Kila mmoja anaomba Mungu, haijalishi tunatofautiana viwango vya kukaa kwenye maombi, maana wapo wanaweza kuomba masaa mengi na wapo wanaweza kuomba masaa machache. Lakini wote ni waombaji wanaopeleka mahitaji yao mbele za Mungu.

Kuomba ni sawa tunaomba, je tunaomba kwa imani? Je tukishaomba tunakuwa hatuna mashaka? Jibu lake unaweza ukawa nalo. Kama huwa unaomba Mungu akusaidie mambo fulani utakuwa unajifahamu kiwango chako cha imani, na utakuwa unajua huwa unaona shaka ama la.

Changamoto ambayo inawakabili watu wengi waliomkiri Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wao, huwa imani yao kwa Mungu haipo, wanakuwa na mashaka sana kwa kufikiri wanavyofikiri wao.

Ili uweze kupata msaada wa Mungu juu ya jambo lile linalokusumbua kwenye maisha yako, unapaswa uwe na imani juu uweza wa Mungu, na hupaswi kuona shaka yeyote. Usipokuwa na imani na ukawa unaona shaka juu ya Mungu, maombi yako hayatazaa matunda uliyoyatarajia.

Hakikisha imani yako inajengeka vizuri juu ya Bwana Yesu, na usiwe na mashaka au shaka yoyote juu ya kile ulichomwomba. Wewe amini tu, ajibu siku hiyo hiyo, ama ajibu mwaka ujao, tunachopaswa kufanya ni kuendelea kutulia mbele zake.

Rejea: Ila na aombe kwa imani, pasipo shaka yo yote; maana mwenye shaka ni kama wimbi la bahari lililochukuliwa na upepo, na kupeperushwa huku na huku. Maana mtu kama yule asidhani ya kuwa atapokea kitu kwa Bwana. YAK. 1:6‭-‬7 SUV.

Unaona hilo andiko linavyosema hapo? Linaonyesha wazi kabisa kuhusu hili somo ninalokulekeza hapa, ndivyo ilivyo hata sasa kama huna imani mbele za Mungu shida yako utakayompelekea haitajibiwa.

Kupitia hili somo unaweza kuona ni jinsi gani ilivyo muhimu sana kujifunza Neno la Mungu, utaona matunda yake kwa kile umefanya katika maisha yako. Nakusihi sana usome Neno la Mungu kila siku bila kukoma ili likujengee imani ya kweli.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest
www.chapeotz.com