
Mtu anapookoka siku za mwanzo kabisa anahitaji kupata mafundisho ya awali kabisa ya kumsaidia kuukulia wokovu, mafundisho hayo yanamjengea msingi mzuri wa kumsaidia kuendelea na safari yake aliyochagua katika maisha yake.
Mtu huyo aliyeokoka siku za karibu sio wakati wote atakuwa wa kufundishwa tu, atatakiwa na yeye akafundishe wengine baada ya kukomaa au baada ya kupewa maarifa sahihi ya kutosha ndani yake. Hatua hiyo inamtosha kabisa kuwagawia na wengine kile kidogo alichopata ndani yake.
Haipaswi kuwa mtu wa kufundishwa tu kila siku, bila kuchukua hatua zozote za kuonyesha na yeye amekomaa anahitaji kuwafundisha na wengine yale muhimu yatakayowafanya wamjue Yesu Kristo kwa undani zaidi.
Tofauti yake ni kwamba, wapo watu wengi wameokoka siku nyingi sana ila ule uwezo wa kumshuhudia mwingine au kumfundisha mwingine Neno la Mungu inakuwa ngumu kwao. Sio kana kwamba wanajifanyisha hapana, ni jambo wasiloliweza kweli.
Watu wa namna hii ni wale ambao wanapenda sana mafundisho laini, yaani maziwa, wala hawapendi chakula kigumu. Mafundisho yao wanayoyataka kila siku ni yale yale, tena yale yasiyowagusa maisha yao mengine yasiyompendeza Kristo.
Hebu wewe fikiria muda ulionao sasa tangu uokoke, je huwezi kabisa kumfundisha mwingine Neno la Mungu? Mafundisho yote uliyonayo ndani yako hayawezi kweli kukufanya usimame kwa ujasiri mkubwa kabisa na kumweleza habari za Yesu Kristo kwa usahihi?
Utaona ni jambo ambalo haliwezekani kabisa kwa muda mrefu ulionao ndani ya wokovu, sema changamoto hiyo unayo kutokana na kupenda maziwa tu. Hutaki kula chakula kigumu, na maziwa ni chakula cha watoto, mtu mzima hawezi kupata nguvu za kufanya kazi kwa kunywa tu maziwa.
Kama hadi sasa ukipewa nafasi ya kufundisha Neno la Mungu unaanza kujiuliza utasema nini, au ukakosa kitu cha kufundisha kabisa, ujue una shida. Umri ulionao ndani ya wokovu hupaswi kukosa kitu cha kuwashirikisha watu.
Rejea: Kwa hakika, ingawa mpaka wakati huu ingewapasa kuwa walimu, bado mnahitaji mtu wa kuwafundisha tena hatua za awali za kweli ya Neno la Mungu. Mnahitaji maziwa, wala si chakula kigumu! Waebrania 5:12 NEN.
Hili andiko linatuthibitishia hili ninalokuambia hapa, wapo watu walipaswa kuwa walimu wa wengine ila sivyo hivyo ilivyotarajiwa, bali wanaonyesha bado wanahitaji kufundishwa. Tena sio yale mafundisho magumu, yale mafundisho ya awali kabisa.
Hebu tafakari mwenyewe utaendelea kupenda maziwa ya watoto wachanga hadi lini? Na utaanza lini kula chakula kigumu cha watu wazima? Unapaswa kukua kiroho ili uweze kuwa faida kwa wengine. Yesu anahitaji umzalie matunda mengi sana.
Acha uvivu wa kujifunza zaidi Neno la Mungu, kuwa na bidii katika kujifunza, tamani kutoka hatua moja kwenda hatua nyingine kubwa zaidi. Usibaki kwenye eneo la uchanga miaka nenda rudi.
Usomaji wako wa Neno la Mungu utoe matokeo mazuri kwako, tukuone ukiwa na ujasiri wa kuwaeleza wengine ukweli kupitia maandiko matakatifu. Bila kuwa na wasiwasi wowote na lile unalolinena kupitia kinywa chako.
Usibaki unasoma Biblia yako miezi yote au miaka yote bila kuwa na mabadiliko yeyote, hakikisha unakuwa mtu wa tofauti kabisa na kipindi hujaanza kusoma Neno la Mungu. Kusikiliza kwako mafundisho ya neno la Mungu kila wakati paonekane kupitia matendo yako.
Usibaki mtu wa kufundishwa miaka yote, ufike wakati na wewe uwe mtu wa kuwafundisha wengine, ifike wakati uwe na uwezo wa kujisimamia mwenyewe. Uondoke kwenye eneo la uchanga, uwe mtu aliyekomaa sawasawa na mwenye uwezo wa kujisimamia mwenyewe.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com