
Katika eneo ambalo linawazuia wengi wasisamehewe makosa yao, ni eneo hili la kutosamehe wale waliowakosea katika maisha yao, maana kwao limekuwa jambo gumu kusamehe wale waliowakosea katika maisha yao. Kutokana na uzito wa jambo lenyewe walilokosewa na hao watu ambao hawataki kuwaachilia mioyoni mwao.
Tena wengi hawajui kuwa kutokusamehe inaumiza zaidi kuliko angesamehe na kuachilia, mtu anaweza kufikiri kutomsamehe yule aliyemkosea ni kumkomoa. Lakini ukija katika uhalisia, anayeumia zaidi ni yule ambaye hajasemehe.
Kumsamehe aliyekukosea ni ufunguo wako wa kukufungulia eneo litakalokufanya usikilizwe na Mungu na akishakusikiliza atakusamehe yale makosa yako yote. Tofauti ukiwa unaenda mbele za Mungu kuomba msamaha ukiwa wewe mwenyewe hujasamehe yule aliyekukosea.
Ukiangalia ni kama Mungu ametuwekea zoezi gumu sana au ametupa mashrati magumu sana, maana ukiangalia yule aliyekukosea hakustahili kabisa kusamehewa kirahisi hivyo kutokana na kosa alilokufanyia.
Lakini pamoja na uzito wa kosa alilokufanyia, Mungu anakutaka umsamehe kwanza kabla hujaenda mbele zake, inaumiza sana ila hakuna namna lazima usamehe yule aliyekukosea.
Rejea: Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. MT. 6:14 SUV.
Unaweza kusema hayo ni maneno tu, au ukaanza kusema kimoyo moyo kuwa huyu anayeandika haya hajui vile inaumiza ukikosewa na mtu, au unajiambia kuwa huyu anayeandika haya hajui tu kuna makosa mengine ni nyeti sana.
Akiwa na maana kuwa yapo makosa huwezi kumsamehe mtu hivi bila kumlipiza kisasi, na ukiangalia kibinadamu unaona ni jambo ambalo ni gumu kweli. Lakini kwa kuwa tumeokoka, na Yesu Kristo yupo ndani yetu na sisi tupo ndani yake, uchungu wa kushindwa kusamehe unawezaje kukaa ndani yako?
Utaona ni jambo ambalo haliwezi kupata nafasi kwa mtu aliyeokoka sawasawa, tena mwenye Neno la Mungu la kutosha moyoni mwake. Ni vigumu sana kuhangaika na mtu ambaye amemkosea miezi kadhaa iliyopita au miaka kadhaa iliyopita.
Tena Mungu mwenyewe anatuzuia kulipiza kisasi kupitia Neno lake, kazi ya kulipiza kisasi ni ya kwake mwenyewe, kazi yako ni kuendelea kuishi maisha yanayompendeza yeye. Kweli kabisa utaona Mungu akifanya malipizi kwa wale ambao walikutendea mabaya na hawakutaka kubadilika.
Rejea: Wapenzi, msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana imeandikwa, Kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena Bwana. Warumi 12:19.
Ndugu yangu kama umekaa unapanga kulipiza kisasi juu ya mtu fulani, awe ndugu yako, awe rafiki yako, au awe jamaa yako yeyote yule wa karibu. Nikuambie tu ukweli kuwa utakuwa unakosea sana, kazi ya kulipiza kisasi ni ya Bwana peke yake.
Hakikisha unasamehe wale wote waliokukosea kwenye maisha yako, kufanya hivyo inakuondolea mzigo ndani yako na ikakufanye upatane na Mungu. Unapomwendea Mungu kumwomba akusamehe mahali ulimkosea, atakuwa na nafasi ya kukusamehe kabisa makosa yako.
Mungu akubariki sana.
Ndugu Yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com