
Wasiwasi unaweza ukawa mwingi sana kwa mtu aliyetenda uovu mwingi, na aliyetenda dhambi nyingi mbele za Mungu, pale anapoenda kutubu na kuyaacha yote ya kale. Anaona kama vile Mungu bado hajamsamehe yale yote aliyowahi kutenda kabla ya kuokoka.
Huenda ukawa miongoni mwa hao watu wanaopata shida hii mioyoni mwao, au huenda una ndugu au rafiki ambaye ni mhanga wa hili. Ameokoka lakini bado anajiona ana hatia mbele za Mungu, akikaa muda mwingi unamwona hana raha kabisa.
Ukifuatilia kwa kumuuliza kitu gani kinachomsibu katika maisha yake, atakueleza kuwa kutokana na mambo aliyowahi kutenda huko nyuma kabla hajachukua maamzi ya kuokoka. Mambo hayo anaona kabisa bado Mungu hajamsamehe japokuwa ametubu na kuyaacha yote.
Hebu jiulize swali rahisi tu, ingekuwa Yesu Kristo hawezi kusamehe maovu yetu na dhambi zetu, ilikuwa ina maana gani kutoa agizo la watumishi wake kuhubiri habari njema ulimwengu kote?
Rejea: Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. MK. 16:15-16 SUV.

Yesu alikuwa na haja gani ya kutoa agizo la kuhubiri habari njema ulimwengu kote, ilikuwa na haja gani kutoa nafasi ya kutubu? Ni maswali mepesi yenye tafakari nzito ya kuweza kukusaidia kutoka kwenye kifungo cha kufikiri bado hujasamehewa.
Kujiuliza hayo maswali inaweza kukusaidia katika kumpa majibu sahihi mwenye shida hii ya kufikiri bado hajasamehewa makosa yake. Yale maovu na zile dhambi alizokuwa anazifanya, akizipima kibinadamu anaona kabisa bado Yesu hajamsamehe.
Mtu wa namna hiyo ni rahisi sana kurudi nyuma tena baada ya kuokoka au baada ya kumkiri Kristo kama Bwana na mwokozi wake, au baada ya kutubu dhambi zake. Kufikiri kwake bado hajasamehewa anaona ni heri kurudia maisha yake ya zamani.
Unapaswa kufahamu Yesu Kristo anasamehe kabisa, sio kusamehe tu, hatazikumbuka tena dhambi zako, au hatazikumbuka tena dhambi za mtu aliyemsamehe.
Rejea: Kwa sababu nitawasamehe maovu yao, Na dhambi zao sitazikumbuka tena. EBR. 8:12 SUV.
Wale marafiki zako uliokuwa nao kwenye mambo mabaya yasiyofaa mbele za Mungu, wasikutaabishe na maneno ya kukukejeli/kukukebehi kuwa bado wewe ni mwenye dhambi mbele za Mungu.
Wakitazama historia yako, au wakitazama yale matendo yako ya nyuma uliyokuwa unafanya nao au uliyokuwa unawafanyia watu, wanaona Mungu hawezi kukusamehe kabisa kutokana na uzito wa matukio uliyowahi kufanya.
Kama umeamua kuachana nayo na kumrudia Yesu Kristo kwa kumaanisha kutoka ndani ya moyo wako, amini kwamba umesamehewa siku ile ile uliyoamua kutubu dhambi zako. Na kuanzia siku hiyo Yesu hazikumbuki tena dhambi zako.
Vyema ukafurahia kuokoka kwako, vyema ukamsaidia mwenzako anayepitia changamoto hiyo kumweleza ukweli kuwa Yesu Kristo hakumbuki tena dhambi zake. Hata kama wapo watu wanamtia hofu, mwambie amesamehewa na aendelee mbele.
Hii ndio faida ya kusoma Neno la Mungu, maana kadri unavyozidi kujifunza zaidi ndivyo unavyozidi kujua zaidi, unavyozidi kujua unaacha kuhangaishwa na mambo kama haya. Huko ndio kukua kiroho kwa mwamini, anatoka kwenye utumwa wa kuhangaishwa na watu wenye mitazamo potovu.
Hakikisha unasoma Neno la Mungu kila siku inayokuja kwenye maisha yako, bila kujalisha mazingira mazuri au mabaya, tafuta kila namna ya kupenya ili upate chakula cha roho yako angalau kwa dakika ambazo Mungu atakujalia wakati huo kuwa nazo.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com