Jina tulilonalo na tuliloliamini katika maisha yetu ya wokovu, yaani jina la Yesu Kristo, shetani naye anaamini yupo na anatetemeka. Anajua uweza wa Mungu ulivyo mkuu, ndio maana unapokemea pepo wachafu wanamtoka mtu kwa kulitumia jina la Yesu Kristo.

Uweza wa Mungu wetu ni mkuu sana, kila kiumbe chini ya jua kinasujudu mbele zake, haijalishi kinatisha sana au kinaogopesha sana. Uweza za Mungu ni mkuu sana kuliko vyote, kuliko miungu mingine, kuliko chochote kile unachokijua au kukisikia.

Ikiwa mashetani yenyewe yanaamini na kutetemeka juu ya Mungu wetu, kwanini usijivune na kujua uliyenaye ndani yako ni mkuu sana. Haijalishi watu wanakuambia vile shetani na mawakala wake wanavyofanya kazi, bado wanasaluti mbele za Mungu.

Kuokoka kwako na kumwamini Yesu Kristo, maisha yako yapo salama kwa asilimia zote, ikiwa njia zako hutozichanganya ujue jambo lolote baya litakalokupata litakuwa limepata kibali kwa Mungu.

Wakati unaendelea kumwamini Mungu na kumtumikia kwenye maeneo tofauti tofauti, ujue shetani ana tetemeka sana juu ya Mungu. Anajua nguvu aliyonayo Mungu wetu, tena anaamini yupo na ana tenda kazi.

Rejea: Wewe waamini ya kuwa Mungu ni mmoja; watenda vema. Mashetani nao waamini na kutetemeka. YAK. 2:19 SUV.

Sijui sana imani yako mbele za Mungu ikoje, ikiwa imani yako ipo imara au unamwamini ila njia zako sio sahihi, unapaswa kuelewa uwezo alionao Mungu ni mkuu sana kutokana na tunavyosoma habari zake.

Usitishwe na mganga wa kienyeji au mchawi, ulichobeba ndani yako kina thamani kubwa sana, tena Shetani anatambua hili ndio maana anaamini na kutetemeka kwake.

Kama wewe humwamini Mungu, mashetani yana mwamini na kutetemeka kwake, sasa wewe ni nani ushindwe kumwamini Mungu? Yeye ni Alfa na Omega. Anakujua vyema kuliko wewe mwenyewe unavyojijua.

Hii ndio faida ya kusoma Neno la Mungu kila siku, unakutana na maneno ambayo yanaweza kukuvusha sehemu moja kwenda nyingine. Kama hivi ulikuwa hujui kama mashetani yanamwamini Mungu na kutetemeka, kupitia usomaji wako unaweza kutambua mengi sana.

Usiache kusoma Neno la Mungu kila siku, ipo faida kubwa sana kwako, kile kidogo kinachoingia moyoni mwako, ndicho kinaweza kuwa msaada mkubwa kwenye maisha yako yajayo.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com