulia wokovu wa kawaida sana, kwa kufikiri huna haja ya kumpokea Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wako, huna haja ya kuishi maisha yanayompendeza Mungu, huna haja ya kuhofu siku ya hukumu.

Huwezi kupona kwa kuuchukulia wokovu kawaida, ipo siku itafika utataka kusikia habari njema za Yesu hutokuwa na hiyo nafasi, ipo saa utatamani kumkiri Bwana Yesu kwa kinywa chako. Nafasi hiyo haitokuwepo kamwe wakati huo.

Wapo wengine wanaweza kudharau wokovu na kuiona dunia ni ya maana sana kwao kufanya wanachotaka, wakawa wanafanya mambo ambayo ni chukizo mbele za Mungu. Wakifikiri wapo salama sana, ipo saa watajutia kutumia nafasi zao vibaya.

Hakuna mtu atakayeweza kupona kwa kuupuzia/kudharau wokovu mkuu, uliopatikana kwa gharama kubwa sana, ambapo kwa sasa mtu anaweza kuupata bure kabisa na kwa hiari yake mwenyewe. Hakuna anayelazimishwa isipokuwa kwa kuamua mwenyewe kwa hiari yake.

Ndivyo maandiko yanavyotuhoji sisi wanadamu, je! Tutawezaje kupona tusipojali wokovu mkuu namna hii? Kwa kweli itakuwa ngumu sana kupona ikiwa hatutajali wokovu mkuu.

Rejea: Sisi je! Tutapataje kupona, tusipojali wokovu mkuu namna hii? Ambao kwanza ulinenwa na Bwana, kisha ukathibitika kwetu na wale waliosikia. EBR. 2:3 SUV.

Tunza sana maisha yako ya wokovu, usiishi kama mtu asiyeelewa yeye ni nani, ishi kama mtu anayejua amebeba nini ndani yake, au amepokea nini kwenye maisha yake. Ukishajua wokovu ni wa kujali sana, hutafika mahali ukapotea njia labda wewe uruhusu hilo.

Hakikisha unajali sana wokovu wako, hiyo ni tiketi yako ya kuingia mbinguni, maana ukiujali sana wokovu ulionao hutoiba, hutozini, hutomtukana mtu, hutomseng’enya mtu, kwa kifupi hutofanya jambo lolote lile linalomkosea Mungu wako kwa makusudi.

Mungu akupe neema ya kujua thamani ya wokovu wako, ukishajua utakuwa makini sana katika tembea yako hapa duniani, maana utakuwa unajua ulichopokea na ulichobeba ni cha thamani sana kuliko vyote.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com